Rais wa Marekani Donald Trump ameishinikiza Urusi kukubali mpango wa usitishaji mapigano bila masharti kwa siku 30 na Ukraine. Amesema ukiukaji wowote wa mpango huo utaadhibiwa na vikwazo.
Trump ameanzisha upya wito huo baada ya kuzungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye ameimarisha uhusiano wake na serikali ya Marekani baada ya makabiliano yaliyozuka katika Ikulu ya White House Februari 28.
Zelensky amewashinikiza Warusi kukubali mpango huo akisema lazima wadhihirishe nia yao ya kumaliza vita. Amesema Ukraine iko tayari kuanza kutekeleza maramoja usitishaji kamili wa mapigano kwa siku 30.
Rais wa Urusi Vladmir Putin kwa upande wake aliamuru usitishaji mapigano kwa siku tatu kuanzia jana kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 80 ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Aliandaa maonesho makubwa ya gwaride la kijeshi tukio lililodhuhuriwa na viongozi wa kigeni akiwemo Rais wa China Xi Jinping. Ukraine hatahivyo ilipuuzilia mbali mpango wa upande mmoja ikisema Urusi ilikiuka saa chache baada ya kuanza kutekelezwa.
