Lowassa pembaChama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibuka na hofu mpya juu ya kudhuriwa kwa mgombea urais wa chama hicho kwa kofia ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kutokana na hali hiyo, umoja huo sasa umeimarisha ulinzi kwa kiongozi huyo pamoja na wale wote wa Ukawa baada ya kuibuka madai kwamba huenda “maadui” wakatumia nafasi ya kujitokeza watu kwa wingi kuwadhuru.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amethibitisha kwamba wameongeza ulinzi kwa viongozi hao hususani Lowassa kwa kuwa anastahili ulinzi wa ziada ili kumlinda na wabaya wake (CCM).

Anasema kwamba wamefanya hivyo kwa hofu inayoweza kufanywa na watu wanaoitakia mabaya Ukawa kwani wanaweza kufanya vitendo vya kigaidi ambavyo hufanyiwa wanasiasa wa upinzani.

“Nilimwambia Lowassa huku ni upinzani, kwa hiyo ajiandae kwa virungu. Na kwa hali hii sisi tumeamua kumuongezea ulinzi maana kuna wakati jeshi la polisi haliaminiki,” anasema Mbowe kwa umakini.

Mbowe amesema kwamba anachokifahamu yeye ni kwamba CCM kwa sasa wanahangaika na kwamba hawana namna nyingine ya kupambana na Ukawa zaidi ya kuwadhuru katika vitendo viovu.

Mbowe anasema: “Kwa sasa Lowassa ndiye adui namba moja wa CCM. Hawampendi na hilo tumeliona na tunaona ni wazi kuwa   na waovu hawa wako tayari kufanya kila hila yoyote dhidi ya Ukawa.”

Anasema kwamba uadui huo unatokana na juhudi za CCM kutaka Lowassa abaki CCM baada ya kunasa sauti kwamba anataka kuhama kwenda Chadema mwishoni mwa mwezi uliopita.

Katika hatua nyingine Mbowe anasema kwamba wakati wa uchaguzi, katu hawatakubali kuibiwa tena kura na kuanza kulalamika kwani wana uhakika wa kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Mbowe anatoa kauli hiyo baada ya kuibuka madai kwamba Lowassa na Chadema wamejiongezea ulinzi katika kile kinachodaiwa kufanya vurugu kama ikitokea wameshindwa uchaguzi.

Mbowe amelazimika kusema hayo baada ya kuibuka taarifa kwamba Lowassa amekuwa na vikao na viongozi wa Ukawa ambako akahoji idadi ya walinzi wa Red Brigade. Mbowe alimtibitishia kuwa wana kikosi imara.

Taarifa zinasema kwamba baadhi ya walinzi hao ni kutoka mgambo, Jeshi la Kujenga Taifa na askari wastaafu. Na kila mkoa wako zaidi ya 200.

Mbowe anasema, “Baada ya uchaguzi mara nyingine kumekuwa na malalamiko. Ooh mambo tumeibiwa kura. Safari hii hakuna kuibiwa kura bwana, kuibiwa kura maana yake hauko tayari kuongoza dola,” anasema.

Mbowe anasema kwamba mbali ya kujiongezea ulinzi, kadhalika wameongeza mafunzo kwa vijana wengine nchi nzima kwa lengo la ulinzi wa chama na kuwa viongozi wa baadaye.

Anasema kwamba wamewaandaa vijana hao kujenga moyo wa kujitolea, na kwamba chama hicho kilijengwa na watu wenye moyo ambao baadhi walipata madhara mbalimbali, ikiwamo kupoteza maisha.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye amedai kwamba vijana hao wa Chadema, wapo kwa ajili kuingia msituni kwa shughuli za ugaidi na kupinga matokeo ya uchaguzi.

Nape, akizungumza mara baada ya mkutano wake na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, anasema kwamba “Si ajabu ni tabia ya Chadema kuandaa vijana kupitia Red Brigade ili kuingia msituni na kuchukua madaraka ya nchi kwa mabavu.”

Nape anadai kwamba Chadema hawana ubavu wa kuchaguliwa kwa sababu Watanzania hawapendi vurugu zao zinazoweza kuendeshwa na vijana hao wa red Brigade, “Mimi huwa najiuliza, eti wanalinda kura, kura gani?”

Anadai kwamba CCM wamepata taarifa nyeti za mpango ovu unaoandaliwa na Chadema kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu kwamba kuna mpango wa kuwatumia vijana wa Red Brigade.

Licha ya kuwako kwa wagombea wengine, lakini mpinzani mkubwa wa Lowassa ni Dk. John Magufuli wa CCM. Chadema ilianza kuisumbua CCM hasa mwaka 2010 katika Uchaguzi Mkuu ambako Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilimtangaza Rais Jakaya Kikwete wa CCM kuwa mshindi dhidi ya Willibrod Slaa wa Chadema.

Rais Kikwete alipata kura milioni 5.27 ambazo ni sawa na asilimia 61.17 wakati Dk. Slaa alipata kura milioni 2.27 ambazo ni sawa na asilimia 26.34. Chadema safari hii ina Lowassa wakati CCM ina Dk. Magufuli.

Katika hatua nyingine, taarifa zinasema kwamba kwa sasa Lowassa ana amani moyoni tangu ahamie Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako aliteuliwa kuwania urais na mkutano mkuu.

Watu wa karibu wa mwanasiasa huyo mkongwe, wameliambia JAMHURI kwamba “Hali ya woga na hofu na unyonge kwa Lowassa, imeondoka. Ana amani. Anacheka, anafurahi. Simu za ajabu ajabu na vitisho, hazimgusi tena.”

Mmoja wa wasaidizi hao aliyezungumza na JAMHURI, anasema kwamba mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz alimng’ang’ania Lowassa hadi sekunde ya mwisho kabla ya kwenda Hoteli ya Bahari Beach kutangazwa mwanachama mpya wa Chadema.

“Hadi asubuhi ya Jumanne Lowassa alikuwa na Rostam ambaye wakati wote alimsihi asiondoke CCM, lakini Lowassa alijipima kwa muda mrefu, na kufanya uamuzi alioufanya. Kuondoka CCM,” anasema.

Taarifa mpya zinasema kwamba Lowassa sasa analazimika kukatisha ziara yake ya kujitambulisha na kurejea Dar es Salaam ili kujipanga kurejesha fomu kesho Jumatano Agosti 19, mwaka huu.

Lowassa alipanga kwenda Mbeya Ijumaa iliyopita na kutimiza hiyo ratiba kama alivyofanya Arusha Jumamosi iliyopita. Jumapili alipanga kwenda Mwanza kumalizia Zanzibar Agosti 17, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema mwisho wa kurejesha fomu ni kesho Agosti 19 badala ya Agosti 21, mwaka huu.

3276 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!