Kesho Mei 25 ni Siku ya Afrika, siku ambayo imewekwa na Umoja wa Afrika (AU) kwa nia ya kukumbuka na kutathmini nguvu na uwezo uliofanywa na Umoja huo katika harakati za kukomboa nchi za Bara la Afrika.

Historia ya Umoja huo inaanzia tangu Mwafrika alipokataa kuvunjiwa utu wake na kujenga harakati za kudai uhuru na ukombozi wake kutokana na kuonewa, kudhalilishwa na kunyonywa na wakoloni ambao kwa kweli wamechukua mali nyingi za mama Afrika bila ya ridhaa ya watoto wa Afrika.

Kuanzishwa kwa vyama vya ukombozi katika nchi mbalimbali Afrika, Umoja wa Vyama vya Ukombozi vya Afrika Mashariki na Kati (Pan African Freedom Moment for East and Central Africa-PAFMECA)  zikiwamo nchi za Kenya, Uganda, Tanganyika, Malawi, Zambia na Zanzibar katika Umoja huo.

Nchi sita hizo ziliunda Umoja huo na kuzaliwa kwake mjini Mwanza Septemba 1958 na kumchagua Mwenyekiti wake kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Vijana wa Afrika nao hawakuwa nyuma katika harakati za ukombozi huo. Walianzisha Umoja wa Vijana wa Afrika na kumteua kijana shupavu, Kingunge Ngombale-Mwiru kuwa Katibu Mkuu wake. 

Harakati za ukombozi zilipamba moto na baadhi ya mambo yakipewa uzito wake kama vile kupinga ukoloni na kupambana na ukoloni mamboleo na ubeberu, ulioendeshwa katika nchi za Afrika. 

Katika mapambano hayo dhidi ya ukoloni, ukweli mapambano yaliyoendeshwa yakitumia silaha na kutumia katiba, yalishamiri na nchi moja baada ya nyingine ilijikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni. Ukombozi huo ulipofikisha mwaka 1987, nchi zipatazo 50 barani Afrika zilikwishapata uhuru.

Mkikimkiki huo wa ukombozi ulitoa njia pia ya kuundwa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika mwaka 1963. Juhudi hizo zilikamilisha kuundwa rasmi Umoja wa Nchi Huru za Africa (Organization of Afrika Union-OAU) mnamo Mei 25, 1963 mjini Adis Ababa, Ethiopia. Leo Umoja huo unaitwa Umoja wa Afrika (AU).

Hakika, Umoja huo ulianzishwa na nchi huru 30 chini ya viongozi wao wakuu Tanzania ikiwa nchi mojawapo. Ukweli, historia ya ukombozi wa Mwafrika ni ndefu na safu hii haitatosheleza. Nimetoa kwa ufupi historia hiyo kuonesha siku yake ina umuhimu gani kwa mtoto wa Afrika.

Lengo langu ni kujiuliza shabaha ya uhuru na ukombozi wa Mwafrika tangu uhuru wa nchi ya Gold Coast sasa Ghana mwaka 1957 hadi uhuru wa nchi ya Afrika Kusini mwaka 1994, ikiwa ni nchi ya mwisho kujikomboa barani Afrika. Je? Kwa harakati hizo Mwafrika amejikomboa?

Mwafrika huyu ninamwangalia katika mambo yafuatayo: Mwenendo na msimamo wake kisiasa, amepevuka na kujikomboa? Anajitambua kwa kauli zake azitamkazo, anatekeleza yale anayoahidi? Nafsi yake inatambua na kuthamini nafsi ya Mwafrika mwenzake? 

Namwangalia Mwafrika huyu kiuchumi; tangu apate uhuru wake amekwea kwa asilimia ngapi kutoka kwenye lindi la umaskini? Uchumi alionao kwa maana ya rasilimali ardhi, misitu, madini na nguvukazi watu; ameitumia kwa faida yake au ameikalia tu? Ni kweli hajisaliti mwenyewe katika kutawanya uchumi wake kwa watu wengine wasiohusika?

Najaribu kumtazama Mwafrika huyu katika kulinda utu na Bara lake la Afrika. Mwafrika huyu anajitambua kuwa yeye ni lulu mbele ya watu wa mataifa ya ughaibuni? Vipi leo yeye mwenyewe amekuwa mstari wa mbele kupokea mapesa kutoka kwa mabepari kwa kutaka kuiangamiza nchi yake?  Uhaini huu anaufanya kwa faida ya nani?

Mwafrika huyu anapojifanya hamnazo kwa kutoangalia tamaduni, mila na desturi zake badala yake kuzipa hadhi na heshima tamaduni za ughaibuni –  kweli yuko sawa? Anashindwaje kulinda na kutetea tamaduni zake lakini anaweza kulinda na kuzipalilia zile za nchi za kigeni? 

Nini faida ya kudai uhuru wa nchi na ukombozi wa Mwafrika? Waasisi wa ukombozi barani Afrika wakiwamo Kwame Nkrumah wa Ghana, Jomo Kenyatta wa Kenya, Haile Selassie wa Ethiopia, Sekeu Toure wa Guinea,  Sir Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria, Francis Tombalbaye wa Chad, William Tubman wa Liberia na Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania. 

Mwafrika; una nini hata unashindwa kujikomboa kifikra? Uhuru wako umerudishwa na nchi yako ipo huru, iweje unajisaliti, unajihaini na unajidhulumu utu wako daima dumu?  Jirekebishe.

By Jamhuri