Tumetafakari kwa kina juu ya taarifa zinazolaumu “Serikali kubariki ufisadi wa UDA.” Lawama hizo hutolewa na Watanzania wachache sana wanaopinga Kampuni ya wazawa ya Simon Group kuuziwa hisa za UDA.

Hoja za msingi malalamiko hayo ni kwamba Simon Group haikufuata taratibu na sheria, na pia kwamba haikuzingatia thamani halisi ya shirika hilo. Tunachofahamu sisi kwa sasa ni kwamba uuzwaji huo uko sahihi na hakuna kinachoweza kubadilika, kwani taratibu na sheria zote zilizingatiwa kikamilifu wakati wa uuzaji wa hisa za UDA kwa Simon Group.  

Hoja kwamba Baraza la Mawaziri halikuhusishwa au kwamba hapakuwa na mwakilishi wa Serikali wakati wa ubinafsishaji huo, bila shaka watoa hoja hawafahamu juu ya sheria na taratibu wakati wa ubinafsishaji wa UDA.

Tunachofahamu ni kwamba uamuzi kuhusu ubinafsishaji wa UDA ulifuata na kuzingatia kikamilifu ‘Memorandum and Articles of Association‘ ya shirika hilo. Ikumbukwe kuwa UDA imesajiliwa na Mamlaka ya Usajili wa Makampuni (BRELA) kama kampuni chini ya Sheria ya Makampuni (Cap. 212). Ifike hatua Watanzania waelewe kuwa uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuuza hisa zake kwa Kampuni ya Simon Group ulikuwa haukwepeki.

UDA ilikuwa na hali mbaya ya fedha kabla ya kuuzwa kwa Simon Group. Haikuwa na uwezo wa kuendelea kusimama, kujiendesha na wala Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hawakuwa na uwezo wa kulikwamua kutoka kwenye matatizo ya kifedha yaliyokuwa yakiikabili.  Tangu mwaka 1985 wakati Serikali ilipoipa Halmashauri ya Jiji asilimia 51 ya hisa za Shirika la UDA, Halmashauri haikuwekeza mtaji wowote ndani ya UDA, na kadhalika Serikali haikuendelea kutoa fedha kulisaidia shirika hilo, na tangu wakati huo UDA imekuwa ikipata hasara kubwa na kudidimia kiuchumi.

Hadi kufikia Juni, 2010, UDA ilikuwa na limbikizo la hasara ya Sh 2,566,468,229 hivyo kulifanya shirika lianze kudidimia na kukosa uwezo wa kutimiza malengo yake ya kutoa usafiri bora na wa uhakika kwa wananchi wa Dar es Salaam. Simon Group wameonesha kwa vitendo dhamira yao ya kulifanya Shirika la UDA litekeleze majukumu yake kikamilifu, wameonesha dhamira yao ya kuwapatia wananchi wa Dar es Salaam usafiri bora na wa uhakika zaidi.

Mpaka sasa, Simon Group tayari wameshanunua mabasi zaidi ya 400 ambayo yapo barabarani jijini Dar es Salaam yakihudumia wananchi na mengine 600 yanaendelea kutengenezwa viwandani huko India na China. Umefika wakati sasa Watanzania tuelezane ukweli. Watanzania wanapaswa kutambua ukweli kuwa shida ya wananchi wa Dar es Salaam siyo nani anamiliki UDA. Shida ya wananchi wa Dar es Salaam ni usafiri bora na wa uhakika.

Wananchi wa Dar es Salaam wanataka kuona adha ya kugombea usafiri nyakati za asubuhi wanapokwenda kazini na jioni wanaporejea nyumbani inakoma mara moja. Wanataka kuona watoto wao hawasumbuliwi tena na makondakta wanapokwenda na kurudi shuleni, wanataka kupanda basi kwa wakati wanaotaka na kufika makazini kwa wakati.

Ndiyo maana tunahoji wanaopinga uuzwaji wa UDA walikuwa wapi wakati shirika hilo lilipokuwa hoi kifedha na kuelekea kufilisika? Walikuwa wapi wakati UDA ikiwa imechoka na kushindwa kununua mabasi mapya na kubaki na mabasi manne tu tena machakavu na hivyo kushindwa kuwahudumia wananchi? Walikuwa wapi wakati UDA ikiwa taabani kifedha kiasi cha kushindwa kujiendesha na kuwalipa wafanyakazi wake na kuamua kuuza au kukodisha baadhi ya mali na rasilimali zake kwa wafanyabiashara wa kigeni, ambao baadaye walitaka kuuziwa shirika?

Kwanini watu hawa hawakuanzisha kampeni maalum wakati huo ya kuichangia UDA ili ikuze mtaji wake na iweze kujiendesha? Wanapata uzalendo leo wanapoiona UDA inanawiri baada ya kuchukuliwa na mwekezaji mwenye mapenzi ya kweli kwa nchi yake na Watanzania wenzake?

Tunachokiona sisi ni kuendelea kwa tabia dhaifu za baadhi ya Watanzania — kupigana vita wenyewe kwa wenyewe kwa kuwanufaisha wageni. Kelele zote hizi zinazopigwa kuhusu uuzwaji wa UDA zinatokana na ukweli kuwa aliyenunua ni Mswahili, Mtanzania mweusi ambaye kwa mtazamo wa wafanyabiashara wa kigeni, hastahili kumiliki uchumi wa nchi yake.

Ni vema watu wenye fikra kama hizo wakatambua kwamba Serikali zote makini duniani, zinawapa kipaumbele kwanza wananchi wake na wageni huangaliwa baadaye.

By Jamhuri