Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
JUMLA ya wanachama 153 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama ili kuwania ubunge wa jimbo na viti maalumu katika Mkoa huo wenye jumla ya majimbo 12 ya uchaguzi.
Akiongea na vyombo vya habari jana Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa huo Idd Moshi amesema kuwa jumla ya wanaCCM waliojitokeza kutia nia ya ubunge katika majimbo 12 ni wanaume 136 na wanawake 17, mmoja hakurejesha fomu.
Kwa nafasi za ubunge wa viti maalumu, amesema kuwa jumla ya wanawake 21 wamechukua fomu kupitia Jumuiya ya Wanawake (UWT), na kupitia Jumuiya ya Wazazi ni mwanamke 1 aliyechukua fomu.

Aidha kwa nafasi ya uwakilishi wa Vijana, Mwenezi amesema kuwa jumla ya akinadada 2 wamejitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha ili kuomba kuwakilisha vijana wa mkoa huo.
Kwa nafasi za udiwani, ameeleza kuwa jumla ya wanaCCM 1,220 wamejitokeza kuomba kupeperusha bendera ya CCM katika kata zote 203 zilizopo katika Mkoa huo huku akinamama 243 wakiomba nafasi za udiwani wa viti maalumu.
Mwenezi amebainisha kuwa zoezi la uchukua na urejeshaji fomu limeenda vizuri kama ilivyopangwa na hapakuwa na changamoto yoyote, alibainisha kuwa mwaka huu waliotia nia wote wana sifa na vigezo vinavyotakiwa kwenye uteuzi.

‘Zoezi linalofuata sasa ni vikao vya awali vya uchujaji wagombea, kisha kuteuliwa majina matatu ambayo yatarudishwa ili kupigiwa kura na wanaCCM, najua vikao vitapata wakati mgumu, lakini kwa kuwa CCM ni chama imara, sina shaka, haki itatendeka na tutapata wagombea sahihi’, amesema.
Amewataka wanaCCM wote kuendelea kuwa watulivu na kudumisha umoja na mshikamano wao katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, Oktoba 25 mwaka huu ili kupata ushindi wa kishindo.
