Na Is-Haka Omar,JamhuriMedia,Pemba

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dk.Abdulla Juma Mabodi, amewataka Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kutekeleza kwa wakati ahadi walizotoa kwa wananchi katika kampeni za uchaguzi uliopita.

Wito huo ameutoa katika ziara yake ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika hafla ya kukabidhi gari ya kubeba wagonjwa (Ambulance) ya Jimbo la Kojani Pemba.

Amesema viongozi hao wanatakiwa kupeleka maendeleo majimbo mwao ambapo ndipo walipo wananchi waliowapa ridhaa ya kuwa viongozi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, akizungumza na wananchi wa shehia ya Chwale Jimbo la Kojani Pemba katika ziara yake ya kikazi.

Dk.Mabodi, amesema kwamba wakati wa kufanya kazi za kuwatumikia wananchi ni sasa kabla ya kufika kipindi cha uchaguzi.

Aliweka wazi kuwa kwa upande wa CCM inaendelea kutathimini na kufuatilia utendaji wa kila kiongozi kwa kila jimbo.

“Endeleeni kufanya kazi za kuwatumikia wananchi tendeni haki ya kupeleka mrejesho wa maendeleo kwao ili nao wawe na imani ya kuwachagua tena katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.” amesema Dk.Mabodi.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo alisema wananchi nao wanatathimi utendaji wa viongozi wao hivyo kiongozi asiyetaka kufanya kazi asipochaguliwa na wapiga kura wake asije kulalamika.

Pamoja na hayo Dk.Mabodi amempongeza Mbunge wa Jimbo hilo kwa kutoa kipaumbele juu ya masuala ya afya za wananchi hasa kuwanunulia gari la kisasa la wagonjwa.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo Hamad Hassan Chande, amesema kuwa ataendelea kuwapelekea huduma muhimu za maendeleo ili kumaliza changamoto.

Amesema gari hilo la wagonjwa limegharimu kiasi cha shilingi milioni 138 ambalo limetengenezwa kwa mfumo wa kisasa wenye vifaa tiba vya dharura vinavyoweza kutoa matibabu kwa mgonjwa kabla ya kufikishwa katika hospitali.

“Gari hili litawasaidia wananchi wote hasa akina mama wenye ujauzito kupelekwa hospitali kwa wakati ili wajifungue salama” amefafanua Chande.

Aliyekuwa Mwenyekiti akina mama wa ACT-Wazalendo Jimbo la Kojani Pemba, akizungumza mara baada ya kujiunga na CCM katika ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi.

Pamoja na hayo amesema anaendelea na mipango ya kukamilisha miradi mbalimbali katika sekta za afya,uvuvi,maji safi na salama,kilimo,elimu,ujasiriamali na utalii ili kila mwananchi anufaike.

Mapema kupitia hafla hiyo jumla ya wanachama wapya 29 kutoka ACT-Wazalendo wamejiunga na CCM akiwemo kigogoro wa Chama hicho aliyekuwa Mwenyekiti wa akina mama jimbo la Kojani Khadija Mohamad Said.

Akizungumza baada ya kula kiapo cha uaminifu cha uanachama wa CCM, Khadija amesema yeye pamoja na wenzake wamejiunga na CCM kutokana na kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa na Chama Cha Mapinduzi Jimboni humo.

Ameeleza kwamba kwa miaka mingi wananchi hao wameishi katika mateso na dhiki kubwa kutokana na kuongozwa na viongozi wabinafsi waliojali maslahi yao badala ya wananchi.

“Tunaomba mtupokee na kutuamini kwani tumefanya maamuzi sahihi ya kujiunga na CCM na tupo tayari kushirikiana nanyi katika masuala mbalimbali ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi na Serikali kwa ujumla.”, alisema Khadija.

Pamoja na hayo amesema sababu nyingine ya kuhama ACT-Wazalendo ni kutokana na kukandamizwa na kudharauriwa kwa kundi la wanawake ndani ya chama hicho

By Jamhuri