Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma
Zoezi la uthamini maeneo yatakayopitiwa na ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa SGR kipande cha 6 kutoka Tabora hadi Kigoma linaendelea kwa kasi katika wilaya sita za mikoa hiyo.
Wilaya hizo ni Tabora Mjini, Uyui, Urambo, Kaliua, Uvinza pamoja na wilaya ya Kigoma.

Timu kutoka ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali ikiongozwa na Mthamini Kiongozi FRV James Mark Mwanakatwe ipo mkoani kigoma ikiendelea na kazi ya uhamasishaji pamoja na ukusanyaji taarifa za mali uwandani kwa wananchi ambao maeneo yao yanaguswa na mradi huo.
Akizungumza wakati wa utoaji elimu na zoezi la uthamini uwandani tarehe 27 Oktoba 2025 wilayani Kigoma
FRV Mwanakatwe ameeleza kuwa, Ofisi ya Mthamini mkuu wa Serikali imepewa jukumu na serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufanya uthamini wa fidia kwa kipande cha 2 hadi 6 ambapo kwa sasa wako kipande cha sita.
Kwa mujibu wa FRV Mwanakatwe, timu yake imeshafanya uthamini wa vipande 52 (land parcel) ikiwemo kipande cha daraja la mto Malagarasi lenye urefu km 3 ambalo liko katika hatua za mwisho za utekelezaji.

Amesema, kwa zoezi linaloendelea sasa, wanaendelea na uthamini wa kilomita 72 hususan kwenye maeneo ambayo ni vipaumbele vya mkandarasi na kuweka wazi kuwa, kazi hiyo ina takriban vipande 44.
“Kwa kazi hii ni kilomita 72 na vipande vya ardhi takriban 44 ambavyo tutavifanyia kazi na tumeanza kazi rasmi hapa” amesema.
Mthamini huyo kiongozi wa Mradi wa SGR kipande cha 6 ameeleza kuwa, wameshafanya utafiti wa viwango vya fidia pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo ili wafahamu na kuzingitia masuala yanayohusu fidia.
Aidha, amebainisha kuwa, uthamini wa fidia kwa sasa unaendelea kwa kasi na timu ya Mthamini Mkuu wa Serikali itaendelea na jukumu lake la uthamini kwa umakini na uweledi mkubwa ili kufanikisha kazi hiyo kwa wakati.
Mkazi wa Nyamoli wilayani Kigoma ambaye eneo lake linapitiwa na mradi wa SGR Bw. Petrick Mathias amesema, wameupokea mradi huo kwa furaha kubwa na kueleza kuwa, ni imani yao wanaopitiwa na mradi huo watalipwa fidia kwa viwango stahili.

“Tumeupokea mradi huu kwa mikono miwili na ni matumaini yetu malipo ya fidia yatatolewa kwa viwango stahili” amesema.
Naye Amina Ashrafu ameshukuru timu iliyotoa elimu kuhusu masuala ya uthamini wa fidia na kueleza kuwa, fidia iliyofanyika maeneo mengine ya mradi huo wa SGR yanawapa imani kuwa, nao watalipwa kwa haki na viwango stahili.




