DAR ES SALAAM

NA AZIZA NANGWA

Wakala wa Vipimo nchini (WMA) umefanikiwa kusambaza huduma zake kwa watu wengi nchini na kuwa karibu zaidi
ya sekta binafsi.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni na Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Dk. Ludovick Manege,
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ambayo wakala umeyapata katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Dk. Manege anasema WMA umefanikiwa kuongeza vipimo mbalimbali vilivyokaguliwa kutoka 660,000 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi vipimo 760,000 kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Ofisa Mtendaji Mkuu huyo wa WMA amebainisha pia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeisaidia taasisi hiyo kwa kuiwezesha kuboresha vipimo katika sekta mbalimbali.
Dk. Manege anasema kwa kutambua umuhimu wa vipimo, hasa katika sekta ya madini, serikali iliipatia WMA kiasi cha
Sh milioni 500 kwa ajili ya kununulia vigezi vya kisasa gredi ya pili vinavyotumika kuhakiki mizani inayotumika kuuza na kununua madini katika mikoa mbalimbali.
Anasema kutokana na jitihada hizo na maboresho, kwa mwaka huu taasisi hiyo imetoa gawiwo la serikali kiasi cha
Sh milioni 12.538 kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali. Anaongeza kuwa wamefanikiwa kununua water meter test bench inayowezesha mikoa yote kutengeneza vifaa vingine vya kuhakiki dira za maji, ambapo kwa sasa zoezi la upimaji wa dira za maji linafanyika mikoani ili kuhakikisha mamlaka za maji zinafunga dira zilizo sahihi kwa wateja wao.
“Mpaka hivi sasa tumeweza kuhakiki jumla ya dira za maji 700,000, ambapo kati ya hizo zilizopitishwa ni dira 570,000
na zilizokataliwa kutokana na kuwa na matatizo mbalimbali ni dira 130,000,” anasema Dk. Manege.
Anasema kuwa Wakala wa Vipimo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusimamia matumizi ya vipimo sahihi katika
ununuzi wa mazao makuu ya kimkakati kama vile pamba, korosho, kahawa na ufuta.
Anaongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kunakuwa na usawa na kuwalinda wakulima wote nchini kwa kuhakikisha
mizani zote zinazotumika katika vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) na vinu vya kuchambulia pamba vinahakikiwa kabla ya kuanza kwa msimu wa ununuzi wa mazao hayo.
Dk. Manege anasema kuwa kwa sasa wanaendelea na ukaguzi wa kushtukiza katika vyama vya ushirika ili kujiridhisha kama mizani zinazotumika zipo kwa usahihi na hazitumiki kuwapunja wakulima.
Anaongeza kuwa marekebisho ya sheria mbalimbali yamesaidia sana kupunguza vitendo vya uchezewaji wa
mizani, kwa kuwa wanaokamatwa kwa kuchezea vipimo hulipishwa faini ya kati ya Sh 100,000 na Sh 200,000.
Anasema kuwa Wakala wa Vipimo umefanikiwa kusaidia waundaji wa ndani wa mizani katika mikoa mbalimbali, kwa
kuwapa ushauri wa kitaalamu ili waweze kuzalisha mizani zenye ubora na imara zinazoweza kumudu ushindani katika
soko la ndani.
Dk. Manege anasema taasisi hiyo imefanikiwa kuwa na wazalishaji (viwanda vidogo) wa ndani wa mizani, ambapo
zaidi ya viwanda vidogo 15 vinazalisha mizani zenye usahihi na ubora na viwanda hivyo vimeweza kutoa ajira kwa
Watanzania wengi hususan vijana.

By Jamhuri