*Yadaiwa huo ni mzigo wa Ridhiwani, Home Shopping Centre

*Home Shopping wasema ni fitina za kibiashara, TRA wanena

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imenasa makontena 500 ya wafanyabiashara mbalimbali nchini, ambayo yamechanganya mizigo kwa nia ya kukwepa kodi ndani ya mwezi mmoja uliopita.

Taarifa zilizoifikia JAMHURI kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali jijini Dar es Salaam, zimedai kuwa makontena hayo ni ya kampuni ya Home Shopping Centre wenye kusaidiwa na mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete, lakini Home Shopping Centre wamekanusha taarifa hizo wakisema ni fitina za kibiashara.

 

Hivi karibuni, Ridhiwani naye amehojiwa na JAMHURI na kati ya mambo aliyokanusha ni kuwa na hisa kwenye kampuni za Home Shopping Centre na kampuni nyingine nchini akisema anasingiziwa.

 

TRA, kwa upande wake, imesema kauli kwamba makontena yaliyokamatwa yakiwa na matatizo ni ya Home Shopping Centre inayojiendesha kwa nguvu ya Ridhiwani ni upuuzi.

Kamishna wa Forodha, Kabisa Masamaki, ameiambia JAMHURI kuwa ni upuuzi baadhi ya wafanyabiashara kupotosha ukweli, wakati makontena yaliyokaguliwa ni zaidi ya 2,000 na ni ya wafanyabiashara mbalimbali nchini, kisha kudai kwamba ni ya kampuni moja ya Home Shopping Centre.

 

Mkurugenzi wa Huduma za Mlipakodi na Elimu wa TRA, Richard Kayombo, amesema kati ya makontena 500 ya wafanyabiashara mbalimbali yaliyokaguliwa, 188 yamebainika kuwa na udanganyifu unaolenga kukwepa ulipaji kodi kwa bidhaa husika.

 

“Tulianza ukaguzi wa makontena hayo Aprili 12, mwaka huu, na tumebaini kuwa nyaraka za takwimu za bidhaa nyingi zinaonesha idadi ndogo kuliko idadi halisi ya bidhaa husika,” amesema Kayombo.

 

Amesema TRA imefuata utaratibu wa kutoa muda wa siku 14 kwa wafanyabiashara husika waweze kuwasilisha vielelezo sahihi ili watozwe kodi halisi.

 

“Lakini endapo watashindwa kufanya hivyo kwa siku 14 tutawaongeza siku 21 na baada ya muda huo tutatangaza mnada kwa ajili ya kuuza bidhaa hizo,” amefafanua.

 

Kwa mujibu wa Kayombo, baadhi ya wafanyabiashara wamejitokeza kuwezesha ukaguzi wa makontena yao na kulipia kodi husika kabla ya kuruhusiwa kuyachukua.

 

Hata hivyo, amesema makontena mengi hayajakaguliwa kutokana na wamiliki wao kutojitokeza, na kwamba thamani halisi ya kodi inayopaswa kutozwa itafahamika baada ya takwimu halisi kutoka bandari zote kuwasilishwa.

 

“Kwa muda mrefu tumekuwa na kawaida ya kukagua mizigo kwa asilimia 30 ili kujiridhisha, lakini kwa sasa tumeanza kukagua kwa asilimia 100 kwa kila mizigo unaoingia bandarini.

 

“Isipokuwa [hatukagui] malighafi ya kuzalisha bidhaa viwandani, mizigo inayokwenda kwenye miradi iliyofadhiliwa na wahisani, mizigo ya mabalozi na inayokwenda maeneo maalum ya kibiashara,” amesema.

 

Ukaguzi huo umefanyika baada ya maofisa wa TRA kubaini viashiria vya udanganyifu wa takwimu za baadhi ya bidhaa zikiwamo nguo, vipuri za magari, vifaa vya ujenzi, televisheni, majokofu na vyandarua.

 

“Kitu cha msingi ni kwamba tumegundua udanganyifu na tumechukua hatua,” amesema Kayombo bila kutaka kutaja kampuni yoyote kwa jina.

 

Msemaji wa Kampuni ya Home Shopping Centre, Joseph Rugakingira, alisema mgogoro uliopo ni fitina za wafanyabiashara wanaoona kampuni ya Home Shopping Centre inachukua nafasi yao kibiashara.

 

“Ni majungu tu hakuna jambo lolote la ukweli. Kati ya makontena yaliyokaguliwa, ya kwetu wamekagua makontena 463, kati ya hayo ni makontena tisa tu, ndiyo yamekutwa na wrong packing (bidhaa tofauti).

 

“Yupo mfanyabiashara mmoja simtaji, yeye ya kwake wamekagua makontena 250 tu, wakakuta 231 yana matatizo. Mimi ni tisa tu, na hii imetokana na kuchanganya document (vielelezo) kutokana na wingi wa mizigo tunayoingiza nchini, lakini hili ndilo wamelishikia bango ajabu.

 

“Na mimi najua tatizo limelala wapi. Hawa wanafanya fitina. Wapo wafanyabiashara wakubwa ambao wamekuwa wakileta mzigo na kuuza kwa bei za juu ajabu au wanasafirisha mizigo kwa bei kubwa na kuwaumiza wafanyabiashara wadogo hapa nchini.

 

“Sasa hivi mfanyabiashara mwenye shilingi milioni 10 na kuendelea anakwenda China, ananunua mzigo analeta kwetu tunamsafirishia kwa bei rahisi, anakuja hapa nchini anauza na kupata faida.

 

“Kinachotokea ni kwamba wale waliokuwa wanawanyonya wafanyabiashara wadogo hapa Kariakoo wameanza kukimbiwa na wafanyabiashara hao. Wafanyabiashara wadogo wanaona bora waje kwetu tuwasafirishie na kuwatolea mzigo kwa bei nafuu, wapate faida.

 

“Sasa hawa wanaokimbiwa na wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakiwanyonya, wanaokuja kwetu tuwasaidie kukua, inawakera (wafanyabiashara wakubwa) wanaamua kutupiga fitina.

 

“Hili la Ridhiwani tumelisikia, lakini tunasema si kweli. Tumekuwa na biashara miaka mingi tu, Ridhiwani kuwa na urafiki au mawasiliano naye ya hapa na pale, si kwamba amekuwa mbia katika kampuni zetu.

 

“Tunasema mwenye wasiwasi na kampuni zetu, basi na aje hata leo akague document au bidhaa zetu. Tuko huru na wazi. Hatuna wasiwasi. Ebu tusaidiane kukua hapa nchini,” alisema Rugakingira.

 

Rugakingira pia aliiomba TRA kujenga utamaduni wa kusafiri hadi nchi kama China na kwingineko kuona bei halisi za bidhaa, badala ya kuweka kodi kubwa zenye kukatisha tamaa walipakodi, kwani bidhaa zinauzwa kwa bei ndogo China ila zinaongezeka bei kutokana na ukubwa wa kodi hapa nchini. Hii inawafanya wafanyabiashara wasio waaminifu kufikiria kukwepa kodi.

By Jamhuri