Wajua mgawanyo wa mali ndoa ya mke zaidi ya mmoja inapovunjika?

Kipindi fulani huko nyuma wakati nikieleza masuala ya sheria za ndoa, nilipata kuzungumzia utaratibu wa mgawanyo wa mali iwapo ndoa inavunjika. Kimsingi nilieleza mgawanyo wa mali katika msingi wa uwepo wa ndoa ya mke mmoja.
Sikuwahi kueleza mgawanyo wa mali iwapo ndoa ni ya mke zaidi ya mmoja. Wengi waliuliza swali hili ambapo baadhi niliwajibu na baadhi sikuwajibu. Leo sasa nitaeleza mgawanyo wa mali katika ndoa ya mke zaidi ya mmoja pale mmoja wa wake anatalakiwa.
Ndoa ya mke zaidi ya mmoja


Kwa jina la kitaalamu ndoa za namna hii huitwa ndoa za mitala. Wanawake wanaoolewa huwa zaidi ya mmoja. Inawezekana wakawa wawili, watatu, wanne, watano au zaidi – neno mitala hubaki kuwa mitala.
Sheria yetu ya ndoa inatambua ndoa ya mke zaidi ya mmoja na hivyo kwa waliofanya hivyo hawajatenda dhambi yoyote kisheria. Ndoa za namna hii mara nyingi zimekuwa zikifungwa na Waislamu au watu ambao huishi maisha ya kufuata mila, ambao wengi wao wako vijijini.


Hata hivyo, tumeshuhudia mazingira ya ndoa za namna hii kwa watu ambao ni wa makundi tofauti na niliyotaja kwa siku za hivi karibuni. Yote kwa yote hizo  ndiyo  ndoa za mitala.

Sheria inasemaje?
Kifungu cha 57 cha Sheria ya Ndoa kinaweka wazi kwa kusema kuwa katika sheria yoyote ile, mwanaume anapokuwa na wanawake wawili au zaidi, wanawake hao wanatakiwa wawe na haki sawa mbele ya macho ya sheria na si vinginevyo.
Kawaida tumezoea kuna u-bi mkubwa na u-bi mdogo. Basi ieleweke kuwa hayo ni mambo ya kwetu, lakini sheria haina u-bi mkubwa wala u-bi mdogo. Sheria inajua mke ni mke awe alianza kuolewa au ameolewa mwishoni. Wake wote wana haki sawa mbele ya mume wao na mbele ya sheria na huo ndiyo msimamo wa sheria.
Mgawanyo wa mali ukoje?


Katika hili msimamo wa sheria ni kuwa japo wanawake ni wengi na mtu aliyewaoa ni mmoja, bado kila mwanamke ana mgawo wake ambao uko tofauti na  mwingine  iwapo ndoa ikivunjika.
Hapo juu tumeona sheria ikisema wanawake walioolewa na mume mmoja wana haki sawa. Ni kweli wana haki sawa, lakini ili haki sawa ipatikane ni lazima baadhi ya mambo ya msingi yazingatiwe.
Ili mke fulani amzidi mwingine katika mgawo wa mali ndoa inapovunjika, kitu kikubwa kinachozingatiwa ni mchango wake  katika upatikanaji wa mali zilizopo.


Ikiwa mchango wa mwanamke fulani ni mkubwa basi atachukua kikubwa na ikiwa mchango wake ni mdogo basi atachukua kidogo. Kubwa zaidi ni kuwa kila mwanamke atachukua kile kinacholingana na mchango wake katika upatikanaji wa mali husika.
 Katika  mgawanyo wa mali za ndoa, sheria haikuweka  msimamo wa kiasilimia kama ilivyo katika mambo mengine  ya mirathi n.k. Katika  hili  sheria humtaka kila  mhusika kuthibitisha amechangia nini ili apate haki yake  kutokana na mchango huo.

Bi mdogo anavuna mali nyingi kuliko bi mkubwa
Kwa msimamo wa nilichoeleza hapo juu, basi yawezekana bi mdogo akapata mali nyingi kuliko bi mkubwa iwapo ndoa yake itavunjika. Yawezekana bi mdogo ameolewa miaka miwili tu lakini lakini fedha yote ya kujengea nyumba za familia imetoka kwake, au nusu yote imetoka kwake, au kiasi cha pesa kilichosababisha upatikanaji wa viwanja na magari n.k. kilitoka kwake.


Na ikawa bi mkubwa pamoja na kukaa kwenye ndoa zaidi ya miaka thelathini lakini mchango wake ni mdogo au ni wa kawaida ambapo hakuwahi kuchangia chochote zaidi ya mchango wake wa kazi za nyumbani.
Kimsingi, mchango wa kazi za nyumbani ni mchango na unatambulika isipokuwa kwa mazingira niliyoeleza hapa mchango huo hauwezi kustahili mgawo sawa na wa bi mdogo aliyetoa pesa yote au nusu mpaka mali hizo zikapatikana.


Nimalizie kwa kukumbusha kuwa kitu kikubwa kinachozingatiwa katika kugawana mali iwapo ndoa ya mke zaidi ya mmoja imevunjika, ni kuangalia mchango wa kila moja au mchango wa anayeondoka katika juhudi za upatikanaji wa zile mali. Kila mtu atachukua kulingana na mchango wake baada ya kuuthibitisha.
Kwa ushauri zaidi wa masuala ya sheria hususani za ardhi, ndoa, mirathi, kampuni na kadhalika. Tembelea: sheriayakub. blogspot.com