Serikali ya Muungano ya Ujerumani imekubaliana juu ya mpango wa kuhalalisha kisheria matumizi ya bangi kama kiburudisho miongoni mwa watu wazima.

Mtu ataruhusiwa kumiliki na hadi gramu 30 (1oz) kwa ajili ya matumizi ya kibinafsi. Maduka ya kawaida yaliyopewa leseni na maduka ya dawa yatauza bangi.

Mpango bado haujaidhinishwa katika Bunge lakini umeidhinishwa na Tume ya Muungano wa Ulaya. Waziri wa afya wa Ujerumani Karl Lauterbach alisema kuwa mpango huo unaweza kuwa sheria katika mwaka 2024.

Katika Muungano wa Ulaya ni Malta pekee ambayo ilihalalisha kisheria matumizi ya bangi kama kiburudisho.

Uholanzi imefikia hatua sawa na mpango wa Ujerumani – chini ya sheria ya Uholanzi, mauzo ya kiasi kidogo cha bangi “katika maduka ya kuuza kahawa” yanakubalika.

Mpango wa Ujerumani pia utaruhusu nyumba kupanda mimea mitatu ya bangi kwa kila mtu mzima.

Hatua hiyo ilikuwa ni miongoni mwa ajenda za serikali ya muungano, zilizotangazwa mwaka jana. Muungano huo unaongozwa na Chama cha Social Democrats (SPD) kikiwa pamoja na kile cha Kijani na liberal Free Democrats kama washirika.

Nchi kadhaa zimehalalisha kisheria matumizi madogo ya kimatibabu ya bangi. Canada na Uruguay pia zimehalalisha bangi kama kiburudisho.

Ripoti ya mwaka 2019 kutoka Taasisi ya kimataifa inayoshughulika na masuala ya bangi Afrika (Africa Regional Hemp and Cannabis), zinaonyesha Afrika inachangia dola milioni $37.3 kwenye soko la dunia la bangi ambayo ni sawa na asilimia 11.

Kwa sasa dunia inashuhudia nchi nyingi zikiifanya bangi kuwa zao halali na kuanza kulimwa kwa wingi. Ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia uhalifu na dawa za kulevya (UNODC), inasema kati ya mkwa 1995 mpaka 2005, nchini 19 kati ya 53 barani Afrika ziliripoti kuzalisha bangi au marijuana.

Morocco ni nchi ya hivi karibuni kutoka Afrika kuruhusu kilimo cha bangi kwa matumizi ya dawa na viwanda. Afrika Kusini, Ghana, Uganda ni nchi zenye uelekeo huo licha ya kuwa na sheria zinazokataza matumizi yake kwa starehe.