Na Suzy Butondo, JamhuriMedia, Shinyanga

Wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka mkoani Shinyanga kutoka wagonjwa watano na kufikia 18 baada ya wataalamu kufanya vipimo vya kuthibitisha kwa wagonjwa wa kuhara na kutapika 41 mkoani hapa.

Hayo ameyasema leo Januari 9, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema baada ya watu 41 waliokuwa wakiugua ugonjwa wa kuhara na kutapika kufanyiwa vipimo waliogundulika na ugonjwa wa kipindupindu ni 18, na wagonjwa 30 waliruhusiwa.

Mndeme amesema waliogundulika kuwa 15 wanatoka Manispaa ya Kahama, 15, Kishapu mmoja na wawili Manispaa ya Shinyanga ambapo 13 walitibiwa na kuruhusiwa mpaka sasa walioko hospitali ni wagonjwa watano wanaendelea na matibabu .

“Licha ya kugundulika ugonjwa wa kipindupindu hakuna vifo lakini wale watano wanaendelea kupata matibabu,”amesema Mndeme.

“Mnamo Desemba 28, 203 mkoa wetu katika Kata ya Kagongwa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama vilitokea vifo vitano ambavyo vilisababishwa na kuhara na kutapika, hali iliyopelekea mkoa kufanya ufuatiliaji katika eneo la Kagongwa Manispaa ya Shinyanga,”amesema Mndeme.

Amesema baada ya kutokea ugonjwa wa kuhara mkoa umeunda timu ndogo ya watalaamu ya kuratibu na kufuatilia mwenendo wa ugonjwa huo ambayo tayari imeanza kazi, na kila halmashauri zimeundwa timu kwa ajili ya kusimamia kikamilifu ili kuzuia kusambaa na kuenea kwa ugonjwa huu hatari.

“Mpaka sasa tuna kambi tatu za kufanya matibabu ya ugonjwa huo ambazo ni Kituo cha afya Ihapa katika Manispaa ya Shinyanga, Kituo cha afya Kagongwa Manispaa ya Kahama kituo cha afya Kishapu halmashauri ya Kishapu ,”amesema Mndeme.

“Na ugonjwa huu wa kuhara na kutapika husababishwa na watu kula kinyesi kibichi kupitia vyakula au vinywaji na huenezwa kwa haraka na kuweza kusambaa kwa muda mfupi zaidi, na dalili za ugonjwa huu ni kuharisha mfululizo na mgonjwa kuishiwa maji mwilini, hivyo ni vizuri wananchi kujikinga kwa kuchemsha maji ya kunywa, kuosha matunda kwa maji tiririka, kula chakula cha moto,”ameongeza Mndeme.

Pia Mndeme amewataka wananchi ili kuepukana na ugonjwa watumie maji yaliyotiwa dawa ya Aqwa tabs na watumie vyoo bora, na mkoa umejipanga kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa ajili ya kutolea huduma kwa wananchi.

“Pia tunaendelea kutoa elimu juu ya namna nzuri ya kujikinga na magonjwa ya milipuko ikiwemo kuhara na kutapika, kwa kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kutembelea kaya na kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa hayo, kufanya vipimo vya maji katika visima mbalimbali katika halmashauri zilizoadhirika na ugonjwa wa kuhara na kutapika na kuwasafirisha wagonjwa kutoka maeneo yao ya awali kwenda katika vituo vya matibabu”amesema Mndeme.