Na Pendo Nguka,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mwalimu Nyerere Foundation (MNF), Mzee Joseph Butiku, amezungumza na wazee leo jijini Dar es Salaam kuhusu ujenzi wa amani, umoja na haki nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mzee Butiku ameeleza kuwa msingi wa haki na umoja ni nguzo muhimu katika mfumo wa uendeshaji wa Taifa na nchi imara ni ile yenye mshikamano, umoja na amani.

Mzee Butiku amekumbusha kuwa siku chache zilizopita Taifa lilipitia changamoto kubwa iliyolisababisha kutetereka huku akieleza kuwa tangu octoba 29 kulikuwepo hali ya sintofahamu na aibu kwa Taifa.

“Kulikuwa na jambo lililotokea katikati na kusababisha kutikisika kwa misingi ya umoja ingawa kwa bahati nzuri Taifa halikuanguka ,”anasema Butiku.

Ameongeza kuwa hali hiyo haikuwa aibu ya Tanzania pekee, bali hata majirani na marafiki wa Tanzania walihuzunika, kwani hawakutarajia Taifa lifikie hali kama hiyo.

Mzee Butiku ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliamua kuunda tume maalum ili ichunguze kwa kina na kwa upana kilichotokea ili baadaye Taifa lielezwe ukweli wa mambo.

“Rais Samia anaendelea kulitazama Taifa kwa umakini, na kwamba Watanzania wameelezwa kuwa majibu ya tume yatatolewa mwezi ujao,”anasema

Katika kipindi cha mpito, hofu na sintofahamu vilianza kujitokeza, na baadhi ya mambo yaliyokuwa yakiunganisha Taifa yalianza kuogopwa, hali iliyosababisha mazungumzo kuwa marefu na magumu.

Mzee Butiku amekumbusha hotuba ya Rais Samia ya tarehe 2, huku akisema kuwa wazee walikaa na kushauriana, na hata kufikia hatua ya kuahirisha kikao chao cha Dodoma na baadaye waliamua kuendelea na mazungumzo, wakitambua umuhimu wake kwa mustakabali wa Taifa.

“Kikao cha leo kinalenga kukumbushana misingi aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yaliyotokea ni msiba wa kitaifa, na kwamba msiba huombolezwa kwa pamoja,”anasema.

Butiku ameongeza kuwa taasisi ya MNF inasimamia haki, umoja na amani, na changamoto zozote zisije zikawafanya Watanzania kupoteza misingi hiyo.

Tanzania ina sheria zinazolinda umoja na amani, na kwamba kikao hicho kinapaswa kutoa mwelekeo wa mustakabali wa Taifa. Akisema kuwa wazee wanapokutana hakuna jambo linaloharibika, huku akilitaja tukio lililotokea kuwa somo kwa wote.

Mzee Butiku ameeleza kuwa wazee hawazungumzi mambo makubwa kwa fujo, bali kwa hekima, yatakayowezesha pande zote kuelewana vizuri.

“Pamoja na kusubiri kuelezwa kilichotokea, ni muhimu kutathmini mema na mabaya yaliyojitokeza na kueleza kuwa uzalendo na haki vilitetereka katika maeneo fulani, “amesema Butiku.

Butiku ameongeza kuwa mazungumzo ya wazee yatalenga kujadili masuala mbalimbali yakiwemo maafa na uharibifu, mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uzalendo, haki na uwajibikaji, pamoja na ujenzi wa amani, utatuzi wa migogoro na maridhiano.