Mpita Njia (MN) yapo mambo anamkosoa Rais Magufuli, lakini yapo mengine – tena mengi – anayokubaliana naye.

Waswahili walisema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Kazi inayofanywa sasa katika maeneo mbalimbali nchini inatia fora.

Kumjaza sifa zilizopitiliza kunaweza kumfanya abweteke, lakini itoshe kusema yapo mazuri yanayopaswa kusemwa na kwa kweli Watanzania wana kila sababu ya kujidai.

Ujenzi wa barabara umeshika kasi. Ile barabara ya Kimara – Kibaha inajengwa kwa kasi ya kutia moyo. Kazi inaonekana.

Lakini jambo moja tu linakera kwa kweli. Nalo si jingine, bali ni hili ambalo Mpita Njia amekuwa akiliona eneo la Mbezi Mwisho. Wachuuzi ambao wamepewa jina la ‘wafanyabiashara’ wanakwamisha hii kazi.

Pale wajenzi hawa wanapokuwa wakitaka kupitisha greda, wamepambana na meza zenye bidhaa za wachuuzi. Uwepo wao katika eneo hili umepunguza kwa kiwango fulani kasi ya ujenzi wa barabara hii muhimu.

Mpita Njia anakumbuka wakati fulani Rais Magufuli aliwaruhusu waendelee kuwapo hapo, lakini wawe tayari kuwapisha makandarasi wakati wakikaribia maeneo walipo.

Agizo hilo la Rais Magufuli, Mpita Njia hadhani kama lilikuwa la kuwafanya wachuuzi hawa wawe na viburi au wasumbufu kwa wajenzi.

Kinachoonekana sasa ni kama wameamua kutafsiri vibaya kauli na huruma ya Rais Magufuli na kuamua kukomalia eneo la ujenzi.

Kuwapo eneo hilo kuna hatari nyingi, maana kuna malori na mitambo inayoweza kupoteza mwelekeo ikawapamia na kusababisha majeruhi na hata vifo.

Hatari anayoiona Mpita Njia hapa ni kuwa endapo kutatokea ajali kwa mchuuzi kuumizwa au kufa, kutatokea vurugu kubwa, maana wataona kama vile wanaonewa.

Mpita Njia anadhani kuwa pamoja na nia njema ya Rais Magufuli ya kuwapenda wamachinga hawa, basi nao wawe na staha kwa kutambua kuwa barabara hii inapaswa kujengwa na kukamilika ndani ya muda uliopangwa. Litakuwa jambo la ajabu, na kwa kweli la aibu, kusikia kuwa ujenzi umecheleweshwa na watu waliopanga sidiria na bamia katika eneo la kazi.

Lakini jambo jingine kuhusu wachuuzi hawa ni kuwa barabara ikishakamilika watapelekwa wapi? Mbona Mpita Njia na wenzake hawaoni dalili za kujengwa soko ili kuwaweka pamoja? Au ndiyo wataachwa wapange bidhaa barabarani kama ilivyo katika mitaa ya majiji yote?

Mwisho, Mpita Njia anawaomba wachuuzi wa Mbezi Mwisho wasiwakwaze wajenzi hao wa barabara. Wawape fursa ya kutekeleza wajibu wao ambao kwa kweli ni ukombozi mkubwa kwa kina MN ambao nusu ya maisha yao wanayamalizia kwenye foleni.

Please follow and like us:
Pin Share