UJUMBE WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA KWA WAUMINI WAKATOLIKI NA WATU WOTE WENYE MAPENZI MEMA

 

Sisi Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tumekutana katika Mkutano wetu Mkuu wa 65 wa kawaida tangu tarehe 23-30 Juni 2012 uliowajumuisha Wakuu wa Mashirika ya Kitawa, wakuu wa Idara, Tume na Taasisi za Baraza pamoja na wawakilishi Walei.

 

Lengo la Mkutano huu lilikuwa kutathmini shughuli na kazi zetu za Kichungaji na za huduma za jamii kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2009-2012) na vile vile kupanga mikakati ya kuboresha shughuli hizo za Kichungaji na za huduma za jamii katika nyanja za afya, Elimu, maji, misaada kwa wasiojiweza, utetezi na ushawishi, kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo (2012-2015).

 

Pamoja na kufanya tathmini ya kina ya utendaji wa Baraza letu katika kipindi hicho kilichopita, na kupanga mipango kabambe kwa ajili ya utendaji wa Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, Mkutano wetu Mkuu umekuwa fursa ya kujadiliana na kushirikishana baadhi ya matukio/mambo ambayo, kwa hakika, yameitikisa jamii yetu ya Watanzania na kuidhalilisha mbele ya jumuiya ya kimataifa.

 

Kwa namna ya pekee kabisa, tumetafakari juu ya vurugu za kidini za hivi karibuni zilizotokea katika Visiwa vya Zanzibar kuanzia 26-28 Mei, 2012 na kusababisha kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa Visiwani humo pamoja na uharibifu mkubwa wa mali na uvunjifu wa amani.

 

Bila kupenda kurudia matamko ya wadau mbalimbali waliyoyatoa katika nyakati tofauti kulaani bila kusita hali hiyo ya kutisha na kusikitisha iliyojitokeza Visiwani humo, tunaunga mkono kwa nguvu zote kauli na jitihada za wale wote wenye mapenzi mema walioguswa na vitendo hivyo na hivyo kuvilaani.

 

Tunatoa pole na kueleza mshikamano wetu wa kindugu kwa wale wote walioathirika kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo vya vurugu ambavyo vimefanya sehemu ya jamii ya wakazi wa Visiwani humo, hasa Wakristo, kuishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na vitisho vinavyoendelea kutolewa na baadhi ya vikundi pamoja na hali ya kutopewa ulinzi wa kutosha na vyombo husika. Tunaendelea kuwaahidi Sala na mshikamano wetu katika kipindi hiki kigumu.

 

Pamoja na hayo, tunapenda kuwakumbusha Watanzania wenzetu, hasa mamlaka husika kutafakari na kuzingatia busara ya wahenga waliosema kwamba “mwanzo wa makubwa ni madogo” na kwamba “mdharau mwiba mguu huota tende”.

 

Kumbukumbu zinatuambia kwamba, chuki za wazi za kidini zilianza kuinyemelea nchi yetu miaka ya 1990, pale mihadhara ya kashfa za kidini ilipoanza kuruhusiwa.

 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwa kuongozwa na busara ya kichungaji, kwa nyakati tofauti, liliandika barua kuziomba na kuzihimiza mamlaka husika kuingilia kati na kuhakikisha kwamba mihadhara kama hiyo haipati nafasi ya kuendelea katika nchi yetu kwani kamwe haiwezi kuwa na tija isipokuwa kuamsha hisia kali za kidini, jazba na kujenga chuki miongoni mwa waamini wa dini tofauti.

 

Kwa bahati mbaya, ushauri huo wa Baraza la Maaskofu ulipuuzwa na mamlaka husika.

 

Hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la vyombo vya habari ambavyo vimeanzishwa na ambavyo badala ya kuzingatia malengo mazuri ya vyombo vya habari ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, vimeonyesha malengo ya wazi ya kueneza uzushi, kashfa, chuki na uchochezi.

 

Bado kuna CD/DVD na kanda chungu nzima zilizozagaa mitaani zenye malengo kama hayo ambapo, kwa mshangao mkubwa wa raia wema wa nchi hii, licha ya wahusika kufahamika na kuonekana wazi wazi, hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa dhidi yao. Tunachelea hata kudhani kwamba mamlaka za dola zinawakingia kifua wadau wa harakati hizo.

 

Mkusanyiko wa mambo yote haya ndiyo uliotufikisha hapa tulipo. Kwa upendo tulio nao kwa nchi yetu na kwa kuzingatia historia ya mlolongo wa matukio yaliyotufikisha hapa tulipo, tunahofu, lakini kwa uwazi tunapenda kuziambia mamlaka husika, watu wote wenye mapenzi mema na Watanzania wote kwa ujumla, kwamba iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa mara moja ili kurekebisha hali hii, baada ya miaka michache, hakika kwamba nchi yetu inaweza kuingia katika machafuko makubwa ya kidini.

 

Ili kuepuka hali hiyo isitokee, kwa moyo wa unyenyekevu kabisa, tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:-

 

•Sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tutaendelea kusali ili kuiombea nchi yetu amani. Licha ya sala na maombi ya kawaida kwa ajili ya lengo hilo, Mkutano Mkuu umeamua kwamba tutakuwa na siku moja ya kusali kitaifa kwa ajili ya kuomba amani;

 

•Tutaendelea kutumia sauti yetu ya kinabii kuonya, kukemea na kukaripia vitendo vyote vile vinavyoashiria kueneza chuki miongoni mwa watu wa dini mbalimbali;

 

•Kwa kutumia Tume na Idara zetu, tutaendelea kujenga na kueneza mazungumzano na waamini wa dini mbalimbali tukiheshimu tofauti zilizopo. Hii ni kwa sababu tunaamini kwamba suala la dini ni wito na hiari ya mtu na hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kumlazimisha mwingine ajiunge na dini yake.

 

Kwa upande wa wadau wengine na hasa kwa Serikali yetu pamoja na vyombo vyake vya usalama, tunapendekeza yafuatayo:-

 

•Mihadhara, makongamano na mikutano yenye lengo la kutoa kashfa na kuchochea chuki miongoni mwa dini mbalimbali ipigwe marufuku;

 

•Vyombo vya habari vinavyoeneza uzushi, kashfa na uchochezi vidhibitiwe kwa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa;

 

•Uzushi na uongo unaoenezwa na vyombo vya habari na watu wenye lengo la kuwachonganisha Watanzania na waamini wa dini mbalimbali utolewe ufafanuzi mara moja na wizara na vyombo vingine vinavyohusika;

 

•Kuweko na mpango kabambe wa kutoa elimu ya uraia yenye kina na upana katika nafasi zote, itakayowawezesha vijana wetu kuwa wazalendo kwa nchi yao na kuepuka propaganda za kuwagawa Watanzania kwa misingi ya kidini;

 

•Suala la ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, liangaliwe kwa makini kwani linaweza kuwa moja ya sababu zinazowafanya vijana wengi kujiingiza katika vikundi vya kidini vinavyojenga chuki na kutoa matumaini ya uongo;

 

•Lakini, zaidi ya yote, iwapo Serikali yetu na mamlaka husika inataka kuwa na imani mbele ya jamii kwamba ina nia thabiti ya kuhakikisha kwamba vurugu za kidini hazipati nafasi katika nchi yetu, wale wote wanaohusika na vurugu hizo wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.

 

Ni vigumu kuamini kwamba katika kipindi cha kuanzia mwaka 2001 mpaka sasa, makanisa 25 yamekwishachomwa moto Visiwani Zanzibar, lakini hakuna aliyekamatwa na kuchuliwa hatua za kisheria.

 

Tumefanya mkutano wetu katika mazingira ya kuwapo mvutano kati ya madaktari na serikali na kwa bahati mbaya sana, kama tulivyokwisha kutamka huko nyuma, mvutano huu unaleta athari kubwa kwa raia wasio na hatia, athari ambayo haiwezi kurudishwa.

 

Uhai wa raia wa Tanzania unaangamia kwa kukosa ulinzi wa tiba. Katika hili tunapenda kukumbusha kuwa kila mmoja ni mdau. Hakuna hata mmoja anayeweza kulikwepa hili.

 

Tunapenda kurudia himizo letu la awali kwamba ni bora ikapatikana njia nyingine iliyo mwafaka zaidi ya kudai haki na mazingira yanayofaa ya kazi bila kuleta madhara ya kupoteza uhai ambao ni haki msingi ya kila mwanadamu.

 

Tunaiasa Serikali yetu ikae tena pamoja na madaktari na kuchambua hoja zitakazowekwa mbele yao. Uwazi na ukweli vikitawala hakuna pande itakayokataa kuridhia eti kwa sababu ya kukataa tu bila hoja. Taifa letu limejipatia aibu mbele ya macho ya ulimwengu ya jinsi tunavyoshindwa kuishi kile tunachosema kwenye majukwaa.

 

Mwisho, tunaendelea kuwaalika Watanzania wenzetu, hasa viongozi wa dini mbalimbali kuwahamasisha waamini wao wawe raia wema wa nchi hii kwa kuungana pamoja kuhamasisha upendo, haki, amani na maridhiano miongoni mwa Watanzania wote. Licha ya tofauti zetu, tuzingatie hasa yale yanayotuunganisha: ubinadamu wetu na uraia wetu wa nchi yetu Tukufu ya Tanzania ambamo tutake tusitake, ni lazima wote tuishi.

 

Tuepe ushindani ambao hauna tija isipokuwa kutupeleka katika kujenga chuki na hali ya kudhaniana vibaya miongoni mwa waamini wetu. Iwapo kuna sababu ya kushindana, tushindane katika kubuni mbinu za kujenga upendo na amani miongoni mwa Watanzania katika kutafuta njia za kuwaletea maendeleo yatakayowatoa kutoka katika umaskini, ujinga na maradhi ambao ndiyo adui wetu sote.

 

Tunaiombea nchi yetu amani na usalama.

 

Jude Thaddaeus Ruwai’chi

RAIS: BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA/ASKOFU MKUU JIMBO LA MWANZA

 

 

By Jamhuri