Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Idadi ya waliopoteza maisha kutokana na ajali ya kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam imefika 20.
Hayo yamesemwa leo Novemba 20, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan alipotembelea eneo la ajali kujionea hali halisi na kutoa pole kwa wafanyabiashara walioathirika na tukio hilo.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Rais Samia amesema; ”Tatizo limetupa ujumbe wa usalama wa watumiaji wa majengo Kariakoo, jengo halikujengwa vizuri”.
Amsema ameangalia nondo, na baadhi ya kuta, ameona wazi jengo halikujengwa kwa viwango.
Rais Samia amesema kuwa zoezi la kusafisha eneo hilo litaendelea; kuondoa mizigo na mali za wafanyabiashara lakini wasafishaji watakuwa wakitafuta pia miili ambayo kwa namna moja au nyingine haikuwa imepatikana, kisha itasitiriwa kwa heshima zote.
Amesema mali zotakazotolewa hapo zitahifadhiwa sehemu, kisha baadaye wenye mali wataitwa kuzitambua.
Rais ameahidi taarifa ya Tume iliyoundwa itawekwa wazi, na kwamba mapendekezo yote yatafanyiwa kazi, ikiwa ni pamoja na kubomolewa kwa majengo yote yatakayothibitika kuwa chini ya viwango na hatarishi kwa watumiaji.
Amezitambua taarifa za tume zilizopita zilizohusu majengo na mpangilio wa Kariakoo. Amesema zitatumika pia kuongezea uelewa wa kazi ya Tume hii mpya iliyoundwa.
Pia ameruhusu biashara ziendelee kwenye mitaa mingine kadhaa iliyokuwa imefungwa, isipokuwa huo mmoja ambao jengo limeanguka kuwezesha wasafishaji wafanye shughuli zao vizuri na kuepuka ajali kwa umma.