Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Wabunge leo Juni 3, 2025 wamepitisha bajeti ya Wizara ya Afya yenye makadirio ya Sh 1,618,191,235,000.00, ili kuweza kutekeleza malengo na vipaumbele iliyojiwekea kwa mwaka 2025/26.

Jana Waziri wa Afya Jenista Mhagama, aliwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2025/2026, ikiwa na vipaumbele 10.

Baadhi ya vipaumbele hivyo ni kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza yakiwemo magonjwa milipuko, magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, magonjwa yasiyoambukiza na huduma za Lishe.

Wakati huo huo, Waziri Mhagama amesema wizara yake itapambana kuhakikisha mifumo ya vipimo vinavyofanywa kwa wagonjwa visomane katika hospitali zote nchini.

Akifanya majumuisho kwenye hoja mbalimbali za wabunge waliochangia hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2025/2026, Waziri Mhagama amesema tayari wameanza na baadhi ya hospitali za Rufani za Mikoa na za Kanda na sasa wanaelekeza nguvu kwenye hospitali nyingine za chini.
Amesema haiwezekani mgonjwa anatoka Songea amepimwa, lakini akifika Njombe atatakiwa kupimwa upya kipimo kilekile na wakati mwingine kumuongezea gharama mgonjwa.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika ngazi zote kuanzia Zahanati hadi Taifa; Kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.