Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetoa wito kwa wananchi kutembelea banda lao lililopo katika Viwanja vya maonesho ya Kilimo na Ufugaji (Nanenane) ili kuona fursa mbalimbali zinazopatikana katika mamlaka hiyo.

Wito huo umetolewa na Afisa Mkuza Mitaala wa VETA, Anna Nyoni kwenye maonesho hayo yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.

“VETA tumekuja Nanenane kuwaeleza wananchi fursa mbalimbali zinazopatokana VETA. Tunatoa mafunzo katika fani mbalimbali takribani 89 ambazo zimejikita katika sekta tofauti tofauti 13.

“Tuna Sekta ya Utalii, sekta ya sanaa za maonyesho na mikono, sekta ya ufundi vyuma, sekta ya ufundi umeme, sekta ya ususi na urembo, sekta ya kilimo na usindikaji wa vyakula, sekta ya uchapaji, sekta ya huduma za biashara, sekta ya ufundi magari pamoja na sekta ya uziduaji madini,” amesema.

Amefafanua kuwa wanatoa mafunzo katika kozi za muda mrefu na kozi za muda mfupi ambapo kozi za muda mfupi zinaanzia mwezi mmoja mpaka miezi sita, na kozi za muda mrefu ni kwa miaka mitatu.

“Mwanafunzi anasoma mpaka miaka mitatu ambapo kuna ngazi ya kwanza hadi ya tatu na akifika ngazi ya pili anafanya mtihani wa kitaifa tunampa cheti cha ngazi ya pili na akifika ngazi ya tatu pia anafanya mtihani wa kitaifa tunampa cheti cha ngazi ya tatu.

“Kwahiyo pamoja na kwamba tuna hizo sekta nyingi na fani nilizozitaja, pia tuna sekta ya kilimo na usindikaji wa chakula na ndo hasa ambayo tunaitangaza hapa Nanenane. Katika sekta hiyo tuna fani mbalimbali ambazo ni kilimo cha mbogamboga na matunda, fani ya uchakataji wa miti, kilimo cha mazao ya nafaka, Bioenergy na fani ya utunzaji wa mifugo,” amesema na kuongeza kuwa:

“Kwenye utunzaji wa mifugo tunasema kila kinachotoka sisi tunakitumia kwa mfano kinyesi cha Ng’ombe tunakibadilisha kinaweza kutumika kwenye kupikia na shughuli zingine mbalimbali. Hivyo hakuna tunachokitupa…pia tuna fani ya kuchakata nyama, fani ya kufuga nyuki pamoja na fani nyingi ambazo zinahusiana na masuala ya kilimo,”.

Aidha ametoa wito kwa Watanzania kuwapeleka watoto wao kusoma Veta ili wapate Ufundi wa aina mbalimbali ambao utawasaidia huku akibainisha kuwa VETA ina vyuo vinavyofanya kazi 80 na wanampango mwakani wa kuongeza vyuo vingine 65.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share