Wajumbe kutoka mataifa mbalimbali walioshiriki mkutano wa 65 wa shirika la utalii la Umoja wa mataifa duniani (UNWTO) uliofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 5 hadi 7 Oktoba, 2022 wametembelea Hifadhi ya Ngorongoro na kufurahishwa na uwepo wa vivutio mbalimbali vya utalii.

Miongoni mwa waliotembelea Hifadhi hiyo na Naibu Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe. Louis Steven Obeegadoo ambae ameeleza kuwa wamekutana jijini arusha kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha sekta ya Utalii barani Afrika hasa baada ya athari ya Janga la UVIKO-19 na kujadili fursa za uwekezaji katika nchi ya Tanzania ambayo ni miongoni mwa Nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi duniani.

Obeegadoo ameeleza kuwa baada ya mkutano wa UNWTO yeye na wajumbe wenzake zaidi ya 200 wameamua kutembelea hifadhi ya Ngorongoro ili kushuhudia hifadhi bora yenye maajabu mengi na mazingira ya asili ambayo yametunzwa na kuhifadhiwa yakiwa na Wanyama wa kila aina wanaomfanya kila mgeni atamani kutembelea hifadhi ya Ngorongoro.

“Wajumbe wa mkutano wa UNWTO tumetembelea eneo la Kreta ya Ngorongoro, ni eneo lenye maajabu ambalo kila mtu anapaswa kuja kuliona na kujifunza mengi.

….Ni fahari kutembelea hapa kwa kuwa ni hifadhi yenye mvuto wa asili barani Afrika na duniani kote, hatuna haja ya kwenda,Ulaya, Asia na Amerika wakati tuna vivutio vizuri Afrika hasa hapa Tanzania ambako Utalii unaenda kuwa injini ya uchumi huku watu wake wakiwa wakarimu na wenye mapenzi na Nchi yao” ameongeza Mhe. Obeegadoo.

Mohamed Yahyouh kutoka nchi ya Algeria amebainisha kuwa Ngorongoro ni sehemu ya moyo wa Afrika kutokana na historia yake na juhudi za uhifadhi ambazo zimefanya Wanyama kuwa na utulivu wa akili unaowafanya watalii wawaone kwa urahisi na ukaribu ndani ya muda mfupi katika eneo moja.

“Wanaopenda kujifunza mafanikio ya uhifadhi wa wanyamapori waje Ngorongoro, ni eneo lenye mazingira mazuri yaliyotunzwa, maji ya kutosha na malisho….

Hii inatufundisha kwamba uhifadhi katika mazingira asili unafanyika Ngorongoro kwa vitendo tofauti na baadhi ya Nchi ambazo maeneo ya Hifadhi yamekuwa jangwa lenye joto kali, mimi kama mtengeneza filamu nitarudi kurekodi filamu katika eneo la Kreta ya Ngorongoro” ameongeza Mohamed.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi (Huduma za Shirika) NCAA Needpeace Wambuya amewapongeza wajumbe hao kwa kuchangua kufanya ziara katika Hifadhi ya Ngorongoro na kuwaalika kwa mara nyingine kuja na familia zao na kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Ngorongoro katika mataifa yao.