Anne MakindaMapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Bunge, ya kumlipa kila mbunge mafao ya Sh milioni 238 baada ya Bunge kuvunjwa mwezi ujao, yanazidi kuichanganya Serikali.
Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa tayari Serikali inakabiliwa na ukata mkubwa, kiasi cha kusuasua kuwalipa wabunge mishahara yao ya kila mwezi. Mishahara ya mwezi Mei ililipwa mwanzoni mwa mwezi huu.
Mzigo wa malipo hayo mapya yanayopendekezwa sasa umesukumwa kwa Rais Jakaya Kikwete, ili endapo ataridhia, basi mafao hayo yalipwe kwa wabunge wote 357 waliopo kikatiba.


Endapo Rais Kikwete ataridhia mapendekezo ya Tume, walipa kodi wa Tanzania watalazimika kukamuliwa Sh bilioni 85.024 ili kuwalipa wabunge hao mafao yao.
Tayari wananchi na wanaharakati mbalimbali wamekwishaonyesha wazi kupinga mpango huu wa wabunge wa kujineemesha. Wanaopinga wanasema jamii inakabiliwa na matatizo makubwa, hasa ya ukosefu wa huduma muhimu za kijamii, hivyo si jambo la busara kutumia Sh bilioni 85 kuwalipa wabunge mafao.
Nyaraka ambazo JAMHURI inazo zinaonyesha kuwa Tume imetoa mapendekezo mengi yenye kulenga kuwanufaisha Spika, Naibu Spika, Wabunge, Wajumbe wa Tume na Watumishi wanne wa kila mbunge.


Mapandekezo haya yanajengewa hoja ya kihistoria kwamba wabunge wengi wamekuwa kwenye wakati mgumu kimaisha pindi wanapokosa ubunge.
Mtiririko mzima wa namna wabunge wanavyoandaliwa ulaji huu tunauchapisha neno kwa neno hapa chini.
Ulaji unaopendekezwa


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 62 ya Katiba ambapo mshahara na marupurupu mengine ya wabunge yameelekezwa katika Ibara ya 73 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kutokana na msingi wa Katiba hii, Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Spika, Naibu Spika, Wabunge na Wajumbe wa Tume hulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Hitimisho la Kazi ya Viongozi wa Kisiasa Sura Na. 225 ya mwaka 1999 pamoja na Sheria ya Marekebisho mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2005.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi ya Sheria ya Marekebisho, mafao hayo kama ifuatavyo:-


(a)    Spika wa Bunge
Spika anastahili kulipwa Kiinua Mgongo kinachokokotolewa kwa kiwango cha asilimia hamsini (50%) ya mshahara wa mwisho kwa kipindi chote alichotumikia wadhifa wa Spika, pensheni ya kila mwezi iliyo sawa na asilimia themanini (80%) ya mshahara wa Spika wa sasa, Posho ya Hitimisho la kazi (winding-up allowance) sawa na mishahara ya miezi itakayoamuliwa na mamlaka husika pamoja na stahili nyinginezo. Aidha, Spika ambaye ni Mbunge anastahili kulipwa posho nyinginezo kadiri itakavyoamuliwa na mamlaka.


(b)    Naibu Spika
Naibu Spika anastahili kulipwa Kiinua Mgongo cha kiwango cha asilimia hamsini (50%) ya jumla ya mshahara katika kipindi chote alichotumikia wadhifa wa Naibu Spika. Aidha, anastahili kulipwa Posho ya Hitimisho la Kazi sawa na asilimia ya jumla ya mishahara aliyolipwa katika kipindi chote alichotumikia wadhifa wa Naibu Spika itakavyoamuliwa na mamlaka husika.

Naibu Spika ambaye ni Mbunge anastahili kulipwa posho zinginezo itavyoamuliwa na mamlaka.

(c)    Wabunge
Kifungu cha 21 cha Sheria ya Hitimisho la Kazi ya Viongozi wa Kisiasa Sura Na. 225 na Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na.2 ya mwaka 2005, ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 19(2)(d)(iii) cha Sheria ya Uendeshaji Bunge Sura Na. 115 ya mwaka 2008, kinabainisha kuwa Wabunge wanastahili kulipwa mafao kama ifuatavyo:-

(i)    Kiinua Mgongo (gratuity) cha asilimia 40 ya mishahara ya miezi katika kipindi alichotumikia nafasi ya ubunge;
(ii)    Posho ya Hitimisho la Kazi (winding-up- allowance) ya asilimia ya kiinua mgongo;
(iii)    Posho ya usumbufu (Relocation allowance) na;
(iv)    Posho nyinginezo kadiri itakavyoamuliwa na mamlaka (other allowances).

(d)    Wajumbe wa Tume ya Bunge
Kwa mujibu wa kifungu cha 16(3) cha Sheria ya Uendeshaji Bunge Sura Na. 115 ya mwaka 2008, Wajumbe wa Tume wanaendelea kutekeleza majukumu yao hadi Wajumbe wapya wa Tume wanapochaguliwa au kuteuliwa. Hivyo, Wajumbe wa Tume wanastahili kulipwa mafao kama ifuatavyo:-
(i)    Kiinua mgongo cha asilimia ya mishahara ya miezi katika kipindi walichotumikia nafasi ya ujumbe wa Tume.
(ii)    Posho ya Hitimisho
(iii)    Posho ya Usumbufu; na
(iv)    Posho nyinginezo kadiri itakavyoamuliwa na mamlaka (Other allowances).
Pamoja na Mafao haya, kwa mujibu wa kifungu cha 21 (3) cha Marekebisho ya Sheria ya Hitimisho la Kazi katika Utumushi wa kisasa mwaka 2005 (written laws (miscellaneous amendments No. 2, 2005), Spika, Naibu Spika, Mbunge na Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge wanapomaliza kipindi chao cha Ubunge/Ujumbe wanastahili kulipwa posho na mafao mengine kama itakavyoamuliwa na mamlaka husika.
Kwa mujibu wa kifungu cha 24 (1) (b) cha sheria husika posho na mafao ya Spika, Naibu Spika, Wajumbe wa Tume na Wabunge yanaweza kuhuishwa na mamlaka baada ya miezi isiyopungua hamsini kuanzia tarehe ya uhai wa Bunge baada ya kushauriwa na Tume ya Utumishi wa Bunge.

Aidha, mafao waliyolipwa Spika, Naibu Spika, na Wabunge kwenye Bunge la Tisa ambalo ukomo wake uliishia mwaka 2010 ilikuwa ni kama ifuatavyo:-
(a) Spika wa Bunge
Spika alilipwa mafao yafuatayo:
(i)    Asilimia 50 (50%) ya mshahara wa mwisho kwa kipindi chote alichotumikia wadhifa wa Spika;
(ii)    Asilimia 80 (80%) ya mshahara wa Spika wa sasa; na
(ii) Posho ya Hitimisho la Kazi (Winding- up Allowance) sawa na jumla ya mishahara ya miezi ishirini na nne (24) anayolipwa Spika wa sasa
b) NAIBU SPIKA
Naibu Spika alilipwa :-
i) Kiinua Mgongo cha asilimia 50% ya mishahara katika kipindi chote
ii) Posho ya Hitimisho la Kazi sawa na asilimia 10% ya jumla ya mishahara aliyolipwa katika kipindi chote
iii) Posho ya Usumbufu (Relocation Allowance) ya asilimia 40% ya Kiinua Mgongo

c) WABUNGE
Wabunge walilipwa mafao kama ifuatavyo:
i)Kiinua Mgongo cha asilimia 40% ya mishahara
ii)Posho ya Hitimisho la Kazi ya asilimia 60% ya kiinua mgongo na;
iii)Posho ya Usumbufu (Relocation Allowance) ya asilimia 40% ya Kiinua Mgongo

d) WAJUMBE WA TUME
Wajumbe wa Tume ya Bunge hawakulipwa mafao ya ujumbe wa Tume na badala yake walilipwa tu mafao ya kazi ya ubunge
Madhumuni ya Waraka huu ni kuwasilisha:-
a) Mapendekezo ya kuhuisha viwango vya sasa vya Malipo ya Posho ya Hitimisho la Kazi
b) Mapendekezo ya Posho Mpya kwa ajili ya Muda wa Mpito (Transition Allowance) na Posho ya Mafao kwa watumishi wanne (4) wa mbunge wanaotambulika kisheria na
c) Majumuisho ya gharama za malipo ya Mafao ya Wabunge baada ya Hitimisho la Kazi mwezi Julai 2015.

    MSINGI WA MAPENDEKEZO
Msingi wa kuwasilisha mapendekezo haya ni kama ifuatavyo:-
Utekelezaji wa sheria
Tume imepewa mamlaka kwa mujibu wa kifungu 24(1)(b) cha Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Kisiasa kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho Mbalimbali  Na. 2 ya mwaka 2005 ya kuhuisha na kupendekeza kwa Rais viwango vya Posho na Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Spika, Naibu Spika, Wajumbe wa Tume wa Wabunge baada ya miezi isiyopungua hamsini kuanzia tarehe ya uhai wa Bunge.
Mzunguko Mpya wa Bajeti (New Budget Cycle)
Kutokana na mzunguko mpya wa Bajeti ya Serikali, Mheshimiwa Rais atalazimika kuvunja Bunge mapema mwezi Julai, 2015 badala ya mwezi Agosti kama ilivyokuwa awali. Utaratibu huu utawaathiri Wabunge wengi wenye mikopo kwa kuwa walikopa kwa matarajio kuwa uhai wa Bunge ungekuwa miezi sitini na badala yake watalipwa kwa miezi hamsini na saba (57) na hivyo, kuwajibika kulipa tofauti hiyo toka katika Kiinua Mgongo.
Haki ya Kulipa Kifuta Jasho kwa Watumishi wa Mbunge
Kwa mujibu wa kifungu cha 19(2)(d)(iii) cha Sheria SURA NA.115 ya mwaka 2008, Mbunge ana Watumishi wanne (4) ambao kwa mujibu wa Sheria SURA NA 225 ya Mwaka 1999 pamoja na Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.2 ya Mwaka 2005 hawalipwi stahili yoyote baada ya Wabunge kuhitimisha kazi yao ya Ubunge. Hivyo, ili kulinda na kutekeleza misingi ya utawala bora, Tume inapendekeza posho mpya ya Kifuta Jasho kwa Watumishi hao.

UCHAMBUZI KUHUSU MAFAO
Kiwango cha posho ya Hitimisho la Kazi
a)Ukokotoaji kwa kuzingatia Asilimia Sitini (60% Scenario )
Mwaka 2010 Wabunge walilipwa Posho ya Hitimisho la Kazi (Winding-up Allowance) ya asilimia 60 ya malipo ya Kiinua Mgongo. Kwa kuzingatia kiwango cha mshahara wa sasa wa Wabunge wa shilingi 3,920,000 kila Mbunge anatarajia kulipwa Posho ya Hitimisho la Kazi ya shilingi 48,921,600 baada ya kuhitimisha kipindi cha ubunge. Endapo Wabunge watalipwa kwa 60% Serikali itatumia shilingi 17,367,168,000 kugharamia malipo ya Kiinua Mgongo kwa Wabunge wote wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
b) Ukokotoaji kwa kuzingatia pendekezo la asilimia 75 (75% Scenario)
Endapo Serikali itaongeza kiwango cha malipo ya kiinua Mgongo kwa asilimia 25 na kulipa posho hiyo kwa asilimia 75 ya malipo ya Kiinua Mgongo kila Mbunge atalipwa Posho ya Hitimisho la kazi ya shilingi 61,152, 000. Aidha, endapo Wabunge watalipwa asilimia 75% Serikali itatumia shilingi 21,708,960,000 kugharamia malipo ya Kiinua Mgongo kwa Wabunge wote.
(C) Ukokotoaji kwa kuzingatia pendekezo la asilimia 85 (85%) Scenario)
Endapo Serikali itaridhia kuongeza kiwango cha malipo ya kiinua Mgongo kwa asilimia 42 na kulipa posho hiyo kwa asilimia 85 ya malipo ya kiinua mgongo kila Mbunge atalipwa Posho ya Hitimisho la Kazi ya shilingi 69,305, 600. Aidha, Serikali itatumia shilingi 24,603,488,000 kugharamia malipo ya Kiinua Mgongo kwa Wabunge wote.


MTIRIRIKO WA MAPENDEKEZO
Kutokana na uchambuzi uliofanyika, inapendekezwa kwamba:-
Tume ihuishe mafao ya Viongozi wa Bunge, yaani, Spika, Naibu Spika na Wajumbe wa Tume ya Bunge kama ifuatavyo:-
(a) Spika wa Bunge  
Spika wa Bunge alipwe mafao kama ifuatavyo:-
*Kiinua Mgongo cha Asilimia 50 ya Mshahara wa mwisho;
*Posho ya Hitimisho ya kazi sawa na mishahara ya miezi            itakayoamuliwa na mamlaka husika;
*Posho ya Muda wa Mpito (Transitional Allowance);
*Malipo ya Kifuta Jasho kwa Watumishi wanne walioko katika Ofisi yake ya Jimbo; na
*Stahili zingine zilizotajwa kwenye Sheria.
(b) Naibu Spika
Naibu Spika alipwe mafao kama ifuatavyo:-
*Kiinua Mgongo cha Asilimia 50 ya Mshahara wa mwisho;
*Posho ya Hitimisho ya Kazi sawa na mishahara ya miezi itakayoamuliwa na mamlaka husika;
*Posho ya Muda wa Mpito (Transitional Allowance);
*Malipo ya Kifuta Jasho kwa Watumishi wanne walioko katika Ofisi yake ya Jimbo; na
*Stahili zingine zilizotajwa kwenye Sheria.
(c) Wajumbe wa Tume
Wajume wa Tume walipwe mafao kama ifuatavyo:-
*Kiinua Mgongo cha asilimia ya mishahara ya miezi katika kipindi walichotumika katika nafasi ya Ujumbe wa Tume;
*Posho ya Hitimisho;
*Posho ya Usumbufu;
*Posho ya Muda wa Mpito (Transitional Allowance);
*Kifuta Jasho cha Watumishi wanne walioko katika Ofisi zao za Majimbo;
(d) Wabunge
Wabunge walipwe Mafao kama ifuatavyo:-
*Kiinua Mgongo cha asilimia ya mishahara ya miezi katika kipindi walichotumika nafasi ya Ujumbe wa Tume;
*Posho ya Hitimisho;
*Posho ya Usumbufu;
*Posho ya Muda wa Mpito (Transition Allowance); na
*Kifuta Jasho cha Watumishi wanne walioko katika Ofisi zao za Majimbo.
Tume iridhie kiwango cha malipo ya mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Wabunge na Wajumbe wa Tume kwa asilimia 75% au asilimia 85% kama Mheshimiwa Rais atakavyoona inafaa.

(a)  Mchanganuo wa mafao kwa kuzingatia pendekezo la asilimia 75% itakuwa ni kama ifuatavyo:-
NA
Aina ya Mafao
Jumla ya Mafao kwa Mbunge
Jumla ya Mafao kwa Wabunge wote
1
Kiinua Mgongo (Gratuity 40% of salary)
89,376,000
31,728,480,000
2
Posho ya Hitimisho la Kazi (Winding Up Allowance 75% of Gratuity)
67,032,000
23,796,360,000
3
Posho ya Usumbufu (Relocation Allowance 40% of Gratuity)
35,750,400
12,691,392,000
4
Posho ya Mpito (Transition Allowance 3 months salary)
11,760,000
4,198,320,000
5
Mafao ya Watumishi wa Mbunge
25,308,000
9,034,956,000

             JUMLA KUU
229,226,400
81,375,372,000
 
(b)  Mchanganuo wa Mafao kwa kuzingatia pendekezo la asilimia 85% itakuwa kama ifuatavyo:-
NA
 Aina ya Mafao
Jumla ya Mafao kwa Mbunge
Jumla ya Mafao kwa Wabunge Wote
1
Kiinua Mgongo (Gratuity 40% of Salary)
89,376,000
31,907,232,000
2
Posho ya Hitimisho la Kazi (Winding Up Allowance 85% of Gratuity)
75,969,600
27,121,147,200
3
Posho ya Usumbufu (Relocation Allowance 40% of Gratuity)
35,750,400
12,762,892,800
4
Posho ya Mpito (Transitional Allowance 8 months salary)
11,760,000
4,198,320,000
5
Mafao ya Watumishi wa Mbunge
25,187,500
9,034,956,000

     JUMLA KUU
238,043,500
85,024,548,000
 
Kuanzisha Posho ya Muda wa Mpito (transition allowance)
Tume inapendekeza kuanzisha posho hii kutokana sababu zifuatazo:-
(a)    Wabunge na Wategemezi wao kwa hivi sasa wanapata matibabu kupitia utaratibu wa huduma ya Bima ya Afya kama sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kifungu cha 24 cha Sheria ya Uendeshaji Bunge Sura. Na. 115 ya mwaka 2008. Kuna baadhi ya wabunge ambao wanahitaji kuendelea kupata huduma kutokana na udhaifu wa afya zao. Aidha, kwa kuwa huduma ya Bima ya Matibabu wanayopata wabunge kupitia wakala wa Jubilee Insurance itakoma kisheria mwezi Julai, 2015 baada ya ukomo wa uhai wa Bunge hivyo, inashauriwa na Tume kwamba wabunge walipwe posho mpya ya mpito (transitional Allowance) ili kuwasaidia kulipia gharama za matibabu na mahitaji mengine.

(b)    Mzunguko mpya wa Bajeti ya Serikali kwa kiasi kikubwa utaathiri ulipaji wa mikopo ya wabunge. Kwa msingi huo, inashauriwa na kupendekezwa kuwa wabunge walipwe Posho ya Muda wa Mpito ambayo itakuwa sawa na mishahara ya miezi nane bila ya malipo ya posho ya ubunge (constituency allowance). Endapo Serikali itakubali pendekezo hili kila mbunge atalipwa Posho ya Muda wa Mpito ya Sh 31,360,000. Aidha, Serikali itatumia Sh 11,132,800,000 kugharamia malipo ya posho ya muda wa mpito kwa wabunge.
Kuanzisha Posho ya Kifuta Jasho kwa Watumishi wa Mbunge
Kama ilivyoelekezwa katika aya ya 2.3, kwa mujibu wa kifungu cha 19 (2) (d) (iii) cha Sheria Sura Na. 115, Mbunge ana watumishi wanne (4) ambao hawaguswi kwenye Sheria Sura Na. 225 ya mwaka 1999 na marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2005 kupata stahili yoyote baada ya wabunge kuhitimisha kazi yao ya ubunge. Kwa msingi huu na ili kutekeleza dhana ya utawala bora inapendekezwa kwamba Serikali ikubali kuwalipa kifuta jasho watumishi hawa kwa kiwango cha asilimia 25 ya mishahara yao kulingana na kipindi ambacho mbunge amekuwa madarakani.

 

By Jamhuri