Na Mwandishi Wetu, Bukoba
Wakandarasi walioshinda zabuni ya kutekeleza miradi ya TACTICS Manispaa ya Bukoba yenye thamani ya Sh bilioni 40, wamekakabidhiwa maeneo ya kutekeleza miradi tarajiwa katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Akizungumza na wananchi mapema leo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa ametaja maeneo waliyokabidhiwa kuwa ujenzi wa soko jipya la Manispaa ya Bukoba, Stendi ya Mabasi Kyakailabwa, ujenzi wa kingo za Mto Kanoni zenye urefu wa Kilometa 7.3 pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara kilometa 10.75 ukiambatana na usimikwaji wa taa za barabarani 423
Amesema kuwa miradi hiyo imegawanywa katika makundi mawili ambapo mkandarasi mzawa M/s Dimetoclasa Realhope Limited atajenga soko na Stendi ya Mabasi Kyakailabwa kwa gharama ya Sh bilioni 18.9.
Aidha, Mkandarasi wa Kigemni M/s Shandon Luqiao Group Company Limited atajenga barabara kilometa 10.75, kingo za Mto Kanoni kilometa 7.3 na kuweka taa za barabarani 423 kwa gharama ya Sh bilioni 21.3.
Amesema kuwa matarajio yake ni kuona miradi hiyo inakamilishwa kwa wakati kulingana na mkataba ambapo wamepewa kipindi cha miezi 15 kuanzia Julai 15, 2025 hadi Oktoba 14, 2026.

“Miradi hiyo inatarajia kusisimua wa Manispaa ya Bukoba na mkoa wa Kagera kwa ujumla kwa kutengeneza maelfu ya ajira kwa vijana lakini pia kuwa kivutio kwa wananchi hivyo nawataka wananchi kuhakikisha wanailinda miradi hiyo na kuwapa ushirikiano wakandarasi kufanya kazi yao bila vikwazo vyovyote.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Stephano Byabato ameishukuru serikali kwa kulidhia kutekeleza miradi hiyo ameishukuru serikali kwa kuridhia kutoa fedha za kutekeleza miradi hiyo.
Amesema kuwa kiimekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi kuomba stendi mpya huku viongozi wengi waliopita wakishindwa kutegua kitendawili hicho.
Amesema moja ya ahadi za Chama Cha Mapinduzi katika kutafuta kura za mwaka 2020 ilikuwa ni haadi kwa wananchi kuwa watapata soko la kisasa na stend ya kisasa
Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji 15 ya awamu nyingine zinazotelekeza miradi ya TACTICS lengo likiwa ni kupendezesha miji na kuongeza mapato ta ndani.
