Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema tangu kuanza kwa mikutano ya kampeni za Urais kupitia CCM kwa mgombea wake Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari zaidi ya wananchi milioni 45 wameshiriki kikamilifu kwa namna mbalimbali.
Kati ya hao, milioni 14.6 wamehudhuria mikutanoni, huku milioni 31.6 wakifuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kampeni hizo za mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 5 Oktoba 2025 Jijini Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Kuu ya CCM , Kihongosi amesema kuwa uzinduzi wa kampeni hizo ulifanyika kwa kishindo tarehe 28 Agosti 2025 katika Uwanja wa Kawe, Dar es Salaam, ambapo uliweka historia kwa kuvunja rekodi ya mahudhurio na shamrashamra tangu kuasisiwa kwa chama hicho.

Akitaja takwimu za kampeni, Kihongosi amesema kuwa hadi sasa Dkt. Samia amefanya jumla ya mikutano 77 katika mikoa 21 inayounda kanda mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwemo Kanda ya Kati, Magharibi, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Pwani, Pemba na Unguja.
Amefafanua kuwa katika maeneo yote hayo, wananchi wameendelea kuonesha imani kubwa kwa Dkt. Samia kwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025–2030) pamoja na sera na ahadi zake.
Kihongosi amesema imani hiyo imetokana na uongozi wenye mafanikio makubwa uliooneshwa na Dkt. Samia katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, akibainisha kuwa mafanikio hayo ndiyo yanayowapa Watanzania matumaini makubwa ya mustakabali wa taifa lenye maendeleo, umoja na ustawi wa watu wote.

