Waliokuwa wafanyakazi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Makao Makuu mjini Moshi na baadaye kufukuzwa kazi kwa tuhuma mbalimbali za ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni 3.4, wameanza kuitunishia misuli serikali.

Wafanyakazi hao ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha, Astery Bitegeko na aliyekuwa Mkaguzi wa Ndani, Issaya Mrema, wamekimbilia Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, wakitaka wasiondolewe kwenye nyumba za TCB.

Hata hivyo umeibuka utata wa kisheria juu ya  Mahakama ya Wilaya ya Moshi kudaiwa kushughulikia madai yanayohusu masuala ya kazi na kutoa amri kwamba nafasi ya Bitegeko isitangazwe wala kujazwa.

Uchunguzi unaonyesha Bitegeko licha ya kufungua madai katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kupinga kufukuzwa kwake kazi, alikimbilia tena mahakama ya wilaya kuweka zuio akiomba asiondolewe kwenye nyumba ya  Bodi ya Kahawa.

Katika maombi yake namba 28/2018, dhidi ya TCB, Bitegeko kupitia kwa wakili wake, Julius Semali, anaeleza kuwa yeye alikuwa Mkurugenzi wa Fedha TCB, nafasi aliyoishikilia kwa miaka tisa.

Anadai Desemba 12, 2018 alipokea barua ya kuachishwa kazi na pamoja na mambo mengine, alipewa siku 30 kuondoka katika nyumba ya shirika iliyopo Kiwanja namba 1481/11 Kilimanjaro Farm.

“Tunaiomba mahakama yako itoe amri ya muda ya kuwazuia wajibu maombi (TCB) kumuondoa muombaji kwenye nyumba hadi shauri lililopo CMA litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” amesema Semali.

Wakili Semali pia aliiomba mahakama itoe amri ya muda ya kuizuia TCB kujaza nafasi yake ya Mkurugenzi wa Fedha mpaka pale shauri alilolifungua CMA litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Katika uamuzi wake, Hakimu Mkazi wa Moshi, Julieth Mawole, alisema kwa kuwa maombi hayo yamewasilishwa kwa ‘chemba samansi’, anaona suala la makazi ni haki ya msingi ya kila mwanadamu.

“Kutafuta nyumbani kwa mtu mwenye familia na hasa mjini si jambo rahisi. Inahitaji muda wa kutosha na kupata nyumba eneo linalofaa kuishi. Muda wa siku 30 aliopewa hautoshi,” amesema Mawole.

“Katika mazingira ya kawaida, naona muombaji (Bitegeko) atapata hasara isiyoweza kufidiwa kama mahakama haitatoa amri ya kuwazuia wajibu maombi (TCB) kumuondoa kwenye nyumba.

“Hivyo amri ya muda inatolewa ya kuwazuia wajibu maombi na mawakala wao kumsumbua au kumuondoa mleta maombi kwenye nyumba anayoishi kiwanja namba 1481/11.

“Mjibu maombi (TCB) anazuiwa kuondoa huduma ya ulinzi katika nyumba hiyo mpaka shauri lililoko CMA litakapomalizika, pia wanazuiwa kuijaza nafasi yake hadi shauri lake CMA litakapotolewa uamuzi,” amesema hakimu katika uamuzi wake.

Wakati Bitegeko akikimbilia Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mrema yeye alikimbilia Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, akiomba amri ya muda ya kuwazuia TCB kumuondoa kwenye nyumba ya shirika.

Naye akapata amri ya kuizuia TCB kumuondoa kwenye nyumba iliyopo Kitalu J, Kiwanja namba 38, Mtaa wa Makongoro, amri ambayo ilitolewa Januari 15, 2019 na Mwenyekiti wa Baraza, T. J. Wagine.

Uchunguzi uliofichua ufisadi na utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh bilioni 3.4 katika bodi hiyo uliagizwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mwaka jana baada ya ‘kunusa’ harufu ya ufisadi katika bodi hiyo.

Kutokana na agizo hilo, Bodi ya Wakurugenzi ya TCB chini ya Mwenyekiti wake, Amir Hamza, ikampa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu ndani ya TCB.

Ingawa taarifa ya uchunguzi wake haijawekwa wazi, lakini inaelezwa ni kutokana na kubaini madudu na wizi wa zaidi ya Sh bilioni 3.4, bodi ya wakurugenzi iliwafukuza kazi Bitegeko, Mrema na wengine wawili.

Wengine waliofukuzwa kazi kutokana na tuhuma hizo za ufisadi wa mabilioni ya fedha ni aliyekuwa mhasibu wa TBC, Goodluck Moshi na Hashimu Mohamed kutoka idara ya uhasibu.

Wanasheria wakosoa uamuzi wa hakimu

Baadhi ya mawakili wa kujitegemea wakiwamo kutoka Mahakama Kuu mjini Moshi wamezungumza na JAMHURI na kukosoa uamuzi uliotolewa na Hakimu Julieth Mawole wakidai kuwa haukuzingatia matakwa ya kisheria.

Mawakili hao walioomba kutotajwa majina yao wamedai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa hakuna shauri lililofunguliwa kwenye mahakama hiyo linalohusu kufukuzwa kazi kwa Bitegeko.

“Kwanza hoja ya zuio kwa mwajiri asimwondoe mfanyakazi kwenye nyumba ya mwajiri ni zuio la ovyo kabisa kuwahi kutolewa na halina miguu ya kusimamia, kwa vile limetolewa na mahakama isiyo na uwezo wa kusikiliza mashauri yahusikanayo na kazi,” amesema wakili huyo.

Amesema kuwa hata amri nyingine za zuio zilizotolewa na Hakimu Mawole pia hazina mashiko ‘machoni’ mwa macho ya sheria kwa vile zimetoka katika mahakama isiyo na uwezo wa kusikiliza mashauri ya kazi.

Wakili mwingine aliyezungumza na JAMHURI amesema ni Mahakama Kuu pekee ambayo inaweza kusikiliza na kutolea uamuzi maombi hayo, huku pia akikosoa kifungu kilichotumiwa na Hakimu Mawole kutoa uamuzi huo.

“Ukiangalia hicho kifungu alichotumia kutoa uamuzi kinahusu vitu ambavyo vinaweza kuharibika, sasa mtu amefukuzwa kazi hapo kuna kitu gani kinaharibika? Isotoshe hauwezi ukatoa uamuzi kwenye shauri ambalo halipo mbele yako,” amesema wakili huyo.

Please follow and like us:
Pin Share