RAIS wa Marekani Donald Trump ametangaza kuiondolea vikwazo vyote Syria akisema kwamba ni wakati wa nchi hiyo “kusonga mbele” na hivyo kuipa nafasi ya kuanza kuufufua uchumi wake ulioporomoka kutokana na vita.

Rais Donald Trump alisema kuwa Marekani haina mshirika wa karibu zaidi kuliko Saudi Arabia wakati wa ziara yake ya kwanza nje ya nchi – ziara katika mataifa ya Ghuba inayolenga zaidi kuimarisha uwekezaji.

Akizungumza mjini Riyadh, kiongozi huyo wa Marekani pia ameahidi kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Syria akisema kwamba sasa ni wakati wa nchi hiyo kusonga mbele na kuipa nafasi muhimu ya kuufufua uchumi wake ulioporomoka kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi.

Alieleza kuwa vikwazo dhidi ya Syria vimetimiza malengo yake na hivyo havihitajiki tena.

Tangazo la Trump kuiondolea Syria vikwazo linaashiria mabadiliko makubwa katika sera ya muda mrefu ya Washington kuhusu Syria, ambapo vikwazo viliilenga serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad, na nchi hiyo kwa ujumla kutokana na visa vya ukandamizaji wa upinzani na ukiukwaji wa haki za binadamu katika muda wa karibu miaka 14.