Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Wito umetolewa kwa Wanawake kujiamini na kujipambanua kitaifa na kimataifa kwenye kusimamia ajenda za maendeleo yenye usawa wa kijinsia na kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito huo wakati wa hafla ya kumkabidhi Balozi Dkt. Getrude Mongella Tuzo ya Heshima, iliyofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 18, 2023.

Tuzo hiyo iliyotolewa na Umoja wa Wanawake wa nchi Huru za Afrika (PAWO-Africa) Julai 31, 2022 nchini Namibia, lengo lake ni kutambua mchango wa Balozi Getrude kwenye uongozi wa ngazi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo kuwa rais wa utetezi wa wanawake Afrika na rais wa kwanza wa Bunge la Afrika.

Vilevile, Balozi Getrude amekuwa Mshauri Mwandamizi na Katibu Mtendaji wa Kamisheni Uchumi ya Afrika katika masuala ya Jinsia, Mlezi wa Asasi za Kiraia zisizo za Kiserikali pamoja na kusimamia Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Wanawake Jijini Beijing nchini China Septemba, 1995.

Waziri Dkt Gwajima amempongeza Mhe. Balozi Getrude kwa ujasiri na uthubutu wake kwenye kutoa mchango wake kwa maendeleo ya wanawake na kuhimiza kuwa, mafanikio haya yakawe chachu kwa Wanawake wengine wote kujiamini kusimamia ajenda za maendeleo ya wanawake.

Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amewahakikishia Wanawake kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan tayari ameweka mazingira mazuri kwa Wanawake wote wenye mchango kwenye safari ya maendeleo yenye usawa wa kijinsia kuendelea kusimama kwenye nafasi zao ikiwemo, kwenye kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto.

Kwa upande wake Balozi Getrude ameshukuru kwa kutambuliwa kwake ambapo amesema, utambuzi huo ni kwa ajili ya wanawake wote walioshiriki kupigania haki za wanawake tangu kuundwa kwa PAWO mwaka 1965.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda amempongeza Balozi Getrude na kutoa wito kwa Wanawake wote kuunganisha nguvu na kuelekeza juhudi zao kwenye kupambana kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa Watoto.

By Jamhuri