Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Katavi

MABORESHO na ujenzi wa miundombinu ya kisasa inayofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imevutia wawekezaji katika Bandari ya Karema iliyopo Ziwa Tanganyika, mkoani Katavi, Wilaya ya Tangabyika.

Hayo yameelezwa leo kwa Wabunge wenye majimbo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika waliofanya ziara katika bandari ya Kerama kwa ajili ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa meli nne za mizigo zinazojengwa na Kampuni ya Zijin Ltd .

Akizungumza mbele ya Wabunge hao, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe David Kihenzile ameipongeza TPA kwa usimamizi mzuri na kwa kazi nzuri waliyoifanya kuratibu mazungumzo mpaka kupata mwekezaji anayejenga meli hizo za mizigo Ziwa Tanganyika.

“Tunaipongeza timu nzima ya TPA .Pia wawekezaji kwa kazi nzuri ambayo wameanza kuifanya ,tumefurahishwa na kazi inayofanyika.Tumekuja bandari ya Karema kwa kazi moja tu kutembelea na kuona mradi wa ujenzi wa meli nne za mizigo unaofanywa na kampuni ya Zijin Ltd.

“Meli hizi nne zinazojengwa katika bandari hii zitakuwa zinafanya kazi katika ziwa Tanganyika ,Ujenzi wa meli hizi umeanza Aprili 4 mwaka 2025 na zinatarajia kumalizika baada ya miaka miwili na tumeelezwa Julai mwaka 2026 zitakuwa zimekamilika,”amesema Mhe Kihenzile

Kwa upande wake Dkt Boniface Nobeji aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA,amesema kutokana na Ujenzi wa meli hizo TPA itapata dola Milioni moja na elfu hamsini na nane kwa ajili ya eneo linalotumika kujengea.

“Faida za uwekezaji huu unafanywa na kampuni tanzu nyingine ambayo inatokea China yenye mgodi kule Congo DRC wanataka watengeneze meli hapa ambazo zinafanya kazi ndani ya ziwa Tanganyika lakini wakisafirisha shehena ya madini kutoka Manongo.

“Kwahiyo wanajenga meli lakini zitakuwa zinaenda Kalemii na maeneo mengine.Muhimu zaidi ni kuvutia shehena ambayo itapitia Bandari ya Kigoma kisha itaenda Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga.

“Kwahiyo tunategemea kuwa na shehena kubwa sana ya madini inayopita katika bandari zetu na kwenda nchi za nje .Hivyo itachochea biashara zetu katika maeneo yanayozunguka ziwa ziwa Tanganyika na maeneo ambayo yanapita reli ya kati kutokea Kigoma kwa maana reli ya kawaida na reli ya SGR ikikamilika.”

Awali Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Kilumbe Ng’enda amesema hatua hiyo ya kupata mwekezaji ambaye anakaa kwa muda mfupi lakini anaipa Bandari zaidi I a Sh.bilioni mbili ndicho kitu ambacho walikuwa wanatamani kuona kinatokea.

“Meli hizi ambazo zinajengwa hapa zitakuwa zinatumika Ziwa Tanganyika kwa kuleta mizigo kutokea DRC Congo na kupitisha katika bandari zetu kwenda Duniani. Sasa jambo hili ndio tulikuwa tunaliomba siku nyingi kwani Serikali haiwezi kufanya kila kitu lazima ikaribishe sekta binafsi ifanye baadhi ya Kazi kwa kutumia mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali,”amesema Kilumbe Ng’enda.

Ameongeza kuwa ukienda kwenye Bahari ya Hindi Zanzibar na Dar es Salaam Meli zinazofanyq kazi ni za mzee Bakharesa sio za Serikali lakini watu wanafurahia wanapata huduma na Serikali inapata kodi.

“Kwahiyo na hichi kinachofanyika hapa ndicho tulikuwa tunaelekeza siku zote kwamba kama Serikali itakuwa na meli ya Lihemba, Muongozo lakini na meli nyinyine mbili wanajengwa.Hatahivyo Serikali haitaweza kumaliza mahitaji yote ya meli kwa fedha za watanzania.

“Hivyo lazima kukaribisha sekta binafsi kama hicho kilichofanyika watu wanakuja wanajenga meli na meli hizo zitatumika kwa kazi zao lakini wamesema watakapokuwa wanaleta mizigo yao na kama kutakuwa na mtu anamzigo watambebea na watakuwa na makubaliano.”