Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baadhi ya wanawake waliopo katika vyombo vya ulinzi na usalama wameshiriki Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Wabunge Wanawake wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) unaofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIC) jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Suzan Kaganda, Mkurugenzi wa Kanda wa AFUTA International Alliance kutoka Kenya, Betty Mutesi na Mwakilishi wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania, Luteni Kanali Shani Masasi, wameshiriki mdahalo wakati mkutano huo ukiendelea kufanyika.

Mkutano huo umeanza Novemba 2-5, 2026 na umefunguliwa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akifungua mkutano huo, Ndejembi, amesema wanawake ni viongozi, wapatanishi na wajenzi wa amani, hivyo ni muhimu kuondoa mila kandamizi, ubaguzi na vikwazo vya kiuchumi vinavyopunguza ushiriki wao.

Amesisitiza kwamba Tanzania inaendelea kuwawezesha wanawake kupitia fursa za uongozi, elimu, masoko, mitaji na mikopo yenye masharti nafuu.

Kwa upande wake, Rais wa Jukwaa la Mabunge la Ukanda huo na Spika wa Bunge la Angola, Adão de Almeida, amesisitiza ushiriki kamili wa wanawake katika kujenga amani ya kudumu.

Mkutano huo unahudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Judith Tuluka, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia, Rais wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Beijing wa Mwaka 1995, Balozi Dk. Gertrude Mongella na Spika mstaafu, Anne Makinda.

Pia unawakutanisha maspika, wabunge, mawaziri, mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, washirika wa maendeleo na asasi za kiraia.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ukanda wa Maziwa Makuu Wenye Amani na Maendeleo.”