Saratani ni muunganiko wa magonjwa ambayo mara zote husababishwa na uzalishwaji wa seli za mwili kupita kiasi kinachohitajika mwilini, na seli hizo huendelea kujigawa kupita kiasi na kutengeneza kiasi kikubwa kuliko mwili unavyoweza kuhimili.

Ukuaji huu wa seli hizi unaweza kusababisha vimbe mbalimbali katika mwili na uvimbe unavyokuwa mkubwa unasababisha kubanwa kwa baadhi ya viungo muhimu mwilini kama vile neva, mishipa ya damu, ubongo, mapafu na vingine na kutofanya kazi yake vizuri.

Lakini pia si kila uvimbe ni saratani. Kuna saratani za aina nyingi sana. Tafiti za kisayansi zinaonyesha zaidi ya aina 100 za saratani zinawapata watu na kwa kawaida huwa ni vigumu sana kutambua pale unapoanza, mara nyingi mgonjwa anajitambua baada ya ugonjwa kukomaa mwilini.

Kwa kuwa saratani ni ugonjwa ambao kwa kawaida huwa unakuja kwa kujificha sana, ni vigumu sana kwa mtu kujitambua kama ana ugonjwa huu wa saratani au yupo katika hatari ya kushambuliwa na ugonjwa huu kutokana na uelewa mdogo sana kuhusu saratani.

Dalili kama uvimbe, kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwilini ambako si kwa kawaida, kukohoa sana na kikohozi kisichokwisha, kupoteza uzito kwa kasi na mabadiliko katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, ukiona dalili hizi, haupaswi kuzifumbia macho, huenda ukawa hatarini kuugua saratani.

Madoa madoa na uvimbe mpya kwenye ngozi, au kingo za ngozi kubadilika umbile muonekano wake halisi na hata rangi, ni ishara ya saratani ya ngozi. Kingine ni vipele vikubwa ambavyo huwa vinavimba na ukivitomasa unahisi ugumu sana ndani yake na vinaambatana na maumivu ya kawaida.

Vipele hivi vinaweza kutokea sehemu yoyote ya mwili na kwa muonekano wake havifanani kabisa na vipele vya magonjwa ya ngozi ya kawaida. Kama unaona kwenye ngozi una alama ambazo unahisi si za kawaida, ni vizuri kumuona daktari ili akufanyie vipimo vya ngozi.

Daktari ataondoa sehemu ndogo ya ngozi yako na kuifanyia vipimo ili kuangalia uwezekano wa uwepo wa seli za saratani katika ngozi yako. Kipimo hiki cha kuondoa sehemu ya ngozi kitaalamu kinaitwa ‘Biopsy’.

Mabadiliko kwenye matiti, si kila mabadiliko yanayotokea kwenye matiti yanaashiria saratani. Lakini pia bado ni muhimu sana kuwasiliana na daktari kuhusu mabadiliko yoyote yanayojitokeza kwenye matiti ili ayafanyie uchunguzi.

Mjulishe daktari  kuhusu uvimbe wa aina yoyote, mabadiliko katika chuchu ikiwemo kuziba kwa chuchu, uwepo wa rangi nyekundu au kuhisi ugumu, au maumivu kwenye matiti kwa ujumla. Daktari atakufanyia kipimo cha X-ray kwenye titi. Kipimo hiki kwa kitaalamu kinaitwa ‘Mammogram’. Kipimo hiki kinatumika kuchunguza saratani ya matiti kwa wanawake ambao hawana dalili za saratani ya matiti.

Kujaa gesi mfululizo, mara nyingi unaweza kuhisi unajaa gesi tumboni, yaweza kuwa ni aina ya vyakula unavyokula au kiafya hata msongo mkubwa wa mawazo pia una uhusiano mkubwa na matatizo ya kujaa gesi.

Lakini pia kama hali hii inadumu kwa muda mrefu inaweza kusababisha uchovu, kupungua uzito na  maumivu ya mgongo, basi ni vema kupatiwa vipimo. Kujaa gesi kwa muda mrefu kwa wanawake ni ishara kubwa ya saratani ya mayai ya uzazi (ovarian cancer).

Ili kuchunguza aina hii ya saratani, daktari anachunguza sehemu za ndani za via vya uzazi kama mlango wa kizazi (cervix), mayai ya uzazi (ovaries), mrija wa falopia (fallopian tube), mfuko wa uzazi (uteras), na uke (vagina). Kipimo hiki kitaalamu kinaitwa ‘pelvic examination’.

Matatizo wakati wa haja ndogo, wanaume wengi hupatwa na matatizo ya njia za mkojo kadiri umri unavyokuwa mkubwa. Wale wanaoingia katika rika la uzee ndio wahanga hasa. Matatizo haya ni kama kujisikia kukojoa mara kwa mara, mkojo kuvuja matone machache hata kabla ya kwenda haja lakini hata pia njia ya mkojo kuwa dhaifu.

Kwa kawaida hizi ni ishara kuwa tezi dume imeongezeka ukubwa wake wa kawaida au imepata uvimbe na hivyo kuashiria saratani ya tezi dume. Ni vema kumuona daktari haraka na ni muhimu pia kufanyiwa vipimo maalumu vya damu ambavyo kitaalamu vinaitwa Prostate Specific Antingen Test (PSA). Kipimo hiki ni maalumu kwa ajili ya kuchunguza saratani ya tezi dume.

Please follow and like us:
Pin Share