Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jumla ya viongozi 200 kutoka barani Afrika wamehitimu mafunzo ya uongozi kupitia taasisi ya kikanda ya Uongozi (Uongozi Institute).

Mafunzo hayo katika ngazi mbalimbali zimelenga kukuza uwezo wa viongozi katika maeneo ya sifa za uongozi, usimamizi wa rasilimali watu, na uongozi wa taasisi, kwa namna inayowawezesha kuendelea kujifunza bila kuathiri majukumu yao ya kila siku.

Wahitimu katika ngazi za stashahada ya uzamili ya uongozi pamoja na programu ya uongozi ngazi ya cheti mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa kwa ushirikiano na chuo kikuu cha Aalto cha mafunzo ya Utawala, kilichopo nchini Finland, pamoja na Programu ya Uongozi kwa Wanawake ambazo zinafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women) huku yote kwa pamoja yakiendelea chini ya Serikali mbili za Tanzania na Finland zinazosimama kama wadhamini wakuu.

Hafla ya mahafali kwa wahitimu hao katika fani za uongozi imefanyika leo hii Mei 16 jijini Dar es Salaam katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, wakiwemo wawakilishi kutoka katika sekta za umma pamoja na wadau katika sekta ya elimu ya juu.

Akizungumza kama mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mke wa rais wa Finland, Suzanne Innes-Stubb amesisitiza kuhusu suala la uadilifu na kuepukana kuamua mambo kutokana na hisia na mazoea kwani maamuzi hayo huweza kuleta athari kubwa kwa wanaowaongoza.

“Ukweli na maadili viwe nguzo kuu katika utekelezaji wenu wa mambo. Ni lazima viongozi waelewe kuwa maamuzi yao yanaweza kusababisha athari kubwa kwa wananchi wao.”

Waziri wa nchi, ofisi ya Rais- Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, Mheshimiwa George Simbachawene nae amewataka wahitimu hao kuyazingatia mafunzo waliyoyapata kutoka kwa wakufunzi wao.

Nao baadhi ya washirika wa maendeleo nchini wameeleza dhamira yao ya dhati katika kuunga mkono mpango wa kutengeneza viongozi bora wajao.

Mahafali hayo yanakuwa mahafali ya nane ya taasisi hiyo iliyojikita kutoa mafunzo ya uongozi tangu ilipoasisiwa rasmi mwaka 2010 ikihudumu katika bara la Afrika .