Mwezi uliopita Umoja wa Mataifa umezindua mpango mpya wa maendeleo na wa kupambana na umaskini duniani kufuatia kufikia tamati kwa Mpango wa Maendeleo ya Milenia.

Mpango huu mpya unajulikana kama Sustainable Development Goals, na umepitishwa na viongozi wa nchi wanachama za Umoja wa Mataifa waliokusanyika New York kwenye kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Taarifa juu ya Mpango wa Maendeleo wa Milenia inasema kuwa umaskini duniani umepunguzwa kwa zaidi ya nusu kuanzia miaka ya 1990. Kuna baadhi ya asasi za kiraia zinapinga taarifa zinazosema kuwa umaskini umpeungua kwa kiasi hicho.

Lakini ni kwa msingi huu kuwa umaskini umepungua kwa kiasi hicho ndiyo nchi wanachama za Umoja wa Mataifa zimeanza hatua hii ya sasa ya kupambana na umaskini duniani, ikikusudiwa kuwa umaskini uwe umetoweka kwa vigezo vyote ifikapo mwaka 2030.

Hizi asasi zinasema kuwa kama ni kweli kuwa umaskini umepungua kwa kiasi kinachoelezwa kwenye taarifa kuhusu malengo ya milenia basi haina haja ya watu kulalamika, lakini iwapo taarifa hizo siyo sahihi basi kuna kila haja ya watu kutounga mkono harakati hizi za sasa za kupiga vita umaskini.

Kwa kifupi, tunauziwa matumaini ya kufutwa kwa umaskini bila kuwepo uhakika kuwa muelekeo unaotumika kufanya hivyo kweli utafuta umaskini.

Iwapo wote tunaamini kuwa njia sahihi zinafuatwa kuelekea kwenye hiyo hali ya kuwepo neema kwa wote basi harakati zozote za kisiasa kupinga mpango huu mpya hazitakuwa za lazima.

Lakini iwapo upo ukweli kuwa njia tunayopitishwa na viongozi wa dunia siyo sahihi basi tunayo kila haki na wajibu wa kudai njia mbadala ya mpango huu na mfumo mzima unaokusudiwa kuleta matokeo hayo chanya ifikapo mwaka 2030.

Suala hili ni la muhimu kwa wengi wetu ukizingatia kuwa kuna watu wapatao bilioni 1.6 ambao wanakadiriwa kuwa maskini duniani. Aidha, zaidi ya nusu ya watu maskini duniani wanaishi kwenye nchi za Asia ya kusini na zaidi ya asilimia 29 wanaishi kwenye nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Vipo vigezo mbalimbali vya umaskini, na baadhi ya vigezo vinavyotumika vinaonyesha kuwa watu walio maskini duniani wanafikia bilioni 4.1. 

Kwa kigezo chochote kinachotumika matokeo ni kuwa watu wengi duniani ni maskini kwa hiyo hatua zozote zinazofanyika na Umoja wa Mataifa kupiga vita umaskini ni lazima zitaathiri maisha ya wengi, au kwa matokeo hasi au chanya. Na ndiyo hoja ya msingi ya kumulikia jitihada hizi mpya za Umoja wa Mataifa. 

Katika kupiga vita umaskini kuna masuala kadhaa ya msingi yanapaswa kuzingatiwa. Kwanza ni kuuliza nini chanzo cha umaskini. Kuna dhana kuwa umaskini ni lazima uwepo. Kwamba ni hali ya kawaida katika jamii zote.

Dhana hii inajengwa juu ya msingi kuwa jamii imejaa fursa za kila aina ambazo ziko wazi kwa kila mtu kwa hiyo ni suala la kila mtu kuhangaika tu ili aweze kujikwamua na umaskini.

Wanaoziona fursa na kuzichangamkia wanaondokana na umaskini wakati wale wasiozitambua na kuzichagamkia fursa hizo wanabaki maskini. Na dhana hii inasemekana ipo baina ya mtu mmoja na mwingine, na baina ya nchi moja na nyingine.

Ukweli haufanani na dhana hii. Uhusiano baina ya watu na baina ya nchi hutawaliwa na ukweli kwamba fursa hazitiririki kwa usawa ule ule kwa watu wa jamii moja au kwa nchi zilizo kwenye jumuiya ya kimataifa.

Kwa upande wa mataifa, nguvu za kijeshi, za kiuchumi, na za kisayansi na teknolojia baina ya nchi moja na nyingine zinaweza kuwa ndiyo msingi wa kuinua nchi moja au nchi kadhaa zikawa zinapata fursa kubwa zaidi ya kufikia malengo ya maendeleo ya kuziacha nchi nyingi zikitapatapa kuambulia makombo. Tumeshuhudia kwa mfano vita kutumika kama nyenzo ya nchi moja kupata fursa za kufaidika na rasilimali za nchi iliyoshindwa kwenye vita.

Na wale walio na pesa siku zote ndiyo wanaunda taratibu na sheria ambazo zinahakikisha kuwa wanaendelea kuwa na pesa. Kutambua hitilafu hizi katika mfumo Ingekuwa ni mwanzo mzuri wa kuanza na hii hatua mpya ya kupiga vita umaskini.

Suala lingine la kuzingatia ni kuwa mpango huu mpya unaweka mkazo kwenye kukua kwa uchumi kama kigezo cha msingi cha kupiga vita umaskini. Lakini, kama ambavyo uzoefu unadhihirisha, kigezo cha ukuaji wa uchumi kama kipimo cha kupunguza umaskini kina hitilafu kubwa.

Mfano, tangu mwaka 1990 uchumi wa dunia umekuwa kwa asilimia 271, lakini idadi ya watu ambao wanaishi kwa kipato cha chini ya dola 5 kwa siku wameongezeka kwa asilimia 10 kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, na idadi ya watu wanaoishi na njaa imeongezeka kwa asilimia 9 kwa mujibu takwimu za Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa.

Takwimu za ukuaji wa uchumi huainisha uzalishaji kwa ujumla, lakini hazinyambulishi ukweli kuwa kukua huko kwa uchumi kunanufaisha asilimia ndogo sana ya wakazi wa dunia. Kama tunalinganisha kaya na nchi, kukua kwa kipato cha baba ambaye pekee ndiyo aliyeajiriwa hakuongezi kipato cha mtu mmoja mmoja ndani ya familia yake. Vivyo hivyo kwa nchi; iwapo kuna ongezeko la kipato kwa nchi siyo pia kusema kuwa kila mtu ananufaika na ongezeko hilo.

Kwa hiyo ipo kasoro kubwa ya kufanya ukuaji wa uchumi kuwa msingi wa kupiga vita umaskini bila kuangalia masuala mengine kama tofauti inayoongezeka ya usawa baina ya nchi na nchi, na hata baina ya watu ndani ya nchi moja.

Suala lingine la kuzingatia ni dhana ya kuwa nchi zilizoendelea zinatoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Tafiti zinaonyesha kuwa kwa kila dola moja inayotolewa kama msaada kwa nchi zinazoendelea, zipo dola kama 18 zinazorudi toka nchi zinazosaidiwa kwenda kwenye nchi zinazoendelea.

Na hii inafanyika kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na riba za mikopo zinazoendelea kuumiza nchi zinazoendelea, mikataba kandamizi ya biashara, ukwepaji wa kodi, pamoja na ufisadi unaoshirikisha pande zote husika. Mpango huu mpya wa maendeleo hauzungumzii tatizo hili kwa undani, au kuweka njia madhubuti za kuliepuka.

Maji yameshamwagika, na hayawezi kuzoleka. Tusubiri taarifa ya mpango huu mpya, utakapokamilika mwaka 2030, utapamba kwa kiasi gani matokeo hasi ambayo yatajitokeza.

By Jamhuri