Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Magu

Wananchi wa vijiji vitatu vya Chandulu, Salama, Mwabulenga vilivyopo kata ya Ng’haya wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza wameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kuwapimia na kuwamilikisha maeneo yao kwa kuwapatia Hati za Hakimilki za Kimila.

Zoezi hilo la kuwapatia Hati za Hakimilki za Kimila limefanyika baada ya kufanyika mipango wa matumizi ya ardhi pamoja na upimaji ardhi katika vijiji hivyo vitatu.

Mipango ya Matumizi ya Ardhi huwekwa katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha usalama wa umiliki wa ardhi, kukuza matumizi endelevu ya ardhi pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi.

Wananchi wa vijiji hivyo wametoa kauli hiyo tarehe 26 Septemba 2025 katika kijiji cha Chandulu wilayani Magu wakati wa zoezi la kutoa hakimilki za kimila kwa wananchi waliomilikishwa maeneo yao.

Jumla ya Hati za Hakimilki za Kimila 1,415 zimeandaliwa huku takriban hatimilki 5000 ukamilishaji wake ukiendelea ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga alikabidhi Hati za Hakimilki za kimila 50 kwa niaba ya wannachi wote waliomilikishwa.

Wananchi hao wamesema, wanajisikia furaha kubwa kumilikishwa maeneo yao waliyoyaelezea kuwa sasa umilikishaji wake umeongeza thamani ya maeneo hayo.

“Najisikia vizuri sana kwa sababu ardhi yangu nimemilikishwa kwa hati na sitokuwa tena na uharaka wa kuiuza, niipongeze sana serikali kwa uamuzi wake huu wa kutumilikisha” amesema mkazi wa Chadulu Bw. Mashiku Machunge.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amewataka wananchi waliokabidhiwa Hati za Hakimilki za kimila kuhakikisha wanazitunza na kuacha tabia ya kuuza ardhi hovyo ili ziweze kusaidia vizazi vijavyo.

“Ndugu wananchi hati hizi inatakiwa mzitunze kwa sababu huu ni urithi wenu, ardhi hii ni ya kwenu mzitunze na pili tusiwe na tabia ya kuuza ardhi, ardhi tuitunze itusiadie sisi, watoto wetu, wajukuu zetu na watakaotufutia katika vizazi vyetu” amesema.

Ametaka hati milki walizokabidhiwa wananchi zilete mabadiliko ya kimaisha kwa kuwa mbali na kuwatambulisha kisheria lakini zinasaidia kupata mikopo na kueleza matarajio ya serikali ni kwamba pawepo matokeo chanya ya kimaendeleo na kusisitiza kuwa hati hizo zisiwe sehemu ya migogoro ya kudhulumiana.

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Bw. Wilson Luge ameeleza msingi mkubwa wa ofisi yake ni kuhakikisha wanawamilikisha wananchi maeneo yao kwa kuwapatia hati milki kwa kuwa ardhi ni rasimali itakayowawezesha kiuchumi.

“Ndani ya mkoa wa Mwanza katika halmashauri zote sita tutashirikiana na kampuni za upimaji kuhakikisha ardhi za wananchi wetu zinapimwa na kuwapatia hati zikiwemo hizi Hati za Hakimilki za kimila bila kuwacheleweshea” amesema Luge.

Zoezi la upimaji maeneo katika wilaya ya Magu limefanywa kwa ushirikiano na kampuni za upimaji za GMS Geo tech Consultancy Co.Ltd, GNT Property Ltd na CAIWAY Company Ltd ambazo zinatekeleza mazoezi katika vijiji 16 kati ya vijiji 82 vilivyoko ndani ya Wilaya ya Magu.