Mwaka 2014 nilisafiri kwa ndege nikakaa pembeni mwa abiria raia wa Kenya, ambaye alibaini nilikuwa nikisoma kitabu kimojawapo cha hotuba za Mwalimu Nyerere.

Alisema: “Nasikia Nyerere aliiharibu sana nchi kutokana na itikadi yake ya Ujamaa?”

Katika umri wangu nimeshasikia kwa muda mrefu maoni kama haya, maoni ambayo yamenijengea usugu wa kiasi fulani wa kutafakari hoja bila kuzingatia ni nani anayesemwa au nani anasema.

Nilimwambia kuwa kosa moja kubwa linalofanywa na baadhi ya wanaokosoa sera za Ujamaa, hasa wale ambao wanapendelea itikadi za mrengo wa kulia, ni kutochambua nini hasa kilikuwa ndani ya kapu lililojumuisha sera ya Ujamaa na Kujitegemea.

Nikamkumbusha kuwa Rais Mwai Kibaki alipitisha uamuzi wa kutoa elimu bure ya msingi kwa wanafunzi nchini Kenya mwaka 2003, na nikamtwanga maswali mawili ambayo majibu yake mawili yalifanana: “Hapana.” Unadhani Rais Kibaki alichukua uamuzi mbaya? Kenya ni nchi ya Kijamaa?

Nikamwambia: “Na huyo Mjamaa Nyerere ambaye unasema aliiharibu nchi naye alifanya uamuzi wa aina hiyo hiyo, isipokuwa yeye alipitisha uamuzi wa kutoa elimu ya bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.”

Nilimshauri badala ya kusikiliza maneno ya watu yanayohitimishwa kwa sentensi moja tu, ni bora ajifanyie uchambuzi wake mwenyewe na kujifunza ni uamuzi wa aina gani ulifanywa chini ya mwavuli wa Ujamaa.

Uamuzi wa Rais Kibaki uliwezesha watoto zaidi ya milioni moja kujiandikisha shuleni na kusaidia wazazi ambao hawakuwa na uwezo wa kulipia karo.

Nimeonana na Watanzania wengi wanaokiri kuwa iwapo uamuzi wa elimu ya bure usingepitishwa, wengi wasingepata elimu waliyonayo. Baadhi ya hawa ni wanazuoni waliobobea katika fani zao.

Bila kujali itikadi, siamini kama kuna ubishi mkubwa juu ya manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii ya elimu kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa.

Nadhani tatizo linalojitokeza tunapotathmini sera ya Ujamaa na Kujitegemea ni kushindwa, wakati mwingine, kutenganisha itikadi ya Ujamaa kama mfumo wa kisiasa na kiuchumi na uamuzi ambao ulifanyika chini ya utekelezaji wa sera hiyo, lakini uamuzi ambao, kimsingi, ulizingatia mantiki ya kawaida tu.

Utekelezaji wa Ujamaa ulisimama juu ya msingi wa umma kuwa na uwezo kamili wa kiuchumi na kijamii wa kusimamia mifumo ya uzalishaji na kubuni miongozo ya kisiasa kusimamia mfumo huo. Huu ni msingi wa kiitikadi. Kifalsafa, Ujamaa ulijengwa juu ya imani kuwa binadamu wote ni sawa.

Pamoja na kuwa upo uamuzi uliozingatia itikadi na falsafa ya sera yenyewe, tusipuuze uwezekano kuwa katika mazingira ya wakati huo baadhi ya uamuzi ulikuwa uamuzi wa busara wa kawaida kabisa wa binadamu yeyote ambaye angekabiliwa na uamuzi huo.

Lakini hatuna budi kukubali kuwa itikadi ni kama dini; wanaotofautiana kiitikadi ni nadra kukubaliana. Kwa kawaida, dini ni mkusanyiko wa miongozo ambayo inakubalika na waumini na wafuasi wake kuwa ni mwongozo kutoka kwa Muumba wao. Ni mwongozo ambao hauguswi, haukosolewi, wala hauhaririwi.

Inapotokea kundi la waumini kushindwa kufuata mwongozo huo wanalazimika kutoka kwenye dini hiyo na baadhi yao huanzisha dini ambayo inaakisi mawazo yao mapya.

Waumini hawa siwafananishi na wanasiasa wanaohama huku na kwenda kule na kurudi huku ndani ya kipindi kimoja cha uchaguzi. Nazungumzia mwanasiasa ambaye itikadi kwake ni kigezo cha kila uamuzi ambao anaufanya ndani ya maisha yake ya kisiasa na maisha yake binafsi. Hafanyi uamuzi mpaka aridhike kuwa ni uamuzi ambao unarandana na msimamo wake wa kiitikadi.

Na hata anapofuata yale yale ambayo anaamini ni ya itikadi ambayo hakubaliani nayo, atayapachika jina tofauti ilimradi asihusishwe na suala ambalo halikubali. Atakuwa radhi kusema anaunga mkono sera endelevu, lakini atapinga kwa nguvu zote sera ya Ujamaa na Kujitegemea ingawa ndani yake kuna misingi thabiti ya sera endelevu.

Nimesema kuwa elimu ina manufaa makubwa kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa, lakini inabidi pia kuhoji wakati mwingine kama elimu nyingi inaweza kuwa chanzo cha ujinga pia. Baadhi ya wanasiasa, baadhi ya wasomi, na baadhi ya wanasiasa wasomi wameshikilia uwezo mkubwa wa kupinga uamuzi wa kisera na kisheria unaoweza kuleta manufaa makubwa kwa jamii kwa sababu tu ya tofauti za kiitikadi. Hili si tatizo la mpiga kura wa kawaida ambaye anajaribu kuboresha maisha yake ya kila siku.

Hoja yangu si juu ya uzuri au ubaya wa Ujamaa kama itikadi. Hoja yangu ni rai kwa wale ambao badala ya kuchambua uzuri au ubaya wa uamuzi uliofanyika enzi za Mwalimu, wameweka jitihada kubwa ya kuutathmini kwa misingi ya itikadi.

Si kila uamuzi ambao ulifanyika kwenye awamu ya kwanza ulikuwa wa manufaa kama ambavyo hatuwezi kukubali uongo kuwa sera za mrengo wa kulia zina manufaa makubwa na hazina athari kubwa za kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Kinachoweza kusemwa kwa uhakika ni kuwa, upo uamuzi mwingi wa manufaa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Kwanza, na huo haupaswi kufanyiwa tathmini kwa misingi ya itikadi.

Maoni: [email protected]

Please follow and like us:
Pin Share