Wiki iliyopita Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA), aliwaalika viongozi wa dini kushiriki katika kikao kazi baina yao na Bunge/NACOPHA katika kuongeza jitihada za kupunguza unyanyapaa unaohusiana na virusi vyya ukimwi (VVU).

Machi Mosi kila mwaka ni maadhimisho ya siku ya kupinga unyanyapaa duniani na kwa kutambua hali ya unyanyapaa nchini, Bunge na NACOPHA wakaandaa kikao hiki, pia wanakusudia kufanya uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kupunguza unyanyapaa nchini Machi 9, mwaka huu.

Pamoja na changamoto nyingine nyingi zinazowakabili ndugu zetu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU), unyanyapaa ni changamoto kuu ambayo wao wenyewe wameielezea kuwa ni hatari zaidi ya virusi vya ukimwi na ukimwi wenyewe na wamewaomba viongozi wa dini washiriki katika kuupinga kwa lengo la kuupunguza na hatimaye kuutokomeza katika jamii yetu.

Unyanyapaa ni nini?

Kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa kuhusu kupunguza unyanyapaa na ubaguzi katika programu za virusi vya ukimwi, ukinukuu kutoka jarida la maelezo halisi ya unyanyapaa na ubaguzi lililotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi (UNAIDS), Disemba 2003, (www.unaids.org):  

“Unyanyapaa unaohusishwa na virusi vya ukimwi unaweza kuelezewa kama ni ‘mchakato wa kupunguza thamani’ ya mtu ama akiwa anaishi na virusi vya ukimwi ama anahusiana na virusi vya ukimwi na ukimwi. 

Unyanyapaa huu mara nyingi unaanzia katika misingi ya unyanyapaa kwenye ngono na utumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano – ambazo ni njia mbili kuu za kuambukiza virusi vya ukimwi.

Ubaguzi hufuatia baada ya unyanyapaa na ni kutendewa visivyo sawa na kwa isivyostahili kwa mtu kutokana na hali halisi ama ya kudhaniwa juu ya hali yake ya uambukizo wa virusi vya ukimwi. 

Ubaguzi unatokea wakati ambapo utofautishaji unafanyika dhidi ya mtu unaosababisha kutendewa visivyo sawa na isivyostahili kwa misingi ya kuwa miongoni au kuhisiwa kuwa miongoni mwa kundi fulani.”

Unyanyapaa unafananaje?

Unyanyapaa na ubaguzi (unaoelezwa kama vitendo vinavyochukuliwa na watu ama taasisi kutokana na unyanyapaa) unaweza kujitokeza katika mlolongo wa namna nyingi zikiwemo; kutengwa na kutoshirikishwa kijamii (mfano: kutengewa vyombo vya chakula, kutengwa wakati wa matukio ya kijamii) ikijumuisha kufanyiwa vurugu, maneno (mfano: kutetwa, kupachikwa majina ama kunyooshewa vidole); kupoteza utambulisho na hadhi (mfano: kupoteza heshima katika familia na jamii); na taasisi (mfano: kufukuzwa kazi, nyumba au wateja kukimbia biashara).

Unyanyapaa unaweza pia kuwepo kwa ndani na kuathiri jinsi watu wanavyofikiria juu yao wenyewe. Kwa mfano watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanaweza kujiwekea kwa ndani unyanyapaa unaowakabili na kusababisha wajionee aibu, hawana hadhi, kudhalilika ama kukosa maana. 

Hii inaweza kuwazuia kutafuta huduma za matunzo ama tiba ama kuchukua fursa za maisha kama vile kuendeleza elimu, kupanda cheo au kuanzisha biashara.

Baada ya kupata fasili ya unyanyapaa na mifano yake michache, sasa tuuangazie unyanyapaa kwa jicho la Uislamu na tuiase jamii yetu kuwa unyanyapaa ni ubaguzi dhidi ya ubinadamu na ni dhuluma na dhambi. Tuiangazie mifano michache.

Mfano mmoja wa unyanyapaa ni kutetwa, kupachikwa majina (mabaya) na kunyooshewa vidole. Uislamu unatufundisha nini juu ya yaliyotajwa?

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 49 (Surat Al-Hujuraat), aya ya 11 kuwa: “Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane heshima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwishaamini. Na wasiotubu, hao ndio wenye kudhulumu.”

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya hii anatukataza kudharauliana, kuvunjiana heshima na kuitana kwa majina ya kejeli, na haya ndiyo wanayoyalalamikia ndugu zetu wanaoishi na virusi vya ukimwi kuwa baadhi ya wanajamii wanawadharau, wanawavunjia heshima na kuwaita majina ya kejeli kama vile marehemu watarajiwa na waathirika.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA), Bi. Leticia Mourice, anasema kuwa kumwita ndugu yako anayeishi na virusi vya ukimwi jina la ‘mwathirika’ au ‘marehemu mtarajiwa’ ni unyanyapaa unaowaumiza sana.

Kwa nini umwite nduguyo ‘marehemu mtarajiwa’ wakati unajua siri ya kifo na wakati gani yeyote miongoni mwetu ataiaga dunia anayo mwenyewe Mwenyezi Mungu aliyetuumba? Wewe unayemnyanyapaa nduguyo anayeishi na virusi vya ukimwi unajua lipi litakutokea kesho? Unajua nini utapata au lipi litakupata kesho? Unajua ardhi gani utazikwa? Ikiwa haujui dharau ya nini? Kiburi cha nini? Unyanyapaa wa nini?

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 31 (Surat Luqmaan), aya ya 34 kuwa: “Hakika kuijua saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye anayeiteremsha mvua. Na anavijua vilivyomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua, mwenye habari.”

Kuna kujua kwa hakika, undani na hatima ya kitu au jambo na kuna kujua sehemu ya jambo kupitia elimu na vipawa alivyoturuzuku Mwenyezi Mungu aliyetuambia katika Qur’aan Tukufu kuwa: “Kamfundisha mtu aliyokuwa hayajui.” (Sura 96 – Surat Al-Alaq, aya ya 5).

Unadhani kuvijua vilivyomo ndani ya matumbo ya uzazi ni kujua hali ya mimba/mtoto kupitia Ultra Sound? La hasha! Kujua kwake Mwenyezi Mungu ni zaidi ya hayo, ikiwemo maisha mazima ya kiumbe huyo na hatima yake.

Ni ajabu kwa asiyejua siku ya kifo chake na wapi atazikiwa amdharau na kumbeza nduguye katika ubinadamu kwa kuwa tu anaishi na virusi vya ukimwi kwa kumwita ‘marehemu mtarajiwa.’

Mbali ya Mwenyezi Mungu kuharamisha yaliyotangulia kutajwa ambayo WAVIU yanawakabili kama sehemu ya unyanyapaa, nasaha yangu kwako ni kuwa ufahamu kuwa kuna watu wa aina mbili hapa duniani: Waliotiwa katika majaribu na wale waliosalimishwa na majaribu. Basi waonee huruma waliopatwa na majaribu na wala usifurahie majaribu yaliyowafika kwani Mwenyezi Mungu Mwema ana uwezo, akitaka, anaweza kuwaondolea majaribu waliyonayo na akakutia wewe majaribuni.

Mfano mwingine wa unyanyapaa ni kupoteza heshima na hadhi katika jamii. Unyanyapaa wa aina hii ni mbaya, kwani unamuondolea mwanadamu utukufu na heshima yake alivyopewa na Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi, aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 17 (Surat Al-Israa), aya ya 70 kuwa: “Na hakika tumewatukuza wanadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba.”

Hii ndiyo thamani, hadhi na utukufu wa mwanadamu kwa ubinadamu wake. Basi nani miongoni mwa wanadamu mwenye mamlaka ya kumdhalilisha mwanadamu na kumnyanyapaa kwa sababu tu anaishi na virusi vya ukimwi?

Nihitimishe makala hii kwa kuitaka jamii ithamini hadhi na heshima ya mwanadamu aliyopewa na Mola wetu Mlezi, kwani thamani ya mwanadamu ni kubwa, awe hai au mfu. Jamii ipinge yale yote yanayoingia katika unyanyapaa kama vile kutengwa na kutoshirikishwa kijamii kwa kutengewa vyombo vya chakula, kutetwa, kupachikwa majina ama kunyooshewa vidole, kupoteza utambulisho na hadhi, kwa kupoteza heshima katika familia na jamii.

Pia kwa namna ya kipekee, tuiombe Wizara ya Afya iondoe utaratibu wa kuwatengea sehemu maalumu za kuwapa huduma WAVIU, kwani nalo linashabihiana na ule unyanyapaa wa kutengwa na kutoshirikishwa kijamii kwa kutengewa vyombo vya chakula. 

WAVIU wachukuliwe na wahudumiwe kama wagonjwa wa kawaida badala ya kujengwa mazingira ya wao kunyooshewa vidole kuwa: “Wale pale waishio na virusi vya ukimwi!”

Unyanyapaa ni ubaguzi dhidi ya ubinadamu na Uislamu unapinga ubaguzi. Unyanyapaa ni dhuluma dhidi ya ubinadamu na Uislamu unapinga dhuluma. Unyanyapaa ni dhambi, kwani Mwenyezi Mungu ametukataza kudharauliana, kuvunjiana heshima na kuitana kwa majina ya kejeli.

Shime! Jamii ipinge unyanyaa kwa ndugu zetu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU). Unyanyapaa ni ubaguzi, ni dhuluma, ni dhambi.

Usifurahie majaribu yaliyompata nduguyo, mwanadamu mwenzako, huenda Mwenyezi Mungu, mwenye kukubali toba, akampa nafuu na faraja na kisha akakutia wewe katika mtihani ule au mwingine. Haya tukutane Jumanne ijayo!

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.

Simu: 0713603050/0754603050

555 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!