Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amesema ushindi wa Joshua Nassari katika Jimbo la Arumeru Mashariki, ni hukumu mpya ya vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na viongozi wa Serikali.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, kuzungumza na maelfu ya wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi Leganga wakati wa kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua Nassari, Dk. Slaa alisema kitendo kilichofanywa na wananchi wa jimbo hilo, ni hukumu ya wazi kwa watu wote wenye vitendo dhalimu.

Alisema siku zote uongo hushindwa, na kwamba ufisadi katika taifa la Tanzania una ukomo wake.

“Kazi mliyoifanya hapa ni kubwa sana, kwani hata Mwanza, Songea, Kiwira katika maeneo hayo yote matatu uongo na ufisadi vilitawala, lakini vyote vimepigwa chini, naomba niwapongeze wote waliofanya uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kazi nzuri mlioifanya.

“Napenda kutoa pole kwa wale wote waliopata matatizo sehemu mbalimbali katika kipindi hiki cha kampeni za harakati za ukombozi. Daima damu ya binadamu haipotei bure kwani mbegu mlioipanda kwa damu ya wana-Arumeru ni mbegu ya ukombozi kwa taifa zima, na CCM wapate ujumbe huo,” alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa katika mkutano huo alitumia fursa hiyo kuwatangazia wananchi ahadi ya kuchimbiwa visima vya maji iliyotolewa na kada wa CCM, Mustafa Sabodo, mara baada ya kusikia ushindi mkubwa alioupata Nassari.

“Mfadhili mkubwa wa CCM amekupongeza, na anawapongeza wananchi wa Arumeru kwa uamuzi mkubwa mlioufanya, anaungana na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, katika ahadi aliyoitoa ya kumuunga mkono kuchimba visima vinne katika jimbo la Arumeru Mashariki.

“Nassari ahadi zako zinaanza sasa, Sabodo ametufadhili mengi, ametusaidia sana na amesema kazi hiyo itaanza pale atakapopatikana mkandarasi aliyepo katika aneo hili,” alisema.

Dk. Slaa alimkabidhi Nassari kwa Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, na kusema kwamba kazi waliyokabidhiwa na chama imekamilishwa kwa uadilifu. Alizipongeza timu zote zilizotoka makao makuu na sehemu mbalimbali.

Dk. Slaa hakuacha kumnyanyua John Mrema aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampeni hizo, huku akisisitiza kwamba watu wasioitakia mema waliwaambia wamwondoe Mrema kwa madai kuwa kazi hiyo hataiweza.

“Sasa naomba niutangazie ulimwengu kwamba kazi imefanyika na kazi imewezekana, Mrema na timu yako yote nawashukuru sana. Naomba sasa Mrema ukiwa Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri nakukabidhi Nassari kwa niaba ya chama, kwani kuanzia sasa yupo mikononi mwako umlee,” alisema Dk. Slaa.

MBOWE: SAFARI YA UKOMBOZI BADO NDEFU

Mbowe alisema ni vyema wanaposherehekea ushindi huo wasisahau kwamba safari yao ya ukombozi bado ni ndefu.

Mbowe aliwashukuru Watanzania wote kwa uamuzi wao wa kuwapatia sadaka za kufanyia kazi ya kampeni aliyoamini ilikuwa ni kazi takatifu.

“Tumeshindana na watu waliokuwa na hila, polisi, usalama wa taifa, waganga wa kienyeji, dola, nguvu za kienyeji, lakini hatimaye kauli ya wengi imeenda kuwa kauli ya Mungu, hongera sana wana wa Arumeru.

Alisema wiki hii Nassari atakwenda Dodoma kwa ajili ya kuapishwa bungeni na tayari kuanza kazi moja kwa moja. Katika hatua hiyo Mbowe naye alimkabidhi Nassari kwa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ili amfikishe bungeni Dodoma akiwa ameongozana na ugeni mwingine wa wananchi kutoka Arumeru Mashariki.

Alisema kazi ya kumpata Nassari ilifanyika kwa wiki tatu, huku baadhi ya wananchi wakiwa wamemfahamu Nassari katika kampeni za mwaka 2010 ikiwa ni miaka miwili tu, wakati kazi ya kujenga mageuzi ndani ya nchi ni kazi kubwa inayohitaji muda mkubwa.

“Mimi Mbowe na Ndesamburo tumefanya kazi ya kujenga mageuzi kwa miaka 20. Ndugu zangu, kazi hii ndiyo kwanza imeanza, naomba tumsaidie Nassari, tumuombee tushirikiane naye kwani bado wapo akina Nassari wengi wanaohitajika katika harakati za mapambano.

“Mapambano ya kuleta mageuzi siku zote yanahitaji kujitoa muhanga, kwani mahali popote ambako tumeshinda katika kata tatu za udiwani na ubunge wa Arumeru Mashariki, vijana wetu wamewekwa ndani, mabomu yamepigwa; Songea mabomu yamepigwa, Mbeya mabomu, Kirumba-Mwanza wabunge wamekatwa mapanga.

“Arumeru Mashariki mabomu yamepigwa, watu wamefungwa, lakini tumeshinda. Sasa hizi ni salamu kwa Jeshi la Polisi na ninaomba nipeleke salamu kwa IGP Said Mwema aliambie jeshi lake kuwa hao wanaopigwa mabomu leo, kesho watakuwa viongozi wa taifa hili.

“Tunapenda kujenga mshikamano na tusigombane wakati wa chaguzi mbalimbali kwani sote ni Watanzania. Tumepigwa sana kwenye uchaguzi huu, nawaomba wananchi wa Arumeru Mashariki na maeneo mengine msilipize kisasi, na wewe Nassari nakuomba uende ukatumike kwa wananchi wote bila kubagua.

“Kawatendee haki wananchi wote wa CCM, Chadema na wasio na chama. Nakuomba ukawe mbunge wa kitaifa,” alisema Mbowe.

MCHAKATO KATIBA MPYA

Mbowe aliwataka wananchi kutojisahau katika sherehe za kujipongeza, kwani kazi ya mchakato wa kutafuta Katiba mpya iliyopo mbele ni muhimu kwa wananchi wote bila kubagua vyama wala dini.

Alisema mchakato huo si ajenda ya Serikali. Aliwaambia wananchi kuwa baada ya Bunge la Aprili, chama hicho kitaanza kampeni ya nchi nzima kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi juu ya kutoa maoni yao katika uundwaji wa Katiba mpya.

Alisema kitendo hicho kitakuwa ni kazi kubwa ya kuliandaa taifa kwa ajili ya mabadiliko makubwa ya kiutawala na kimfumo kwa mwaka 2015, kwani kazi hiyo si nyepesi kama watu wanavyofikiria.

Aliwaomba wananchi wa Arumeru Mashariki na maeneo mengine kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao. Alisema yapo mambo mengi yatakayowafaa wananchi wote nchini, hivyo aliwaomba kila mmoja kwa wakati wake kuwa askari wa mabadiliko ndani ya nchi yake.

“Kila mmoja wenu hapa namuomba achukue dhamira kwamba mwaka 2015 anakwenda kuibadilisha nchi, kwani katika uchaguzi huo hakuna kura itakayoibwa, kura zitalindwa kama mboni ya jicho,” alisema.

Aliwarushia ‘kombora’ wananchi hao kwa kuwaambia kuwa hatakubali kuona wakimsifia wakati baadhi yao hawajajitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo mdogo.

“Tumeandikisha wapiga kura 127,000 Arumeru Mashariki, badala yake wapiga kura 60,000 pekee wamejitokeza. Tumefanya kampeni ambayo haijawahi kuonekana nchi hii, tumepita angani, ardhini, nyumba kwa nyumba, watu wamekatwa mapanga.

“Watu ambao hawakupiga kura ni wengi zaidi ya wale waliopiga kura, sasa kupitia nafasi hii naomba nizipongeze kata zilizoongoza kwa kupiga kura. Kata ya kwanza ni Seela Sing’isi… hapo wamepiga kura asilimia 59.

“Kata ya pili ni Kata ya Maji ya Chai asilimia 59, ya tatu ni Kata ya Mbughuni wamepiga kura asilimia 59, na Kata ya nne ni Pori ambako wamepiga kura asilimia 54. Wengine wote ikiwamo Usa River, ngoja niwapashe… Ndugu zangu wa Usa River mmetuangusha kidogo kwani ni watu asilimia 34 tu ndiyo waliopiga kura, nawapongeza sana waliopiga kura, lakini kwa wale ambao hawakupiga kura iwe mwisho,” alisema Mbowe.

Alisema mwaka ujao taifa litakwenda kuanza kuandikisha watu upya katika Daftari la Wapigakura, hivyo aliwaomba vijana na watu wengi kujiandaa kwa kazi hiyo ili waweze kufanya mabadiliko mwaka 2015.

NASSARI MBUNGE WA TAIFA

Katika hatua hiyo Mbowe alimsimamisha Nassari na kuwaambia wananchi kuwa atatumika kwa ajili ya taifa lote na si Arumeru Mashariki pekee.

Alisema kama ilivyo kwa wabunge wengine wa Chadema walioshiriki katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi huo mdogo, ndivyo pia Nassari atakavyoshiriki katika harakati zote za maendeleo zitakazojitokeza sehemu mbalimbali nchini.

1170 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!