Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wamekumbushwa umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa wote ili kujiweka tayari pindi wanapougua wao au ndugu zao ambao ni wanufaika wa bima hiyo, hatua itakayosaidia kuepuza gharama kubwa za matibabu.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH), Dkt. Leonard Subi, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Dkt. Subi alisema Mfuko wa Bima ya Afya umeweka utaratibu maalum unaowajumuisha pia viongozi katika maeneo wanayotoka ili kusaidia kuhamasisha wananchi kujiunga na bima hiyo muhimu kwa ustawi wa afya zao.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ambapo Serikali inaendelea kwa kasi kuwatambua na kuwasajili watu na makundi maalum ambayo hapo awali yalitambuliwa na sera ya afya kuwa yanastahili msamaha wa matibabu.
“Ni muhimu wananchi kufahamu kuwa kiuhalisia hakuna huduma ya matibabu iliyo bure, bali kuna mtu au Serikali inayogharimia huduma hiyo. Hivyo, kuwa na Bima ya Afya ni njia bora ya kujihakikishia matibabu kwa wakati,” alisema Dkt. Subi.
Aidha alisema kuwa uzalendo na utu ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Bima ya Afya kwa Wote, hatua itakayowapa wananchi uhakika wa matibabu na kupunguza kwa kiasi kikubwa adha ya gharama za matibabu, kwani ugonjwa unaweza kutokea wakati wowote.
Vilevile alisema Bima ya Afya kwa wote siyo jambo la kusubiri uugue ndiyo Ujiunge bali ni Kujiunga Kabla hujaugua lengo likiwa ni kuchangiana wakati au pindi mtu anapougua na hivyo kupatiwa huduma ya afya ambayo ni haki ya msingi kwa kila mtu bila kikwazo cha fedha.
Alisisitiza Sekta Binafsi, Vyama vya Ushirika, Vikundi mbalimbali vya kijamii kuwalipia wanachama au wafanyakazi wao na familia zao kwa utaratibu wanaokubaliana.

