Home KitaifaBiashara TPA Yanasa Mtandao Wizi wa Mafuta

TPA Yanasa Mtandao Wizi wa Mafuta

by Jamhuri
Serikali wilayani Kigamboni na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wanasema wamepata taarifa za kuwapo watu wengine wanaoiba mafuta kutoka kwenye bomba kuu katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hatua hii imekuja baada ya kukamatwa kwa watu watano ambao ni mmiliki wa nyumba na wapangaji wanne katika eneo la Tungi wilayani humo, wakiwa wameunga mabomba kutoka kwenye bomba kuu la mafuta ya dizeli linalotoka melini hadi kwenye matangi ya kuhifadhia nishati hiyo.
Mmiliki wa nyumba hiyo, Samwel Nyakirang’ani (63), anatajwa kuwa ni mtumishi mstaafu kwenye sekta ya mafuta.
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, ameliambia JAMHURI kuwa tayari wamepata taarifa za kuwapo watu wengine waliojiunganishia mabomba ya mafuta kutoka kwenye bomba kuu.
“Tumepata taarifa hizo na vyombo vyetu vya uliunzi na usalama vinaendelea na kazi, wametoboa mabomba katikati kutoka kwenye eneo la meli hadi kwenye deport. Tunaomba wananchi wenye taarifa waendelee kushirikiana na sisi kuwapata wahujumu wote,” amesema Mgandilwa.
Anasema kiwango cha mafuta kilichoibwa na watuhumiwa waliokwishakamatwa hakijajulikana, lakini akasema; “Itakuwa ni mafuta ya mamilioni ya shilingi kwa sababu ni mengi na wizi umefanywa kwa muda mrefu.”  
Mmoja wa wafanyakazi wastaafu wa TPA aliyekuwa kwenye sekta ya mafuta, ameliambia JAMHURI kuwa wezi wakuu wa mafuta ni genge la watumishi wanaoshirikiana na viongozi waandamizi serikalini.
“Wizi huu si kazi ya watumishi wa kawaida, ni kazi ya watu wakubwa sana serikalini. Tunaogopa kuwasema kwa sababu wanaweza kutuua. Watu wanapata fedha nyingi sana, ni mabilionea kwa kazi hii hii ya wizi wa mafuta.
“Tulishauri pale kwenye bomba kuwe computerized ili mtu aki-tamper mara moja ijulikane. Wakubwa hawataki teknolojia hiyo maana wanajua huo ndio mwisho wa wizi wao. Kuna watu wamejenga nyumba juu ya bomba hatujui humo ndani ya nyumba wanafanya nini, lakini ndiyo haya unayoyaona sasa.
“Kuna mtu amejenga ukuta ndani kuna mabomba yake. Haagizi mafuta, lakini anauza mafuta. Anatoa wapi?” Amehoji mstaafu huyo. 
 
Mwaka juzi, JAMHURI liliandika habari iliyohusu ufisadi na mwanya wa wizi wa mapato ya Serikali unaofanywa kwenye uingizaji nchini gesi, mafuta ya kula, mafuta ya magari, na mafuta ya viwandani kutokana na kupuuzwa kwa matumizi ya mita (flow meter).
Kwa kawaida TPA inatakiwa iwe na mita 16 kwa uhakiki wa kiwango cha shehena za mafuta ya aina mbalimbali yanayoingizwa nchini ili wahusika walipe kodi na ushuru. Pamoja na ukosefu huo wa mita, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI ulibaini kuwa shirika la Tanzania Italy Petroleum Refinery (TIPER)-ambayo ni ubia kati ya Tanzania na Italia, linahusishwa na hujuma hiyo.
TIPER ambayo hadi wakati huo ilikuwa haiagizi mafuta kutoka ng’ambo, imekuwa ikitumia moja ya kampuni maarufu nchini kuuza mafuta ambayo upatikanaji wake unahusishwa na wizi huo unaoendelea bandarini.
Waagizaji mbalimbali wa mafuta nchini wamekuwa wakilalamikia wizi huo, lakini duru za uchunguzi zimebaini kuwa hujuma hiyo imekuwa ngumu kukomeshwa kutokana na kuwashirikisha watu maarufu-miongoni mwao wakiwa katika idara nyeti na wengine ambao ni wastaafu serikalini.
Malalamiko kuhusu wizi wa mafuta yalianza kitambo, na hilo linathibitishwa na barua ya Novemba 7, 2012 ya Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER.
Barua hiyo iliitaka TIPER iondoe mara moja bomba lenye upana wa inchi 18 ililojiunganishia kinyemela. Barua hiyo ilikuwa ni majibu kutokana na barua ya TIPER ya Oktoba 12, mwaka huo iliyokuwa ikipinga agizo la TPA la kuitaka ifungue bomba ililojiunganishia.
Hata hivyo, JAMHURI lilibaini kuwa pamoja na ‘mrija’ huo, kuna ‘mirija’ mingine mitano yenye ukubwa mbalimbali ambayo TIPER imeiunganisha kwenye mabomba makuu yanayosafisha mafuta kutoka melini.
Vyanzo vya habari vilidokeza kuwa TIPER kwa kuhakikisha haiguswi, ilijijengea uzio mkubwa ambao hakuna mtu yeyote asiyehusika ailiyeruhusiwa kuingia ndani, wakiwamo wafanyakazi wa TPA.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliagiza ukuta huo uvunjwe na mabomba yaliyounganishwa yafunguliwe na Timu ya uchunguzi ya JAMHURI ilizuru eneo hilo na kukuta uboamaji wa ukuta ukitekelezwa na kujengwa seng’enge.
Wizi wa mafuta katika eneo hilo unathibitishwa na aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu katika Wizara ya Nishati na Madini, Injinia Paul Masanja.
Barua yake ya Novemba 26, 2015 kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, inaeleza upotevu wa mafuta mengi kutoka kwenye eneo ambalo meli zinatia nanga (SPM) na pia katika eneo la Kurasini Oil Jetty (KOJ).
Hatua ya Masanja ilitokana na kikao cha Desemba 2014 kilichohusisha kampuni zinazouza mafuta (OMC) kupitia kwa Mratibu wa Uagizaji Mafuta (PICL).
Kikao hicho kilijadili upotevu wa mafuta na kufikia suluhisho la kuunda Kamati kupata ufumbuzi wa kero hiyo.
Masanja, katika barua yake aliandika mapendekezo kadhaa, likiwamo la kuitaka TPA ishirikiane na TIPER kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye ‘mirija’ ya TIPER; jambo ambalo TPA walilipinga wakisema kampuni hiyo haikupaswa kushirikishwa kwa kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa wakuu wa wizi wa mafuta.
JAMHURI limeelezwa kuwa TPA kwa kushirikiana na vyombo vya dola imeanza uchunguzi mzito kuhakikisha wote wanaojihusisha na wizi wa mafuta wanatiwa mbaroni. “Tunaangalia na uwezekano wa kufukua bomba lote na kuweka jipya kabisa kama tulivyopata kufanya siku za nyuma pengine hii itasaidia,” amesema mtoa habari.
Juhudi za kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Injinia Deusdedith Kakoko hazikufanikiwa baada ya ofisi yake kulieleza JAMHURI kuwa yupo likizo na maofisa wengine waliishia kusema suala hilo linafanyiwa kazi katika ngazi ya juu.

You may also like