Rais wa Marekano Donald Trump anatarajiwa kuzungumza kwa njia ya simu mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, kuhusu usitishaji mapigani nchini Ukraine. Ni sehemu ya jitihada za muda mrefu kuvifikisha mwisho vita vya Ukraine.

Viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia kwa mara nyingine tena wamesisitiza juu ya umuhimu wa vikwazo dhidi ya Urusi katika mazungumzo ya simu na rais wa Marekani Donald Trump kabla mkutano wake wa kilele na rais wa Urusi Vladimir Putin utakaofanyika kwa njia ya simu.

Hayo yamesemwa na afisi ya waziri mkuu wa Uingereza, Keir Stamer. Trump anatarajiwa kuzungumza na Putin hivi leo Jumatatu kama sehemu ya juhudi za muda mrefu kutaka kuvifikisha mwisho vita vilivyoanzishwa na uvamizi wa Urusi wa mwaka 2022 nchini Ukraine.

Zelensky akutana na viongozi wa Marekani, EU mjini Rome kabla ya simu ya Trump na Putin

Katika taarifa iliyotolewa Jumapili jioni kuhusu mazungumzo ya simu, msemaji wa waziri mkuu wa Uingereza amesema viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia walijadili kuhusu hali inayoendelea nchini Ukraine na gharama kubwa ya vita kwa pande zote mbili za Urusi na Ukraine.

Viongozi hao walijadili umuhimu wa usitishaji mapigano usio na masharti na kwa rais Putin kuchukua mazungumzo ya kutafuta amani kwa uzito.