Kuna watu huwa wanafikiria wenzao walio ughaibuni – Ulaya, Marekani au hata Mashariki ya Kati – ni wachawi. Halafu kuna wengine walikuwa wakisema kuwa labda waliotoka Tanzania na sehemu nyingine za Afrika kwenda huko na kupata maendeleo, walibebwa au ni kubarikiwa tu.

Sawa, kubarikiwa kupo lakini hata Mungu alimwambia mwanadamu ajenge nyumba imara, aweke mlango na usiku au wakati hayupo aufunge ndipo naye ataweka mkono wake kumsaidia.

Kwa hiyo dhana iliyozoeleka kwamba watu wanabebwa au wanaelea tu kwa nguvu ya wakubwa si sahihi, na utashangaa msomaji wangu kuona wapo wanaojitesa mno hadi wakafanikiwa.

Njia mojawapo ya kufikia hatua hiyo ni kujijengea mazoea ya kutafuta, kupekua na kusoma kwa bidii badala ya kuketi na kufikiria mtu mwingine atakuletea ngekewa hiyo. Kuna watu walikuja Ulaya kwa miezi michache ya kozi fupi, na baada ya kufika hawakulala ‘hadi kikaeleweka’.

Waliangalia taratibu zinataka nini, wakafungua mitandao na kutazama fursa zilizopo kama masomo au nafasi za kazi na kuanza kuomba. Hadi sasa wapo wanaoendelea kila siku kufungua macho na masikio kuhusu nafasi na zinapojitokeza wanaharakisha kuziomba wakati wakiendelea na kazi.

Lakini kwa hili naomba niwe wazi. Kinachosaidia zaidi wengi kupata nafasi hizo ni kasi ya maendeleo pamoja na kuweza kurambaza haraka mtandao, lakini na wenyewe wanavyojitahidi kukimbia na kasi yake hiyo.

Kwa mfano, wakishahitimu kozi walizokuja kusomea, baadhi wana nafasi za kuongeza tena nyingine, na wengine kuomba muda wa ziada wa kukaa ughaibuni na pia kufanya kazi.

Lakini yote hayo yanatakiwa pia utonyaji, vifungua macho au watu wa nchi au eneo moja waliotangulia kutoa ushirikiano, kwa sababu hata kompyuta na mtandao vikiwa vizuri na kasi ya namna gani, mtu hawezi kurambaza tu bila dira.

Kuna watu wenye roho zao nzuri walioingia Ulaya na kuwaita wenzao kutoka nyumbani, ili watafute maendeleo na kuyapeleka kwao. Lakini wapo wale wanaofikiria wanaweza wao wenyewe kumiliki kila kitu.

Kwa mfano ni upenyo unaotolewa kwa watu wetu baada ya kusoma kozi mbalimbali. Hakuna mtu atakayekuandikia ubaoni au kukuimbia isipokuwa ndugu au rafiki yako anayejua. Kwa hiyo, wale waliotangulia ndiyo wanaotarajiwa kuwasaidia waliopo na wanaoendelea kuingia kwa kuwapa ramani halisi ikoje.

Nafasi nyingi sana za kazi baada ya watu kupata digrii zao za pili hapa Uingereza, zimepotea bure kwa muda mrefu sasa. Baada ya watu kujibana kusoma na kufanya kazi kidogo au ndogo ndogo wakati wa kozi zao, walikuwa na haki ya kupata mwaka au hata zaidi ya kuchapa kazi tu kwa saa nyingi kadiri wanavyopenda na kujikusanyia ‘mapaundi’ kabla ya kurudi nyumbani.

Lakini wapo baadhi ya watu wasiopenda ushirikiano na watu wao kutoka nyumbani. Licha ya kujua kuwa Serikali ya Uingereza ilitoa nafasi hizo kwa yeyote anayehitimu, wao walizichukua bila kuwaambia wenzao wanapokuja. Kama kuna madoa ya ushirikiano hapa, hili ni mojawapo na linatakiwa kurekebishwa haraka.

Wenzetu wa Nigeria, Ghana na Afrika Magharibi kwa ujumla na hata Wafilipino, wamejijengea wavu mzuri wa ushirikiano na wana mtandao mkubwa. Wanasaidiana na kuhabarishana juu ya kila kinachoendelea tofauti na wabongo.

Niliona na kucheka kwa uchungu siku jamaa mmoja kutoka Tanzania alipojidai si ‘wa kwetu’, alipokataa salamu ya Kiswahili baada ya mwingine kuambiwa na jamaa fulani kwamba huyo ni Mbongo.

Akishauchuna kinamna hiyo akifika vijiweni anaungana na wenzake wa aina hiyo kwenye stori za jinsi alivyomwepuka ‘wakuja’, na baadaye wanakuja kumcheka alipomaliza miezi au miaka michache na kurudi Bongo mikono mitupu.

Jambo hili linatakiwa lifanyiwe mabadiliko makubwa na walio nchini Uingereza au na hata walio nyumbani, kwa kuwafunda kimtandao. Ungependa tujiulize! Lakini je, nani wa kumfunga paka kengele?

By Jamhuri