Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

Wahitimu zaidi 130 wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Milambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa Tabora wametimuliwa baada ya kuleta vurugu na kutishia kuchoma majengo ya shule hiyo.

Uamuzi huo umechukuliwa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha baada ya kupewa taarifa ya uwepo wa vurugu katika shule hiyo ambapo inadaiwa wanafunzi hao walichukizwa na hatua ya uongozi wa shule hiyo kusitiza sherehe ya mahafali yao.

Akiongea na wanafunzi hao baada ya kupokea taarifa ya mienendo ya wanafunzi hao alieleza kusikitishwa na tabia ya utovu wa nidhamu ambayo wamekuwa wakiionesha kwa walimu wao ikiwemo kutishia kuharibu miundombinu ya shule.

Alisema kuwa serikali inajali sana ustawi wa shule ndiyo maana imeleta mabilioni ya fedha kwa ajili kuifanyia ukarabati mkubwa ili kuboreshwa miundombinu yake yote, ila akaonesha kukerwa na tabia zao za utovu wa nidhamu za mara kwa mara.

 ‘Tabia hizi zinakera sana, hatuwezi kuzifumbia macho hata kama mpo kidato cha sita, wale wote waliohusika kwenye vurugu na kutaka kuchoma moto shule hii waondoke mara moja hapa shuleni, hatua zingine za kinidhamu zitafuata’, alisema.

RC Chacha alifafanua kuwa wanafunzi walioleta vurugu ni wale waliomaliza mitihani yao hivyo akauagiza uongozi wa shule hiyo kuwaondoa mara moja wanafunzi wote wa kidato cha 6 kila mmoja arudi nyumbani kwao.

Awali akitoa taarifa ya vurugu hizo Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa hiyo Benjamin Sipalito, alisema kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakionesha vitendo vya utovu wa nidhamu ikiwemo kumiliki simu za mkononi kinyume cha utaratibu.

Vitendo vingine ni kutoroka bweni na kwenda mitaani bila ruhusa, kuandaa sherehe isiyoidhinishwa na uongozi wa shule na kuhamasisha wenzao kufanya vurugu ikiwemo kupanga njama ili kuchoma shule hiyo.

Alisisitiza kuwa vitendo hivyo havikubaliki na wamekuwa wakionywa mara kwa mara ila wanakaidi, hivyo akaomba hatua zichukuliwe kwa kundi lote lililohusika kabla ya kusababisha madhara makubwa zaidi shuleni hapo.  

Baada ya taarifa hiyo Mkuu wa Mkoa aliagiza uongozi wa shule kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwaondoa mara moja wanafunzi wote wa kidato cha sita waliohusika katika vurugu hizo wakati taratibu zingine za uchunguzi zikiendelea, agizo hilo lilitekelezwa mara moja.