Viwanda 12 vya kubangua korosho nchini vilivyobinafsishwa na Serikali chini ya Rais Benjamin Mkapa hivi sasa vimegeuzwa maghala ya kuhifadhi mazao.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kati ya viwanda hivyo 12, vinavyofanya kazi ni viwili na baadhi ya maghala yake yanatumika kuhifadhi korosho ambapo wakulima hulipia huduma hiyo Sh 14 kwa kila kilo ya korosho inayohifadhiwa.

 

Kwa mujibu wa mtandao wa www.cashewnut-tz.org unaomilikiwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), katika msimu wa 2012/13 ghala la Newala I katika mnada wake wa Machi 30, 2012 lilikuwa na kilo 8,488,000 zilizowaingizia Sh 118,832,000.

Viwanda ambavyo havifanyi kazi ni Mtwara, Newala I, Masasi, Nachingwea, Mtama, Likombe, Lindi, Kibaha, Tanita I na Tanita II. Viwanda vya Newala II na Tunduru vinafanya kazi chini ya uwezo wake kwa kila kimoja kubangua tani 2,000 badala ya tani 10,000 za korosho.

Taarifa ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ya mwaka 2011/12, iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi, Dome Malosha kwa Kamati ya Usimamizi wa Mashirika ya Umma (POAC) inathibitisha hali hiyo.

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe anasema serikali inapaswa kutaifisha viwanda hivyo kwa kuwa hali ya wakulima wa korosho nchini iko taabani baada ya viwanda vya kubangua zao hilo kubinafsishwa.

Kabwe ameshangazwa na hali ya wakulima wa zao hilo jinsi ilivyo mbaya kutokana na viwanda hivyo kutofanya kazi.

“Kwa kuwa viwanda vyote vimeshindwa kazi wanaovimiliki sasa hivi wanyang’anywe kwa sababu hali za wakulima wa korosho ni mbaya na hazionyeshi matumaini,” anasema Zitto.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahmani Kinana akiwahutubia wanachama wa Tawi la CCM Novemba 20, 2012 katika Kijiji cha Mkunwa, wilayani ya Mtwara, alisema viwanda ndiyo dawa pekee ya kuhuisha soko la korosho.

“Tumeuza korosho, lakini ni muda mrefu hatujapata awamu ya pili ya fedha zetu, tunaomba chama kitusaidie,” alisema Hadija Hassan, mkulima wa korosho wa kijiji cha Mkunwa.

Kinana anasema, “Wamenunua viwanda vyetu, lakini wameshindwa kuviendeleza, ajira zimepotea, wananchi wa Mtwara wanaendelea kuwa maskini.”

 

Wakati viwanda hivyo vikifanya kazi kila kimoja kiliajiri watu wengi, lakini sasa hivi vijana wanakosa kazi kwa sababu vimefungwa.

“Ama viwanda hivyo vianze kufanya kazi, au virudishwe serikalini. Nikimaliza ziara hii nitaandika ripoti kupeleka katika Halmashauri Kuu ya Taifa – NEC (ya CCM), kueleza msimamo wetu na nitasimamia hilo,” anasema Kinana.

Maghala ya viwanda hivyo hivi sasa yanahifadhi korosho ambazo hazijabanguliwa zikisubiri kusafirishwa kwenda nchi za China na India.

Kauli zenye matumaini bila vitendo kutoka kwa viongozi wa serikali na chama tawala kuhakikisha zao la korosho linapata ufumbuzi wa bei nzuri katika soko liwe mkombozi wa wakulima ni chanzo cha kuyumba kwa zao hilo.

Licha ya viongozi wa serikali na chama tawala kubaini vyanzo mbalimbali vinavyosababisha kuyumba kwa soko na bei ya zao hilo bado wamekuwa wakitoa ahadi za kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo bila ya utekelezaji wowote na kusababisha kufifia kwa maendeleo ya zao hilo na wakulima husika.

Uchunguzi umebaini pia kuwa tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani katika zao la korosho mwaka 2007/8 kumekuwapo na mafanikio na changamoto za soko la zao hilo.

Mafanikio hayo ni pamoja na wakulima kupata uhakika wa soko na kupanda kwa bei kutoka SH 300 mwaka 2006 hadi Sh 1,200 mwaka 2012/13. Hata hivyo, kumekuwapo na kuyumba kwa soko la zao hilo na kukatisha tamaa kwa wakulima na wakati mwingine kusababisha vurugu.

Mkulima wa korosho wa kijiji cha Mikangaula, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Jabil Suleiman anasema inashangaza kuona serikali ikichelea kuwekeza kwenye viwanda vya kubangua korosho licha ya kujua kuwa viwanda hivyo ndiyo mwarobaini wa matatizo ya wakulima wa zao hilo.

“Viongozi wa serikali wanatwambia matatizo ya zao la korosho yataisha pale tutakapoanza kubangua na kuachana na mfumo wa kuuza korosho ghafi nje, tangu wabaini mbona hakuna utekelezaji?” anahoji Suleiman.

Anaongeza, “Unajua tatizo la viongozi wetu kila kitu siasa, hawa ni sawa na daktari anayetamba kugundua dawa ya maradhi fulani lakini anapoletwa mgonjwa badala ya kumtibu yeye anapita akijigamba tu bila kutibu, tuwaeleweje?”

Rashid Nammole ni mkulima wa korosho wa kijiji cha Mwena wilayani Masasi. Anasema wakulima wa zao hilo wamechoshwa na kauli ambazo zinatia matumaini lakini hazina utekelezaji na kwamba suala la kilimo lisigeuzwe kuwa mtaji wa kisiasa.

“Alikuja Kinana Mtwara, wakulima wakamweleza kilio chao, akasema viwanda vitataifishwa ili vifanye kazi, hadi leo hakuna utekelezaji, hata kiwanda kimoja hakijajengwa, hizo ni siasa katikati ya umaskini. Watueleze nini kinafanyika ili kupunguza pengo baina ya kauli na matendo,” anasema Nammole.

Profesa Do DucDinh wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi ya Vietnam, amesema katika mkutano wa 17 wa mwaka 2012  kuwa ufufuaji wa viwanda vya kubangua korosho hakutawanufaisha wakulima wa zao hilo pekee bali jamii nzima.

 

Akizungumza katika mkutano wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umaskini Tanzania (Repoa), Profesa huyo amesema wakulima watafaidika kwa kupata bei nzuri na ya uhakika pia taifa litaweza kusonga mbele kiuchumi.

“Vietnam hatulimi korosho, lakini tuna viwanda vingi vya kubangua zao hilo, tunategemea malighafi kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania,” anasema Profesa DucDinh.

Profesa huyo anawashauri viongozi kufanya uchambuzi wa kina kuhusu kubinafsisha viwanda vya kubangua zao hilo.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala, Yusuf Nannila anakiri kuwa kukosekana kwa viwanda vya kubangua korosho husababisha kuyumba kwa soko la zao hilo.

“Ni kweli soko linayumba kwa sababu korosho zote tunauza ghafi, sisi kama Tanecu tumeliona hilo na kwa sasa tumeanza utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho wilayani Tandahimba. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kubangua tani 30,000 kwa siku,” anasema Nanila.

Anaongeza, “Tayari ujenzi wa ghala lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 12,000 linajengwa, ifikapo Novemba mwaka huu ujenzi wa kiwanda utaanza, tumepata mkopo kutoka Tanzania Investment Bank. Lengo ni kuwezesha wakulima kuwa na soko la ndani la korosho ghafi.”

Anafafanua kuwa licha ya kiwanda hicho kutoa ajira pia kitafungua soko kwa korosho zilizobanguliwa kutoka kwa wakulima na hivyo kuongeza hamasa ya wakulima kuuza korosho zilizobanguliwa.

“Vyama vya msingi vitanunua korosho ambazo zimebanguliwa kwa kuondolewa maganda ya nje tu, wao watatuletea sisi. Hivyo, ubanguaji wa korosho utakuwa umeenea mkoa mzima, tutasafirisha korosho ghafi lakini kwa kiwango kidogo,” anasema.

Mkurugenzi mpya wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Mkanachapa, anasema utekelezaji wa mpango wa kubangua korosho nchini unatekelezwa kwa kuhamasisha ubanguaji mdogo mdogo pamoja na wawekezaji wakubwa.

“Suala la viwanda vilivyobinafsishwa tuliachie serikali italiangalia, sisi tunaangalia namna ya kutekeleza maazimio mbalimbali likiwemo hilo la kubangua korosho.

“Tuitisha kikao hivi karibuni kutathimini zao la korosho na njia bora ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya soko yanayojitokeza, baadaye utekelezaji utaanza,” anasisitiza Mchapakazi.

 

By Jamhuri