Kumeibuliwa tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.

Miradi mitano ya ujenzi imekwama. Miradi iliyokwama ni ujenzi wa vyumba vya maabara wa mwaka 2014; kliniki ya mifugo na bwalo la chakula, iliyoanza mwaka 2016.

Mingine ni ujenzi wa nyumba tatu za walimu katika shule za msingi za Itegamatu, Ilula na Buchang’wa (mwaka 2014/2015) na ujenzi wa kliniki ya macho (mwaka 2016).

Gazeti la JAMHURI limebaini kuwa mwaka 2014 Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ilipokea Sh milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo za walimu. Licha ya zabuni na mkanadarasi kupatikana, fedha za ujenzi huo hazijulikani ziliko.

Hakuna kumbukumbu za kuonyesha kama Baraza la Madiwani lilifanya mabadiliko ya matumizi ya fedha hizo.

Mkandarasi, Ntangwa Enterprises, alipewa kazi ya kujenga nyumba katika Shule ya Msingi Ilula kwa Sh 45,910,785. Mkandarasi Busiya General Contractors Ltd ilikuwa ajenge nyumba katika Shule ya Msingi Itegamatu kwa gharama ya Sh 50,048,870; na mkandarasi Shileman Construction Co. Ltd alitakiwa ajenge nyumba katika Shule ya Msingi Buchang’wa kwa Sh 43,997,880.
Tuhuma za upotevu wa fedha hizo zimewasilishwa na Diwani wa Kata ya Lyoma, Kasalali Mageni (CCM) katika kikao cha madiwani cha Machi 29, mwaka huu mjini Ngudu.
Amesema Oktoba 7, 2016 Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba inayoongozwa na Mkurugenzi Pendo Malebeja, ilipokea Sh 274,639,200. Sh milioni 137 kati ya fedha hizo zilitakiwa zijenge bwalo la chakula.

“Halmashauri iliingia mkataba wa Sh 162,245,044 na mkandarasi Grinda Builders & Supplies Co. Ltd, kinyume cha makubaliano yaliyoridhiwa na vikao halali vya halmashauri hiyo vilivyotaka bwalo lijengwe kwa Sh 137,495,800. Halmashauri iliingia mkataba bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya Halmashauri,” amesema Kasalali.

Bwalo lilitakiwa liwe limekamilika Novemba 12, 2016 lakini hadi Machi, mwaka huu ujenzi huo ulikuwa haujakamilika. Mkandarasi aliomba aongezewe muda hadi Aprili 30, 2017 kupitia barua yake ya Januari 31, mwaka huo.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa kliniki ya mifugo, Oktoba 2, 2014 Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ilipokea Sh milioni 250; na Sh milioni 100 kati ya hizo zilitakiwa zitumike kwenye ujenzi huo.

Halmashauri iliingia mkataba wa ujenzi na mkandarasi Consel Construction Ltd wa Mwanza wenye thamani ya Sh 94,519,085 uliosainiwa Mei 20, 2016. Ulipangwa ukamilike Novemba 19, 2016.
Diwani Mageni amesema mkandarasi alilipwa Sh 13,313,323.75 Septemba 30, 2015 na Desemba 19, 2016 akalipwa Sh 25,614,850. “Hivyo, kufanya mkandarasi kuwa amepokea Sh 38,928,173.75 ambazo ni asilimia 41. Mpaka sasa kazi haijakamilika, na Sh milioni 64 hazijulikani zilitumika vipi na mkandarasi amesimama kazi na kuacha gofu,” amesema.

Mwaka 2017 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, aliunda tume kuchunguza tuhuma hizo na hadi sasa hatima yake haijulikani.

“Tanzania hii imefikishwa hapa kwa sababu ya urasimu, woga, unafiki na tabia za watu za kupenda kulindana lindana na kubembelezana bembelezana. Magofu yale yapo pale tunayaona. Pale nimekwenda kliniki inapata kutu, waheshimiwa madiwani bado tunazungumza utaratibu.
Utaratibu huu ndio unawapa ujasiri hawa watu kuendelea kufanya hivi vitu.
“Kwa kuweka kumbukumbu sawa, na kwa heshima kabisa ya wananchi wa Kwimba na watu wote wanaopenda haki na maendeleo kwenye nchi hii, na mkumbuke tu jana (Machi 28, 2019) tulikuwa tunahangaika na Mheshimiwa Rais, watu wa ATCL, watu wakubwa aliowateua wanataka kwenda kupaka ndege rangi kwa Sh milioni 200…familia kubwa inayoheshimika Tanzania kuliko zote ni familia ya wanyonge,” amesema.
Diwani wa Kata ya Wala, Elias Kapunda, amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza anapaswa atoe hadharani ripoti ya tume aliyounda kuchunguza ubadhirifu huo.

Diwani wa Kata ya Bupamwa, Sephania Cheyo, amesema: “Tuna miradi mingi ambayo imetuletea kero. Mpaka leo kuna stendi pale tumezika Sh milioni 500 (Stendi ya Ngudu) ambayo haina faida kwa Halmashauri yetu ya Kwimba.”

Madiwani hao wamemuomba Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Simon, kumwandikia barua mkuu wa mkoa ili wapate ripoti ya uchunguzi.

Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza (jina tumelihifadhi), amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ina majalada mengi Takukuru.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Stamili Ndaro, amesema suala hilo haliwezi kujadiliwa na madiwani, badala yake linapaswa lipelekwe kwenye kamati.

 “Kuna mamlaka ambazo zinaendelea na uchunguzi wake, ni vema tuziache zifanye kazi yake na baada ya taarifa kutolewa hatua zaidi zitachukuliwa,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Shija Malando, ameshauri ripoti ya tume ya mkuu wa mkoa iwasilishwe kwa madiwani.

“Kwa sababu waliohujumu hii miradi wapo hapa hapa halmashauri na wengine wameondoka wanaweza kurudishwa kuja kujibu,” amesema Malando.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Peter Ngassa, amesema: “Hatuwezi kulijadili suala hili. Takukuru wanalo, Kamati ya Ulinzi na Usalama inalo. Sasa tujadili tumpelekee nani? Kikubwa, majibu ya tume tuletewe.”

Please follow and like us:
Pin Share