Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) na Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation zimekutana na kufanya mazungumzo ya namna ya bora kushirikiana katika kuwajengea uwezo wanawake kujiendeleza kiuchumi kwa kuwawezesha kuzalisha bidhaa za Mkonge.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Mkonge (Mkonge House) jijini Tanga baina ya Mkurugenzi wa TSB, Saddy Kambona na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwanamke Initiative, Sabra Mohamed wakati yeye na ujumbe wake walipotembelea TSB kujifunza na kujionea fursa mbalimbali za Mkonge.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Sabra ametembelea Kituo Atamizi cha Mkonge (Mkonge BBT), kinachoendesha mafunzo ya kuzalisha bidhaa za Mkonge kwa kutumia mikono (handcraft) kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu na kinasimamiwa na TSB na shamba la Mkonge lililopo Hale na kujionea hatua za uchakataji Mkonge.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi Kambona amesema mategemeo makubwa ni kuona wanatengeneza ajira zaidi, kujenga uwezo zaidi kwa wanawake kujiendeleza kiuchumi kwa kutumia bidhaa za Mkonge.
“TSB tutakuwa tunatoa singa za Mkonge kupeleka Zanzibar na maeneo mengine kwenye taasisi na vituo kama atamizi ili wanawake waendelee kujifunza zaidi kutengeneza bidhaa kwa kuyatumia masoko ya watalii na kuuza kwenye maeneo mbalimbali kwa hiyo ni mchanganyiko wa Uchumi wa Buluu kumsaidia mwananchi wa kawaida hususani vijana na wenye ulemavu kupambana na hali ya ukosefu wa ajira na kujipatia kipato,” amesema Mkurugenzi Kambona.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mwanamke Initiative, Sabra Mohamed amesema lengo la kutembelea TSB ni kuangalia fursa za kushirikiana katika kufanya kazi juu ya matumizi ya Mkonge hususani kupatiwa wakufunzi watakaotoa mafunzo ya kuzalisha bidhaa za Mkonge katika Kituo cha Bungi kilichopo Zanzibar.
“Sisi Mwanamke Initiative, tuna kituo chetu cha Bungi Zanzibar ambacho tunatarajia kukizindua mapema mwakani kitakuwa kwa ajili ya kuwafundisha wanawake na vijana kuwawezesha ikiwamo kazi za mikono na mojawapo kuzalisha bidhaa kwa kutumia Mkonge. Kwa hiyo tumekuja kuangalia namna ya kushirikiana kuwawezesha wanawake.
“Tumeona hii fursa ni nzuri kwetu katika kituo chetu cha Bungi kufundisha vijana na wanawake kuzalisha bidhaa kwa kutumia Mkonge. Nimejifunza mengi kuhusu Mkonge ambayo nilikuwa siyajui, zamani nilijua Mkonge unatumika katika kutengeneza kamba ila sasa hivi nimeona kumbe Mkonge una matumizi mbalimbali kama vile bidhaa za kutumia mikono lakini pia kuna gesi ambayo inaweza kuzalishwa kupitia makapi ya mkonge ambayo pia yanatengeneza mkaa na sisi pia hiyo ni tumeona fursa katika kutumia nishati safi ya kupikia,” amesema.
Naye Msimamizi wa Kituo Atamizi cha Mkonge, Abdulatif Famau amesema; “Ushirikiano huu unaweza kutoa fursa kwa wanawake kubadilishana ujuzi kutoka Zanzibar na Bara katika kuzalisha bidhaa za Mkonge hatua itakayotusaidia kupeleka mbali bidhaa zetu. Katika kituo chetu bidhaa kuu ni Mkonge lakini tunatumia malighafi nyingine katika kutia nakshi na tunafundisha zaidi wanawake, wenye ulemavu na vijana.”











