Chunguza, utabaini kwamba uwepo wa makanisa haya ni kichocheo cha uwepo wa ushirikina. Sipingi uwepo wa makanisa. Hapana, ila napinga uwepo wa wachugaji ambao hawafahamu teolojia ya maandiko matakatifu. Siwezi kuchelea kuandika kwamba, baadhi ya wachungaji wengi wa makanisa hawafahamu teolojia ya maandiko matakatifu. Wengi wao ni wababaishaji. Ninawaomba wakasome. Watakuwa msaada mkubwa wa kuporomosha dhana hii ya uwepo wa uchawi/ushirikina kutoka kwenye fikra za waumini wao.

Waafrika na Watanzania wakiwemo, tunaishi ni kwa sababu tu tumepata fursa ya kuishi. Tunastahili kuishi, lakini hatustahili kuishi haya maisha tunayoishi. Tufikirie upya mfumo wa maisha tunayostahili kuishi. Mwandishi wa kitabu cha “Passages” Gail Sheely ameandika: “Kama hatubadiliki hatukui. Kama hatukui ni dhahiri hatuishi”. Tunakua kiumri lakini hatukui kifikra. Tunahitaji ukombozi wa kifikra. Ni kweli kama anavyoamini Stephen Richards kwamba: “Namna yetu ya kufikiri inatengeneza matokeo mazuri au mabaya’’. Ukosefu wa fikra sahihi na bainifu kwa maisha ya mwanadamu yeyote yule ni ugonjwa. Ni ugonjwa usioonekana kwa vipimo vya kisayansi lakini ni ugonjwa unaoua kwa haraka sana kuliko magonjwa mengine. Ni ugonjwa unaoonekana kwa vitendo na kwa uamuzi mbalimbali wa mhusika.

Utafiti uliofanywa mwaka 2010 na asasi ya Marekani inayoitwa PEW Research Centre ulibaini na kuonyesha kwamba asilimia 93 ya Watanzania wanaamini katika ushirikina. Yaani kati ya nchi 19 za Afrika ambako utafiti huo ulifanyika Tanzania ilishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Cameron yenye asilimia 78. Hii ni aibu kubwa. Watanzania watakuwa mashuhuda kwa kile kilichotokea kwa ‘Babu wa Loliondo’ mwaka 2012. Babu wa Loliondo alijizolea umaarufu wa aina yake kwa kile alichodai kwamba ameoteshwa na Mwenyezi Mungu dawa inayotibu ukimwi. Wasomi wetu waliibukia kwa Babu kupata kikombe. Viongozi wetu waliibukia kwa Babu kupata kikombe.  Wasomi na wasiosoma waliibukia kwa Babu kupata kikombe. Tunao madaktari waliosoma lakini hawakutoa tamko lolote juu ya kikombe cha Babu.  Haishangazi sana kila kona tunakopita tunakutana na vibao barabarani vya waganga wa kienyeji. Matangazo yao utaona yanasomeka hivi: “Dk. Bingwa kutoka Uswazi.” Anatoa huduma zifuatazo:-

Kumrudisha mpenzi wa zamani

Kuongeza nguvu za kiume

Kuongeza akili za darasani

Kumsahaulisha mdai wako

Kuongeza mvuto kwa warembo

Kupandishwa cheo kazini

Dhana ya uchawi inatudhalilisha sana sisi Watanzania. Ni Tanzania kiongozi akiwa anawania nafasi ya uongozi anakwenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta nyota ya mvuto. Anaona elimu aliyopata haijampa uwezo wa kujieleza na kujenga hoja na jamii ikakubaliana na hoja yake.

Tumefika mahali Watanzania wanaamini kupata utajiri mpaka kuiba au kujiunga na mtandao wa kishetani [Freemason]. Hii ni dhana kuntu inayohitaji kuondolewa kutoka kwenye bongo za Watanzania. Ni ajabu sana. Kwa uhalisia wake, Watanzania wanahitaji uponyaji wa kifikra. Tuko gizani. Tunaishi ni kwa sababu tunaishi. Watanzania tumekuwa kama mbuzi wa kiangazi. Mbuzi wa kiangazi wanazunguka kutwa nzima pasipo kuelewa wanaelekea wapi. Hatuwezi kulikomboa taifa letu pasipo tafiti za kisomi. Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kimazoea. Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kuazima. Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kuibia. Tanzania yenye watu wenye akili pevu inawezekana. Tanzania yenye uchumi wa kati, juu inawezekana. Watanzania tunahitaji ukombozi wa kifikra, tumekwama katika mengi, tumedumaa katika mengi, tumenyanyapaliwa katika mengi. Hatushituki? Hatutafakari?

Kiongozi wa dini ya Budha, Dalai Lama, anasema: “Huwezi kufanya jambo sahihi kama kichwani mwako umebeba mtazamo hasi.” Swali la changamoto, Watanzania tuna mitazamo gani kwenye vichwa vyetu? Upo usemi unaosema kwamba: “Kama haukumbuki ni wapi ulinyeshewa na mvua siku ya kwanza, huwezi pia kukumbuka ni wapi ulikaukia.”  Ninaogopa. Ninaogopa historia kutuhifadhi kwenye kumbukumbu za vitabu vya kihistoria kama taifa la watu wasiokuwa na fikra pevu na yakinifu. Ninaogopa kutafutwa na historia mbaya kaburini. Maneno ya aliyepata kuwa waziri nchini, Arcado Ntagazwa [1993], tusipoyatafakari kwa usahihi na kuyafanyia uchambuzi yakinifu yaweza kututokea. Arcado Ntagazwa alipata kusema: “Tutakapokufa vizazi vijavyo vitafukua makaburi yetu ili vione vichwa vyetu viongozi vilikuwa na ubongo wa aina gani, kwa sababu yaelekea hatufikiri sawasawa.”  Na Profesa Palamagamba Kabudi aliwahi kusema: “Ujinga wa kizazi hiki tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho. Vizazi vijavyo vyaTanzania vitakuwa na ujinga wake. Ni vema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao kuliko kulazimisha ujinga wetu uwe ujinga wao. Kwa sababu ujinga wetu ndiyo amali yetu, lakini kwa wengine si amali.”

By Jamhuri