WAKULIMA 2000 WAONGEZA KIPATO KWA UJENZI WA DARAJA LA MIVARF

Wakulima 2000 kutoka vijiji sita vya, Kata ya Kiru Wilayani Babati wameongeza kipato
kutokana na ujenzi wa daraja lililojengwa na Mradi wa Miundombinu ya Masoko,
Uongezaji Thamani na Huduma za kifedha Vijijini (MIVARF), ikiwa ni sehemu ya
malengo ya mradi huo katika kuongeza kipato nchini hususan maeneo ya vijijini.
Wakulima hao wa Kata ya Kiru, inayojumuisha kaya 306, walishindwa kuongeza kipato
kwa takribani miaka 38, tangu mwaka 1978, baada ya Daraja walilokuwa wanatumia
kusombwa na Mafuriko hadi mwaka 2016, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF ilipojenga
Daraja hilo ambalo limeanza kutumika sasa na kuchochea shughuli zao za kiuchumi .
Akiongea na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Mradi wa MIVARF
mara baada ya kutembelea Kijiji cha Masware lilipojengwa Daraja hilo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Babati Hamis Malinga amesema, Serikali kupitia Mradi wa
MIVARF imeweza kuchochea uwekezaji katika kata hiyo
“Kiwanda cha Sukari cha Manyara kimeweza kuongeza uzalishaji kutoka tani 15 hadi
30 kwa siku kutokana na ujenzi wa daraja la kijiji cha Masware ambalo limesaidia
kuboresha biashara baina ya vijiji na kuongeza kipato kwa wananchi. Aidha, Usafirishaji
wa mazao na bidhaa ulikuwa wa gharama kubwa sana lakini kwa jitihada za Serikali ya
Awamu ya Tano kupitia mradi huu tumeweza kuona maendeleo makubwa katika Vijiji
hivi”, alisema Mkurugenzi Malinga.


Kwa upande wa wakulima wa kijiji cha Masware wamesema ujenzi wa Daraja hilo
umeongeza kipato chao kwani wanaweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi pamoja na
vijana wamepata ajira kupitia usafiri wa pikipiki maarufu kama “bodaboda” unaotumiwa
kusafirisha abiria
“Tangu ujenzi wa daraja hili tumeweza kupeleka mazaoyetu katika soko tunalotaka
ambapo awali haikuwa rahisi, wakulima walikuwa wanalanguliwa gunia moja la mahindi
lilikuwa likiuzwa kuanzia shilingi elfu 20,000 hadi 30,000 lakini kwa ujenzi wa daraja hili
wananchi wanaweza kuuza mahindi kuanzia elfu 50,000 hadi 60,000 kwa gunia moja”
amesema Aboubakar Mohamed.

Naye Mkulima wa Kijiji hicho Zena Mpinga ameeleza kuwa, “kabla ya ujenzi wa daraja
hilo wanawake na wamama wajawazito walikuwa wakisafiri kwa shida na kwa gharama
kubwa sana ambapo ukisafiri kwa kutumia pikipiki maarufu kama “bodaboda” ilikuwa ni
shilingi elfu 10,000 kutokana na ukosefu wa kivuko imara na bora na kulazimu
kuzunguka na pikipiki kijiji jirani ila kwa sasa usafiri wa bodaboda ni shilingi elfu 2000
hadi 3000 tu inakufikisha na kuweza kukamilisha mahitaji yako kwa wakati.
Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini (MIVARF), inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kutekelezwa katika
Halmashauri 76 za Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa imegharamiwa na Benki ya
Maendeleo ya Afrika (IFAD) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (ADB) kwa
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

IMETOLEWA NA

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

OFISI YA WAZIRI MKUU