Tunaona juhudi za serikali za kuhamasisha mazingira mazuri ya biashara nchini. Wiki iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameliambia Bunge kwamba serikali imo mbioni kufuta sheria zote zinazokwamisha biashara.

Kauli ya waziri mkuu imetanguliwa na kauli nyingi kutoka kwa mawaziri wa biashara, uwekezaji na watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hivi karibuni Kamishna Mkuu wa TRA ameonekana akipita huku na kule nchini katika kile kilichoelezwa ni kutoa elimu kwa walipakodi, pia kuwasihi wafanyabiashara waendelee na biashara. Lakini kabla ya ziara ya kamishna huyo, TRA wakawa wametoa tamko la kuzuia watendaji wake kufunga biashara pindi wanapokuwa wakimdai mfanyabiashara.

Walau viongozi wetu sasa wameamini kuwa mazingira ya biashara nchini mwetu yamekwamisha wengi, na tayari baadhi yao wamekwenda katika mataifa jirani kuendelea na shughuli zao.

Itakumbukwa kuwa wafanyabiashara wa Tunduma – mpakani mwa nchi yetu na Zambia – ndio waliokuwa wa mwanzo mwanzo kulalamikia mazingira ya biashara. Walipaza sauti, lakini wakubwa wetu wakajifariji kwa kusema waliokuwa wakiongoza kelele hizo ni wapinzani, hasa Chadema kwa sababu eneo hilo “linatawaliwa” na chama hicho.

Kelele za kuomba mazingira yaboreshwe zilipopuuzwa wakahamia upande wa pili wa Nakonde (Zambia) na kuweka maduka. Mapato yakapungua. Viongozi wa serikali walipofika kuwabembeleza warejee upande wa Tanzania, wakagoma. Hali imeendelea kuwa mbaya kwa mapato ya mamlaka zetu.

Kinachosikitisha ni kuona kuwa kelele nyingi zinazopigwa na wananchi, iwe kwenye biashara au katika mambo mengine, viongozi wetu ni wagumu mno kuzipokea na kuzifanyia kazi mapema. Tumekuwa na baadhi ya viongozi wanaodhani kwa kuwapo kwao ofisini, basi walio nje wote hamnazo. Wanadhani kwa kuwa kwenye uongozi, basi wana leseni ya kupuuza chochote kinachosemwa na watawaliwa.

Laiti kama viongozi wetu wangesikia kilio cha wafanyabiashara mapema na kuchukua hatua, haya yote yanayotusibu leo yasingetufika.

Bahati mbaya tunao viongozi na watumishi wasio wakweli. Kunapotolewa taarifa kwamba watu wanafunga biashara na kukimbilia nje ya nchi, majibu yao yamekuwa kwamba “hao ni wale waliokuwa wakwepa kodi”.

Wakiambiwa wanaokimbia wanakimbia kwa sababu ya mazingira yasiyo rafiki katika biashara, wanapinga ukweli huo. Ndiyo maana wapo wanaohoji, ukanushaji huu unatokana na umbumbumbu wa watumishi na viongozi au ni mkakati wa kumkwamisha Rais Magufuli? Maana haiwezekani katika mambo yanayoonekana wazi wazi bado kuwepo watu wenye nguvu za kuukana ukweli.

Katika nchi zinazotuzunguka hakuna nchi ambayo ni pepo ya wakwepa kodi. Kote huko wafanyabiashara wanalipa kodi kama kawaida. Tofauti yetu na wao ni kwamba wao wana mazingira rafiki ya biashara, wana kodi chache zinazoeleweka na hakuna urasimu wala vitisho.

Juzi, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, ameorodhesha idadi ya kodi kwa wafanyabiashara. Kuna eneo kodi zinafikia 26. Kuna eneo lenye aina 18 ya kodi. Yupo mzalendo aliyeomba vibali vya uwekezaji mwaka 2016 lakini akavipata mwaka huu! Haya huwezi kuyakuta Kenya wala Rwanda.

Mlolongo wa ukaguzi nchini mwetu umetia fola. Kila mahali kuna askari wa usalama barabarani. Usafirishaji katika barabara za Tanzania ni shida. Hakuna ukaguzi wala nini, isipokuwa ni kusumbuana tu ili madereva watoe rushwa. Haya yapo. Yanaonekana. Wakubwa wanasafiri barabara zote nchini wanayaona, lakini wanajifanya hamnazo. Wameyabariki kana kwamba ni mambo yenye manufaa kwa nchi, ilhali ukweli ni kuwa hizi ni kero zinazowakatisha tamaa wafanyabiashara wa ndani na wale wanaotumia miundombinu yetu ya bandari na barabara.

Hatuna budi kukabiliana na hali hii. Njia pekee ni kuhakikisha sote tunabadilika. Kila mmoja atekeleze wajibu wake. Wajibu wa wananchi ni kueleza changamoto na kero zinazowakabili. Wajibu wa viongozi na watendaji wote ni kupokea malalamiko ya wananchi (wateja) na kuyachunguza mara moja kwa lengo la kuyapatia majawabu ya kudumu.

Wafanyabiashara wanapolalamika kubambikiwa kodi, TRA wafungue milango, wapokee malalamiko wayafanyie kazi. Watu wanaposema biashara zinafungwa kwa sababu ya mfumo na mazingira ya kibiashara, wasomi waliojaa maeneo husika watoke nje. Wachunguze malalamiko hayo na majibu yatolewe.

Tuendeshe mambo yetu kwa mifumo ya kijeshi. Hakuna jeshi makini linaloweza kupuuza taarifa yoyote ya usalama hata kama inatolewa na mwendawazimu. Jeshini, kila taarifa hupokewa na kuchunguzwa ili kubaini uhalali wake.

Mifumo mingine inapaswa ifanye kazi namna hiyo. Kamwe taarifa yoyote, hasa ya malalamiko haipaswi kupuuzwa kwani kama ni ya kweli na endapo itapuuzwa athari zake ni kubwa. Wanaomsaidia rais wahakikishe wanamsaidia kwa kumpa taarifa halisi na za kweli zilizoko huku mitaani. Waliofunga biashara si kweli kwamba wote walikuwa wakwepa kodi. Wapo wanaodaiwa kodi inayozidi mitaji yao. Kama kweli tumenuia kuijenga nchi yetu, basi wananchi wasikilizwe.

Please follow and like us:
Pin Share