KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito siku ya Jumamosi wa uwepo mpango wa mara moja na wa kudumu wa kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza.

Guterres ameitoa kauli hiyo alipohutubia mkutano wa kilele wa nchi za kiarabu uliofanyika mjini Baghdad nchini Iraq, baada ya Israel kutangaza mpango mpya wa operesheni kali zaidi katika ardhi ya Palestina iliyozingirwa.

“Tunahitaji usitishaji vita wa kudumu, sasa, nimeshtushwa na mipango iliyoripotiwa na Israel ya kutanua operesheni za kijeshi za ardhini, ” aliwaambia viongozi wa nchi za Kiarabu katika mkutano huo.

Viongozi hao wa nchi za Kiarabu wametoa pia wito wa kusitishwa mara moja kwa vita katika Ukanda wa Gaza , wakiishutumu vikali Israel kutokana na operesheni zake katika ardhi ya Palestina.

Wimbi jipya la mashambulizi ya Israel limesababisha vifo vya mamia ya watu tangu kusambaratika mwezi Machi, kwa makubaliano ya usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka. Siku ya Jumamosi, mamlaka za Gaza zimesema watu 146 waliuawa huko Gaza ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.