Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

WADAU wa mazingira nchini wako tayari kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050 katika eneo la Uchumi wa Buluu kwa kuwajengea uwezo wananchi kufanya shughuli endelevu na rafiki kwa bahari.

Katika kufanikisha hilo wadau hao kupitia Shirika la Kimataifa la Uhufadhi Uhifadhi wa Mazingira, na Uasilia (IUCN) kwa kushirikiana na wananchi imefanya urejeshaji wa mikoko kwenye pwani ya Tanga na Pemba.

Hadi sasa kiasi cha Hekta 90.6 zimefanyiwa urejeshwaji katika uoto wa asili baada ya wananchi kupata elimu ya utunzaji wa mazingira.

Meneja wa Miradi ya Uhifadhi Bahari kutoka
IUCN, Joseph Olila, alisema kupitia mradi huo tayari hekta 90.6 zimerejeshwa.

” Kuna maeneo wananchi wamepata elimu ya masuala ya uhifadhi wa mazingira ya Bahari na kurejeshwa uoto wa asili wa miti ya mikoko ndani ya miaka mitatu na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu matarajio yetu ni kufikia hekta 100″ alisema.

Akizungumza na waandishi Habari za Mazingira walio chini ya mwamvuli wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (JET) katika semina ya siku nne iliyoandaliwa na IUCN kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland alisema wamekuwa wakitekeleza mradi wa Bahari Mali kwa kipindi cha miaka mitatu.

Meneja huyo alisema lengo la mradi huo ni kusaidia shughuli za uchumi wa buluu ambao unatekelezwa katika eneo la Tanga kwa Wilaya ya Mkinga, Pangani na Pemba kwa wilaya mbili za Mkoani na Micheweni.

“ Ndani ya hizi wilaya tunatekeleza shughuli mbalimbali ambazo zimejikita katika kutatua changamoto zilizopo katika uchumi wa buluu kwa kuangalia masuala ya uzalishaji unaofanywa na vikundi vya kijamii kwa mazao ya bahari kama mwani, majongoo bahari, kaa na ufugaji wa samaki,” alisema.

Alisema mradi huo utawawezesha wananchi kujikwamua na umaskini na kufanya shughuli zao ambazo ni endelevu na rafiki kwa mazingira.

Aliongeza kuwa wamekuwa wakiangalia masuala ya uhifadhi na urejeshwaji wa bainuwai kwa kushirikiana na vikundi vya kijamii kwa kufanya urejeshwaji wa ‘species’ mbalimbali za mikoko.

Amesema amekuwa wakifanya tafiti kwa kushirikiana na wadau wengine na wamefanikiwa kuangalia eneo la asidi bahari hivyo mradi huo utawasaidia wananchi kutambua fursa zitokanazo na bahari.

“Mpaka sasa tumewafikia wananchi zaidi 400 ambao wamefanikiwa kupitia mradi huu ambao umeleta mabadiliko ya kipato chao.

“Kwa sasa tunafuatilia hali ilivyo ya utekelezwaji kwa maeneo yaliyorejeshwa uoto huo na matarajio ifikapo mwishoni mwa mwaka huu muda ambao mradi utakuwa unafikia mwisho tuwe tumefikia zaidi ya hekta 100,” alisema.

Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi kutoka Asasi ya Utafiti Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Rushingisha George alisema wakiwa wanafanya tafiti wanatarajia matokeo ambayo yatatumika kuboresha shughuli zote za uhifadhi.

“Ili kupata matokeo chanya tumeona ni vyema kuwashirikisha wanahabari ili kufikisha taarifa hizi kwa wananchi kwa usahihi kwa sababu tafiti zetu zinatija kwa uhifadhi wa bahari,” alisema.

Alisema kwa sasa bahari inaathiriwa na ongezeko la asidibahari hivyo kuna mbinu za kukabiliana nazo kwa kupata taarifa sahihi, kufanya tafiti kuangalia athari za tatizo, kutoa elimu na kutekeleza mikakati inayoweza kupunguza athari kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alisema JET imedhamiria kuwa mdau muhomu katika kufanikisha mafanikio ya uchumi wa Buluu.

“Sasa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imetoka na kuhimiza masuala ya uchumi wa buluu hivyo tumeona ni fursa kwa waandishi wa habari za mazingira kujifunza na kuujua uchumi wa buluu na namna watakavyoshiriki kuutangaza,” alisema.