Wanajeshi wa Congo wakiwa na mchanganyiko wa nguo za kijeshi na za kawaida, walijaa kwenye kanisa wiki iliyopita kujibu mashtaka ya uhalifu ikiwa ni pamoja na ubakaji na mauaji yanayodaiwa kufanywa walipokuwa wakikimbia waasi wa M23.
Kauli zao wakati wa kesi hiyo katika mahakama ya kijeshi zinaonyesha kushindwa kwa jeshi ambalo sasa limepoteza maeneo mengi mashariki mwa Congo kutokana na wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kusonga mbele.
Machafuko ya wiki chache zilizopita yamezidi kuzorotesha jeshi dhaifu la Congo, na kuongeza hatari za vitendo vya dhuluma dhidi ya raia, inasema hati ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na Reuters.
Wakati serikali ya Rais Felix Tshisekedi akipongeza juhudi za kuajiri wanajeshi wapya na kupata silaha mpya, ushuhuda kutoka kwa maafisa wakuu wanasema, hilo halina maana kwa askari walio mstari wa mbele, ambao wanalipwa ujira mdogo na wasio na vifaa vya kutosha.
“Tunakosolewa lakini tunateseka kama watu wengine,” alisema kanali mmoja ambaye wanajeshi wake wamepigana katika jimbo la Kivu Kusini.
Katika kesi za Musienene wiki iliyopita na katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bukavu mapema mwezi Februari, waendesha mashtaka wa kijeshi walisikiliza mashtaka yakiwemo wizi, uporaji, unyang’anyi na kupoteza silaha.
Wengi wa washtakiwa walikiri kuwa baadhi ya askari walifanya uhalifu huo lakini wao wenyewe wakakanusha kuhusika.
