Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi lilitangaza kumtia mbaroni mtu anayedaiwa kuwa kinara wa kusambaza ujumbe wa kuchochea chuki na uhasama hapa nchini, kupitia simu za kiganjani.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, kwa vyombo vya habari, inasema mtuhumiwa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, alikutwa akiwa na kadi (sim cards) 13 za simu za mkononi.

 

Inaelezwa kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akisambaza ujumbe wa kuchochea chuki baina ya wananchi na viongozi wa Serikali, pamoja na kuwatusi viongozi kwa lengo la kuzusha machafuko nchini.

 

Sisi tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo, ingawa limechelewa kuanza kushughulikia tatizo hilo ambalo ni kikwazo kikuu cha amani inayoitangaza nchi yetu kuwa ni kisiwa cha amani duniani.

 

Vitendo vya kusambaza ujumbe mfupi wa maneno (sms) siku hizi si kitu kigeni hapa nchini, na huenda karibu kila Mtanzania mwenye simu ya mkononi amekwishatumiwa ujumbe wa uchochezi akitakiwa kusaidia kuusambaza kwa watu wengine.

 

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikitekelezwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati, waliolewa amani na wasioitakia mema nchi yetu ya Tanzania.

 

Umefika wakati vyombo vya ulinzi na usalama nchini kutosita kufanya uamuzi mgumu, kwa kuwashughulikia bila huruma watu wote wenye dhamira mbaya ya kuvuruga amani iliyotafutwa kwa jasho jingi na waasisi wa Taifa letu akiwamo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 

Mtuhumiwa aliyekamatwa abanwe na vyombo vya ulinzi na usalama awataje washirika wake na wafadhili wa uovu huo, ili wote wachukuliwe hatua kali za kisheria kunusuru amani ya nchi yetu.

 

Watanzania wengi tuna imani na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, pamoja na mahakama zetu, hivyo hatutarajii kuona na kusikia kesi ya mtuhumiwa huyo inagubikwa na mizengwe itakayoishia kumwachia huru.

 

Sisi JAMHURI tunaamini kuwa adhabu kali dhidi ya watu wanaojaribu kuwafarakanisha Watanzania na kuitumbukiza nchi katika machafuko yasiyo ya lazima, zitatoa onyo na fundisho kwa wengine wanaojiandaa kujihusisha na uovu huo. Mungu ibariki Tanzania, idumu katika amani.

 

Please follow and like us:
Pin Share