*Boko naye asogelewa na ‘Kiatu cha Dhahabu’

Wakati Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa imeingia katika raundi ya 22, mwelekeo wa ubingwa hivi sasa umebaki mikononi mwa timu tatu za Simba, Azam na Yanga, zote za Dar es Salaam.

Hadi sasa Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 50, ikifuatiwa na Azam iliyokusanya pointi 47 huku Yanga ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 46, lakini ina mechi moja zaidi mkononi baada ya kuingia uwanjani mara 21 tu.

Jumamosi iliyopita, Simba ilizidi kujiimarisha kileleni baada ya kuitungua African Lyon mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini kabla ya kupaa kwa ndege kuelekea Algeria, jana, Jumatatu.

Huko, timu hiyo itarudiana na Entente Setif katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Ijumaa wiki hii. Inatakiwa kushinda, kutoka sare yoyote au kufungwa bao 1 tu ili isonge mbele baada ya kushinda kwa mabao 2- 0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa hapa nyumbani.

Wakati Simba, Azam na Yanga zikichuana kutafuta ubingwa, timu sita katika upande wa pili zinakabiliwa na hatari kubwa ya kuangukia Daraja la Kwanza msimu ujao.

Timu hizo na pointi zake kwenye mabano ni Kagera Sugar (24), African Lyon (21), Villa Squad (19), Moro United (18), Polisi Dodoma (17) huku Toto African ikiwa na alama 16 tu.

Ubingwa kwa timu hizo tatu utaamuliwa zaidi na matokeo ya mechi zilizobaki kwa kila timu kushinda, kutoka sare au kufungwa sambamba na kiwango cha mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika mbio hizo, Simba imebakiza mechi nne sawa na Azam itakapoteremka dimbani kumenyana na Ruvu Shooting (Aprili 15), JKT Ruvu (Aprili 18), Moro United (Aprili 25) na kuhitimishia msimu kwa mahasimu wake wakubwa katika soka la nchi hii, Yanga (Mei 5), mechi ambazo zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba inaweza kuwa na uhakika au matumaini makubwa ya kushinda mechi zake dhidi ya Ruvu Shooting na Moro United, lakini itakuwa na kibarua kigumu kwa JKT Ruvu huku ikiwa haina uhakika wowote wa kushinda ama kutoka sare itakapokutana na Yanga.

Aidha, Azam itasafiri mara moja kwenda kucheza kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma dhidi ya Polisi ya huko hapo Aprili 14, timu inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa ligi hiyo hadi kufikia sasa.

Katika mechi hizo tatu za mwisho, Azam inaweza kuvuna pointi sita kutoka timu za Polisi Dodoma na Toto African, lakini haiwezi kuwa na uhakika wa ushindi wala sare kutoka timu za Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.

Nayo Yanga itashuka dimbani kupambana na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza (Aprili 15), kisha itaikabili Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Aprili 18.

Kutoka huko itakwenda kucheza na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo (Aprili 22), kisha itasafiri hadi Arusha kumenyana na JKT Oljoro katika dimba la Sheikh Amri Abeid (Aprili 25) na kufunga kazi kwa mechi dhidi ya Simba, Mei 5 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hizo pia, Yanga inaweza kuwa na uhakika wa kushinda mechi dhidi ya Toto African, Polisi Dodoma na JKT Oljoro, lakini linaweza kutokea lolote katika mpambano wake dhidi ya Simba.

Azam inajivunia kuwa na mshambuliaji mkali kuliko wote katika ligi hiyo, John Boko ‘Adebayor’ aliyejiuzulu kuichezea timu ya taifa (Taifa Stars) hivi karibuni, ili aweze kuisaidia zaidi timu yake katika mbio hizo za kuwania ubingwa.

Hadi sasa, Boko ndiye anayeongoza katika utikisaji wa nyavu akiwa amepachika mabao 16. Anafuatiwa kwa pamoja na washambuliaji Kenneth Asamoah wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba, wote wakiwa wamefunga mabao 10 kila moja.

Katika hatua hizi za mwisho, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amekiongezea nguvu ya mazoezi kikosi chake kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo. Sasa ameweka mkazo mkubwa wa kuwajengea stamina wachezaji wake ili wawe na nguvu pamoja na uwezo zaidi wa kuhimili vishindo na kutochoka haraka wanapokuwa uwanjani.

Ukimwondoa Boko, Azam haina mshambuliaji mwingine wa uhakika inayeweza kumtegemea katika ufungaji ingawa Gaudence Mwaikimba anaonyesha uhai baada ya “kucheka na nyavu” mara sita hadi sasa, jambo linaloweza kuigharimu kwa vile likitokea lolote inakuwa haina chochote.

Mfungaji aliyetwaa “Kiatu cha Dhahabu” msimu uliopita, Mrisho Ngassa safari hii ameshindwa kuonyesha makali hayo. Wakati ligi hiyo ikikaribia kufika mwisho, winga huyo juzi, Jumapili, ndiyo kwanza alifikisha mabao sita kama Mwaikimba.

Simba nayo inamtegemea zaidi Mganda Emmanuel Okwi na Mnyarwanda Patrick Mafisango aliyetikisa nyavu za wapinzani mara nane huku Felix Sunzu, mchezaji wa kulipwa wa timu hiyo kutoka Zambia, akiwa amefunga mabao matano tu.

“Ugonjwa” wa kutegemea zaidi wachezaji wa kigeni katika upachika huo wa mabao pia unaikabili Yanga.

Kenneth Asamoah, mshambuliaji kutoka Ghana ndiye kinara wa timu hiyo akiwa ameifungia mabao 10 huku Khamis Kiiza, “pro” mwingine raia wa Uganda akiwa amewatungua makipa mara nane na kufuatiwa na Davis Mwape, Mzambia ambaye hata hivyo amefunga mabao manne.

Tofauti na Yanga ya msimu uliopita iliyotwaa ubingwa inaojaribu kuutetea sasa, hakuna Mtanzania yeyote katika kikosi hicho aliyefunga angalau mabao matatu tu.

Vita ya kupambana kutoshuka daraja inayozikabili timu za Kagera Sugar, African Lyon, Villa Squad, Moro United, Polisi Dodoma na Toto African nayo ni kali.

Klabu za Polisi Dodoma, Toto African, Kagera Sugar na Moro United kwa mfano, zina mechi dhidi ya vinara watatu wanaofukuzia ubingwa huku nyingine zikiwa na kazi hiyo kwa timu moja au mbili kati ya hizo, hali ambayo hata zenyewe zinaamini kuwa tayari zimefungwa hata kabla ya kuingia uwanjani.

Mathalani, Toto African si rahisi kuifunga au kutoka sare na Azam au Yanga na hivyo ndivyo ilivyo pia kwa Kagera Sugar; Moro United dhidi ya Simba na Polisi Dodoma ambayo itawakabili vijana wa Jangwani ambao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi hiyo.

Katika hali hiyo, ubingwa wa kandanda Tanzania Bara msimu huu unabaki mikononi mwa Simba, Azam na Yanga huku “Kiatu cha Dhahabu” kikiendelea kumsogelea John Boko ‘Adebayor’.

By Jamhuri